Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nikipongeze Chama changu cha Mapinduzi ambacho kwa kweli wametuandalia Ilani hii ya Uchaguzi ambayo ukiisoma inaenda kuondoa kero kubwa za wananchi wetu. Kwangu mimi Ilani hii ni mkataba kati ya Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Mbagala. Ndiyo maana wakati wa uchaguzi wananchi wa Jimbo la Mbagala walikipa kura nyingi Chama cha Mapinduzi kwa maana waliisoma Ilani hii na wakailewa vizuri. Kwa hiyo, niwashukuru wale wote walioandaa Ilani hii ya Uchaguzi wakiongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wetu Dkt. Bashiru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisoma hii Ilani ya Uchaguzi kwenye ukurasa wa 78 kipengele cha (e) wamezungumzia kuhusu kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Vipo vitu vingi vimeorodheshwa huku ambavyo vinaelekea kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, lakini katika jimbo langu la Mbagala, ukienda katika kipengele cha tatu kimezungumzia upanuzi wa barabara wa Mbagala - Kongowe - Mwandege, kilometa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanini Chama cha Mapinduzi wameleta Ilani na ameelezea barabara hii? Barabara hii ni kiungo muhimu. Ukiangalia watu wanaotoka Kigamboni, Tuangoma ni lazima wapite katika kipande hiki cha barabara. Pia watu wote wanaotoka kusini, ukianzia Lindi, Mtwara, Songea, Mkuranga na Rufiji, wakitaka kuingia Dar es Salaam, lango lao la kuingilia ni kipande hiki cha barabara kilichozungumzwa. Kwa hiyo, Chama cha Mapinduzi kimeweka hili wakijua wanaenda kuokoa na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ukishafika pale Rangitatu, kwa wale wanaotakiwa kwenda Mbande mpaka Airport wanafika. Kwa hiyo, kipande hiki kidogo cha barabara kikijengwa, kinaenda kupunguza msongamano wa magari katika ya Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote mtakuwa mashahidi, kaeneo hako ka kilometa nne kanasababisha msongamano wa magari, kukapita hako ni zaidi ya masaa matatu ili lipitike eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, namshukuru Rais wangu pamoja na Serikali yake, wameliona hili na wamezingatia Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi. Ukienda katika hotuba ya Waziri, ukifungua randama katika ukurasa wa 134 kiambatanisho cha tatu wamezungumzia pale kuhusu upanuzi wa barabara Rangitatu - Kongowe mpaka Mwandege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile barabara hii kama nilivyosema huko mwanzo, ukurasa huo huo wamesema upanuzi wa Barabara ya Chanika mpaka Mbande. Vile vile ukurasa huo wamezungumzia upgrading ya barabara ya Mbagala Mission - Kijichi na Zakhem. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme nini Rais wetu, Mama Samia amezingatia Ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi na ameitafsiri kwa vitendo kwa kutuletea bajeti hii hapa. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi iliyobaki sasa ni kwa Watendaji wa Wizara na Mawaziri. Sasa kama kweli tuna nia ya dhati ya kumsaidia Rais; ambaye ametokana na Chama cha Mapinduzi, ambapo kwenye Ilani yake wameelezea; Rais ametuletea bajeti na ameiweka katika randama ya Mheshimiwa Waziri. Sasa watendaji kazi yenu kubwa iliyobaki sasa ni kwenda kutekeleza kwa vitendo barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hizi ili zitekelezwe inahitajika ifanyike fidia kipande cha kutoka Kokoto - Kongowe mpaka Mwandege. Wananchi wale zaidi ya 3,000 wamekuwa wakisubiria fidia zaidi ya miaka mitatu sasa na kila nikiuliza swali hapa Bungeni Waziri anajibu, barabara itajengwa baada ya fidia kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, leo tunapitisha bajeti, Chama cha Mapinduzi wameandika kwenye Ilani kupunguza msongamano. Rais, mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametuwekea kwenye bajeti tunapitisha, bado hatujaona fedha za kufanya fidia za hizo barabara. Sasa nataka nimwone Waziri hapa anatuletea majibu, wananchi hawa ambao wameteseka kwa zaidi ya mitatu kusubiri fidia, ni lini wanafidiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kipande cha barabara sasa kutoka Mbande mpaka Msongola kipande kile kimebaki kilometa nne tu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, watumalizie kile kipande, ndiyo tunaenda kuondoa ile dhana ya msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna kipande cha barabara ambacho huku mmekiandika kutoka Kijichi - Mission mpaka kuja Zakhem. Mheshimiwa Waziri kipande hiki mmeandika, lakini tunataka tujue hapa mkituletea taarifa mwisho wakati mnajumuisha, pale chini kuna bomba la TAZAMA. Lile bomba la TAZAMA tunatatuaje ile changamoto ili tuweze kujenga ile barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na mradi wa mabasi yaendayo kazi Dar es Salaam (DART). Mheshimiwa Waziri atakuwa shahidi, alifanya ziara katika jimbo langu, wananchi wa Mbagala katika eneo ambalo limepita mradi, barabara imejengwa na maji yote sasa yanaeleke kwa wananchi. namwomba sana Mheshimiwa Waziri atuletee majibu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)