Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi. Niungane na wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu Mtwara tuna barabara moja ya kutoka Mtwara - Mingoyo mpaka Masasi. Barabara hii ni barabara ambayo inaunganisha kiuchumi hasa ukizingatia sasa makaa yote ya mawe kutoka Liganga na Mchuchuma yanapita katika barabara ile, lakini barabara ile ni chakavu sasa. Kwa mpango uliopo tulikuwa tunaelezwa, kwamba barabara ile iko mbioni kupatikana fedha, nimwombe Mheshimiwa Waziri afanye kila njia na namna fedha ipatikane kwa haraka, tuanze ujenzi kwa sababu barabara hiyo ni barabara muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru pia Serikali kwa kutujengea Bandari ya Mtwara ambayo imepanuliwa kwa kiasi kikubwa. Nataka niishauri Serikali tunapozungumza maendeleo yoyote ndani ya nchi, hatuwezi kuiacha bandari, lakini Bandari ya Mtwara mpaka sasa hivi hakuna njia mbadala ya kuweza kuitumia wakati Serikali imewekeza pale zaidi ya bilioni 157. Sasa ombi langu na ushauri kwa Serikali, tunazo nchi jirani ambazo zinaweza zikaitumia kwa ufasaha sana Bandari ya Mtwara, wenye mamlaka niwaombe tufanye mazungumzo ya haraka sana kuinusuru bandari ile ili iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari yetu ya Dar es salaam kwa sasa ukiangalia kwa kweli imezidiwa kwa kila namna. Bandari ile kina kona unavyotaka kuingia imeelemewa na vitu vingi hasa mizigo na vitu vingine. Tuielekeze sasa Bandari ya Mtwara, twende tupanue wigo, watu wa Malawi, Zambia waitumie Bandari ya Mtwara. Ukizungumza kutoka Zambia kuja Dar es Salaam lakini ukizungumza kutoka Zambia kuja Mtwara, Mtwara ni karibu zaidi kuliko Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, isitoshe katika mikoa yote ambayo sasa hivi ina maendeleo tukizungumza Arusha, kuna mpaka wa Namanga, lakini tukizungumza Mbeya kuna mpaka kule Mbeya. Kwanza niishukuru Serikali kwa kutujengea lile Daraja la Mtambaswala, lakini daraja lile unaweza ukakaa zaidi ya miezi miwili huwezi kukuta gari inapita pale, kwa nini?
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
TAARIFA
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimweleze mtoa hoja kwamba Daraja la Mtambaswala sasa hivi ndio njia kuu ya kwenda Msumbiji na linapokea magari mengi ya IT yanayopita pale. Kwa hiyo sio kweli kwamba unaweza kukaa siku nzima bila gari, hizo habari sio sahihi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtenga, taarifa hiyo.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo siipokei na mtoa taarifa nadhani hapatikani kwenye jimbo lake ndio kisa anayazungumza hayo. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtenga, kanuni zetu haziruhusu kumsema Mbunge mwenzio, futa neno hilo.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafuta kauli.
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia Daraja la Mtambaswala na ninapozungumzia kujenga Daraja la Mto Ruvuma, ukitoka Mtwara Mjini kwenye Kiwanda cha Dangote mpaka Mahurunga takribani pana kilomita 70. Ukitoka Mahurunga ukivuka kwenda Msingwe Daplaya pana kilomita zaidi ya 70, tuzungumzie kiuhalisia.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
TAARIFA
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mtenga kwamba Daraja la Mtambaswala analolizungumza tayari limeshajengwa, lipo, yeye ajielekeze kwenye kuomba Daraja la Mto Ruvuma bila kubeza Daraja la Mtambaswala.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtenga, taarifa.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa, siipokei.
NAIBU SPIKA: Endelea na mchango wako.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumza kilomita 140, ninachotaka kukisema tuna Mradi wa NLG unakuja Lindi. Mradi huu utafungua fursa kwenye nchi Jirani, hoja yangu ya msingi ni kwamba miradi hii ambayo inakuja na fursa ambazo zipo na malighafi ambazo tutakuwa tunazitengeneza katika mpaka wa Mtwara la Lindi, ziweze kufikika kwa wakati, lakini gharama iwe ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza leo Dangote wanauza sementi, sementi ya Dangote ikipita Mtambaswala mpaka kwenda Mozambique haiwezi kuuzika, lakini kama tungekuwa tuna daraja ambalo liko shortcut, sementi ile ya Dangote ingepata soko kubwa sana na Tanzania tungepata kodi ya kutosha kupitia Kiwanda cha Dangote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna suala la reli. Tunapozungumzia bandari ni mbadala lazime tuwe na reli lakini reli hii ya Mbambabay - Mtwara imezungumzwa kwa muda mrefu sana. Niiombe Serikali mazingira yote tunayotaka kuyafanya kwenye shughuli zozote za kimaendeleo, hatuwezi kuikwepa reli ya Mtwara, kwa hiyo niiombe sana Serikali, reli hii na nadhani ipo kwenye mpango, lakini nimwombe Mheshimiwa Waziri reli hii ipatikane kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna utanuzi wa airport pale nayo niishukuru Serikali wametujengea uwanja wa kisasa na naamini sasa tutakuwa International Airport Mtwara, lakini rai yangu ni moja uwanja ule unakaribia kwisha, lakini katika package ya uwanja ule bado kuna mapori ambayo yamezunguka ule uwanja, hatujaona mazingira yeyote yanayopelekea kuwa na uzio unaoendana na ujenzi wa Airport ya kisasa. Naiomba Serikali na Waziri kwamba sasa tujielekeze…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mtenga, kengele ya pili.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)