Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia muda. Napenda kutoa ushauri kwa TANROADS, swali la kwanza la kujiuliza kwa TANROADS ni kwa nini miradi yote ya Mikoani imekwama? Mimi nadhani kimoja ni kwamba miradi ninavyoelewa TANROADS kuna miradi inasimamiwa na Mikoa na kuna miradi inasimamiwa na Makao Makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda muda umefika wa TANROADS watafakari zaidi kwanini wasiwe TANROADS moja, miradi inasimamiwa toka Makao Makuu, mikataba inawekwa toka Makao Makuu na wengine wanafuatilia, huo ndiyo ushauri wangu wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa pili kwa TANROADS ni kweli kwamba Wabunge tunafurahia lakini barabara yangu yenye kilometa 92 kwa wastani inachukua mwaka mzima kutayarisha barabara kabla ya kuweka lami, kwa hiyo, itachukua miaka siyo chini ya Ishirini, hii barabara haitakamilika!

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti nimepitia randama nzima wastani ni Shilingi Bilioni Moja na Bilioni Tatu, ni fedha zinaonekana ni nyingi lakini kiujenzi ni fedha kidogo sana. Sasa TANROADS inabidi vilevile wajiulize je, kuna ufanisi mkubwa wa kutoa fedha kidogokidogo barabara ichukue miaka Ishirini, Hamsini kujengwa au itakuwa Serikali inaingia hasara kwasababu kila ikijenga baada ya muda fulani inarudi tena kurekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine kwa TANROADS ni kwamba wajaribu kufuatilia ujenzi wa barabara umeenda unabadilika, nilikuwa na mtaalam mmoja amegundua njia nzuri sana ya kujenga barabara za kisasa kuachana na hizi tulizozizoea tunazoziona za TANROADS. Kwa hiyo, huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu upande huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikija barabara yangu ambayo kiuchumi ni muhimu kwelikweli inapita pembezoni mwa Ziwa Victoria, tunazo samaki, tunayo madini, tunayo pamba, alizeti, barabara hii kama nilivyokueleza huenda itachukua miaka 50 kukamilika. Kwa hiyo, nimejadili na Waziri kwa muda mrefu na mimi kawaida yangu huwa sipendi kuongea ambayo nimejadili na wataalam isipokuwa Mkandarasi lazima wamwangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija upande wa Wakandarasi ukweli ni kwamba tunawapenda wazawa lakini napenda kutoa pendekezo TANROADS, Wakandarasi wote wanaochelewesha miradi awe ni mzawa awe ni Mkandarasi wa kutoka nje, lazima muwe na mikakati mipya. Mkakati wa kwanza muweke kwamba kama mtu hakamilishi mradi kwa muda akichelewesha sidhani kwamba huyo anastahili kupewa mradi mwingine tena. Inavyoonekana ukisikiliza Waheshimiwa Wabunge wote hapa kilio chetu kinafanana, Wakandarasi hawamalizi kwa muda Wakandarasi hawalipwi kwa muda, sasa hii bodi inayo register ma-Engineer ni lazima ianze kuwa na orodha ya blacklist yaani Wakandarasi ambao hawawezi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho naomba TANROADS wawekee maanani ni pale wanapompatia Mkandarasi ambaye tayari ana madeni, kama wa kwangu nilifuatilia kwelikweli ndiyo maana nikakaa kimya nikajua huyu hata miaka Mia Moja hatamaliza kwa sababu zile fedha zangu anazolipwa kujenga barabara yangu ya lami ndiyo anaenda kulipia madeni yake ambayo hayanihusu mimi kabisa, nadhani Waheshimiwa Wabunge hali ndiyo hiyo hiyo. Mkandarasi yupo Mkoa ‘X’ anapewa kazi mkoa Y, akipata fedha za Mkoa ‘Y’ anaenda kulipia deni la Mkoa ‘X’. Kwa hiyo, tutumie ile Sheria ya Mfilisi mtu akiwa amefilisika haaminiki na huwezi ukampatia kazi. Kwa hiyo, naomba TANROADS wasitoe kazi kwa makampuni ambayo mienendo yao kifedha ni mibovu na wengine wanakuwa wamefilisika, wanatupatia matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tena ambacho TANROADS wajiulize je, hizi penalties ambazo wanazipiga hawa Wakandarasi waliochelewesha mbona hawagutuki wa hawastuki hawafanyi chochote? Ina maanisha kwamba hawaogopi wala hawachukui kitu serious kutokana na hiyo penalties ambazo wanapigwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija upande wa kivuko nadhani dakika zangu bado zipo. Ninacho Kisiwa kimoja kinaitwa Rukuba hiki kisiwa ni mashuhuri, kina wavuvi wengi na watu karibu wa East Africa wapo kwenye hiki Kisiwa nimeomba kivuko kwa muda sasa nadhani leo Mheshimiwa Professor atakiwekea maanani, kinaitwa Kisiwa cha Rukuba ninashukuru Serikali na ninamshukuru na Mheshimiwa Rais alishatoa Milioni 250 wameanza kujenga Kituo cha Afya, juzi nilikuwa tena Jimboni wamepewa tena Milioni 250 kwa hiyo zimefika 500 nadhani Serikali bado itaongeza fedha Zaidi, lakini Kisiwa kinahitaji kivuko na hiki kivuko naomba kiunganishe wilaya mbili ambazo ni Wilaya ya Rorya kwenye Kijiji cha Kibui halafu na Wilaya yangu lakini kitatoka Rorya kinapita kwenye hiki kisiwa halafu kinakuja hapa Musoma Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hicho kivuko hakipo kwenye bajeti ya mwaka huu lakini nakiomba kwenye bajeti ya mwaka ujao. Kivuko kingine cha muhimu cha kufanyia marekebisho, kivuko ambacho kinaunganisha Wilaya ya Bunda na Wilaya yangu ya Musoma. Kule Bunda inatokea Mwibara Kijiji kinaitwa Iramba. Sasa kile kivuko kuja huku kwangu Kurugee ni cha siku nyingi walichukua kivuko chakavu kutoka Mwanza wakaona watusaidie, kweli walitusaidia lakini ni kibovu. Kwa hiyo, tunaomba kivuko kipya kile ni chakavu, tulikitumia kwa muda tukiwa na mategemeo kwamba kivuko kipya kinaletwa cha kutoka Iramba kuja Kurugee. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Profesa kwa mchango wako.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: …fedha tupitishe tupewe vivuko vipya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)