Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa fursa hii ya kuchangia Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Kwanza nianze kumshukuru Waziri mwenyewe, Naibu Waziri na timu yote nzima ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kuwa wasikivu na kuwasilikiza Waheshimiwa Wabunge wanapokuwa wanakuja na hoja za wananchi. Mwenyewe ni shuhuda nimekutana na Mheshimiwa Mbarawa kwenye boti tena nilikuwa sijamuona, alivyoniona yeye akaniita, akasema hebu niambie barabara zako zina hali gani, tukazungumza pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iendelee na tabia hiyo, iendelee kuwapokea Wabunge, kuwasikiliza na kupokea changamoto za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lipo mpakani. Linapakana na land lock de-countries za Rwanda, Burundi lakini kuna mataifa ya jirani ya DRC Kongo pamoja na Sudani ya Kusini. Ukaribu huu wa mataifa haya umesababisha mataifa haya kuendelea ku-rely kwenye bandari ya Dar es Salaam. Kuagiza mizigo yao kutoka bandari ya Dar es Salaam kupitia barabara inayopita hapa Dodoma kwenda mpaka Ngara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Ngara tuna mipaka mikubwa mitatu. Upo mpaka wa Lusumo, Kabanga pamoja na Mlukasagamba. Kipande cha barabara inayotoka Rusahunga kwenda mpaka Lusumo kilomita 92 kimeharibika sana. TANROADS na Wizara ya Ujenzi wamejitahidi kufanya periodic maintenance lakini kutokana na magari yanayopita pale kuwa na uzito mkubwa, barabara ile huwa inaharibika mara kwa mara kutokana na uzito wa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake wafanyabiashara wa DRC Kongo, Ruanda na Burundi wanaamua kuahirisha kutumia barabara yetu na bandari yetu ya Dar es Salaam wanakimbilia kutumia bandari za Beira – Mozambique pamoja na bandari za Mombasa – Kenya. Sasa kama Taifa tunapoteza mapato makubwa kutokana na kipande hiki cha kilomita 92 kutotengenezwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nichukue fursa hii kuiomba Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuweka kipaumbele namba moja kuhakikisha kipande cha kilomita 92 kutoka Rusaunga mpaka Lusumo kijengwe kwa lami na kwa viwango vya kimataifa. Kwa kufanya hivyo tutawapa confidence wafanyabiashara wa mataifa niliyoyataja kuendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam na matokeo yake kama Taifa tutaendelea kupata mapato yanayotokana na biashara ya usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la barabara kutoka Rusumo mpaka Rusaunga lina center mbili. Ipo center ya Rusomo na center ya Benako. Ninaiomba sana Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na nimeshateta na Injinia wa TANROADS pamoja na Mkurugenzi wake kwamba eneo la Benako twende tufunge taa za kisasa pale barabarani kwa sababu inapofika usiku magari yote ya mizigo yanapaki pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile eneo la Rusumo tukafunge taa za barabarani, Ngara Mjini pamoja na mpaka wa Kabanga. Ninaomba jambo hilo Mheshimiwa Mbarawa uli-note ili liweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kaya 154 za Ngara ambazo zipo kandokando ya kipande cha kilomita 92 cha kutoka Rusaunga mpaka Rusumo. Kaya hizo zinatakiwa kupewa fidia wakati ujenzi utakapoanza. Nikuombe Mheshimiwa Mbarawa, hawa watu wanaolipa fidia kipindi kingine wanatuma pesa tu hata kipindi ambacho akaunti ziko dormant matokeo yake nimekuwa nikipata shida sana kushughulikia wananchi wenye kero ambao malipo yao yamebaunsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Mbarawa na timu nzima ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha kwamba wananchi wangu hawa kaya 154 zinalipwa vizuri kwa wakati na sitegemei kuona changamoto yoyote katika mchakato huo wa malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Jimbo la Ngara tunamshukuru Mwenyezi Mungu ametujalia kuwa na madini aina mbalimbali, nickel, cobalt, tungsten, manganese na mengine yote in Samia’s voice. Madini haya yanapatikana Lulenge ambako kuna barabara ya muda mrefu sana ambayo watangulizi wangu kwa miaka 10 wamekuwa wakiisemea bila mafanikio. Iko barabara ya kutoka Mrugalama kwenda Rurenge mpaka Kumbuga kilomita 75 na yenye kaya 1,122 za wananchi ambazo zimefanyiwa tathmini kwa ajili ya kupewa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii nimeililia muda mrefu sana. Nimekusumbua Kasekenya kwa muda mrefu sana. Nimemsumbua Profesa Mbarawa. Leo hii ninakuomba Mheshimiwa, Profesa mwana wa Mbarawa, Mheshimiwa Waziri unisaidie sana nipate fedha nianze kujenga kipande hiki cha barabara kwa lami. Bila kujenga kipande hiki cha barabara haya madini hayataweza kusafirishwa. Tunatarajia mgodi wa Tembo Nickel uweze kuchangia kwenye National GDP Trilioni 17 mpaka Trilioni 20, hii ni fedha kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitashangaa sana kuona Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wanatoa vipaumbele kwenye barabara za kusafirisha sijui mazao gani huko, viazi wakati sisi tunatakiwa kusafirisha nickel na hayo madini mengine niliyoyataja ili tuweze ku-inject kwenye National GDP Trilioni 17 mpaka Trilioni 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbarawa utajiuliza, hivi ungekuwa wewe utaenda kujenga barabara wapi. Lazima utoe kipaumbele na nikuombe Mheshimiwa Mbarawa tunaomba barabara yetu ya Mrugalama, Rurenge mpaka Kumbuga kilomita 75 uipe kipaumbele ili tuweze kujenga uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko barabara ya kutoka Rurenge kwenda Tembo Nickel kilomita 34 na barabara hii mwaka jana nimepambana sana, nimeshirikiana na Wizara tumefanikiwa kufanya tathmini, tumefanya detailed design na tumefanya tathmini ya wananchi takribani 600 ambao wanatakiwa kupewa fidia. Barabara hii ndiyo inayokwenda moja kwa moja mpaka kwenye mgodi wa Nickel.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama barabara hii haitotengenezwa hizi nickel tutashindwa kuzisafirisha na nyote ni mashuhuda kwamba nickel imepanda thamani kubwa sana kwenye soko la dunia na ni muda muafaka sasa kutengeneza kipande hiki cha barabara Mheshimiwa, Waziri, Profesa mwana wa Mbarawa, ili nickel hizi tuweze kuzisafirisha tuweze kuzileta kwenye kiwanda cha uchenjuaji Kahama na baadae kuzipeleka Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kipande kingine cha barabara cha kutoka Mzani mpaka Mrusagamba kilomita 32. Hiki kipande ni muhimu sana kwa ajili ya kuunganisha Tanzania na upande wa Burundi ya Kusini. Ninakuomba sana Mheshimiwa Makame Mbarawa uweze kutoa kipaumbele kwa barabara hii ili iweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyosema Jimbo la Ngara ni Jimbo la kimkakati, liko mpakani na nimeona kwenye mpango wa Serikali kuna mpango wa kujenga kipande cha SGR kutoka Isaka kwenda mpaka Lusumu ili bidhaa na makontena ya wafanyabiashara kutoka mataifa niliyoyataja yatakapokuwa yanafika pale Isaka basi kipande hicho cha reli ya SGR kiweze kutumika kupeleka bidhaa hizi mpaka Kigali – Rwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri uweke kipaumbele kwenye kipande hiki cha barabara kwa sababu tunapokijenga kuelekea Rwanda tutawezesha mataifa ya Sudani ya Kusini pamoja na DRC Kongo kuweza kuagiza migizo yetu kutoka bandari ya Dar es Salaam kupitia SGR. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utoe kipaumbele kwenye eneo hili.

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ndaisaba.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie. Ninakushukuru sana. ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)