Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii kuipongeza kwa dhati kabisa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi kubwa sana ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanya vya ndege. Hatua tunayopiga inatutia moyo sana Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja katika barabara muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Madaba, Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Ruvuma katika ujumla wake ni barabara ya Mkiu – Liganga - Madaba. Barabara hii inatumika na wananchi kwa malengo ya kiuchumi kutoka Wilaya ya Ludewa ndani ya Mkoa wa Njombe kwenda Songea kupitia Madaba Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa zaidi ya miaka mitano maelezo yamebaki yale yale kwamba tunafanya upembuzi yakinifu na wa kina. Kazi hii mpaka leo, nimesoma kwenye taarifa za Wizara kwamba upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika, lakini barabara hii haijatengewa bajeti ya ujenzi wa viwango vya lami. Wananchi wa Mavanga ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, wananchi wa Mahanje, wananchi wa Ifugwa, wananchi wa Madaba wametutuma tuwaulize Serikali ni lini kwa uhakika barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Waziri, wakati unaendelea kujipanga kutoa majibu haya kwa wananchi hawa niliowataja, kumbuka…

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa napenda kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Joseph Mhagama kwamba barabara hii pia ina umuhimu zaidi; kila siku tunapiga kelele kuhusiana na suala Liganga na Mchuchuma na barabara hii imepita maeneo hayo. Kwa hiyo, Serikali ione umuhimu hasa wa kutengeneza barabara hii kutokana na uzito na unyeti wa mahitaji wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhagama, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Njombe kwa kuniongezea hoja kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ramani ya Tanzania imebadilika, jiografia ya nchi hii imebadilika. Wakati Mwalimu Nyerere anakwenda kuomba fedha Uingereza za kujenga barabara ya Makambako – Songea, Uingereza walimwambia, hatuwezi kujenga barabara from nowhere; by then Songea ilikuwa nowhere, lakini Baba wa Taifa alienda na picha akamwambia Songea, Mkoa wa Ruvuma, Madaba na maeneo mengine ndiko tunakozalisha chakula cha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, umuhimu wa barabara ile kwa wakati ule ilionekana ni muhimu wa chakula, leo ramani ya Mkoa wa Ruvuma imebadilika. Leo makaa ya mawe yanatokana Mkoa wa Ruvuma, leo Mheshimiwa Neema amesema Liganga na Mchuchuma kuna madini ya chuma kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aelewe, tunaposema barabara ya Mkiu – Liganga – Madaba, tunaongeleza uchumi wa Taifa la Tanzania, tunaongelea maelfu ya Wana-Madaba na Wana-Ludewa watakaoajiriwa kama mama ntilie, akina mama watakaoajiriwa kama wafanyabiashara wadogo wadogo katika sekta nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wanaoishi Liganga, wanaoishi Mavanga, wanaoishi Mahanje, wanaoishi Madaba Mjini, hawa wote waliopo pembezoni mwa barabara hizi, wamewekewa ‘X’, wanashindwa kuziendeleza nyumba zao kwa sababu wanaamini kesho barabara itajengwa. Wanaishi maisha ya dhiki, maisha ambayo hayana hadhi ya wananchi wa maeneo hayo kwa sababu wanaamini kesho barabara itajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tukamsaidie Mama Samia Suluhu Hassan kuwafuta machozi wananchi wa Madaba, wananchi wa Ludewa watengenezewe hii barabara ili uchumi wa maeneo yale uweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niku-address in a very special way. Huwezi kuongelea maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma kama barabara ya Makambako - Songea haitajengwa kikamilifu. Barabara hii ilijengwa kwa viwango cha chini sana miaka ya 1980 na historia yake nimeisema ndani ya Bunge hili, Baba wa Taifa alienda kuomba msaada Uingereza. Wakati huo Mbunge wa wakati huo kabla hajawa Mbunge, Profesa Mbilinyi ndio alikuwa anabeba mikoba ya Baba wa Taifa. Leo angekuwa hai angewaambieni changamoto alizozipata kupata hii barabara. Leo barabara imebomoka, barabara ina mashimo, barabara haina ubora kabisa, ajali ni kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wanaopita maeneo haya wanapata changamoto ya barabara ya Makambako – Songea. Wananchi wa Igawisenga, wananchi wa Lilondo, wananchi wa Wino, wananchi wa Ifugwa, wananchi Matetereka, wananchi wa Magingo, wananchi wa Lutukila, Ndelenjumba, Bangamawe, wananchi wote wa barabara hii mpaka unafika Likalangiro. Barabara hii nyumba zao zimewekwa ‘X’ wasiziendeleze, wanaishi kwa dhiki sana wakisubiri barabara ijengwe.

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Ni lini watapata fidia ya barabara zao, ya majengo yao na barabara hii kwa uhakika itajengwa lini? Mheshimiwa Waziri atuambie.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara ile imejengwa muda mrefu sana na ilikuwa imara ndiyo maana imetusaidia kipindi chote hicho, ila sasa hivi imeharibika, ajue hilo msemaji.

NAIBU SPIKA: Actually, ndicho anachokisema hicho. Mheshimiwa taarifa.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napokea taarifa nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Ruvuma, akiwakilisha Vyuo Vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Makambako - Songea inahitaji attention ya Serikali kwamba usanifu umefanyika, lakini barabara haijengwi. miaka kwa miaka tunaomba fedha tukaijenge ile barabara. Tukawafute machozi wananchi wanaokaa pembezoni mwa barabara, wakapate fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante Daktari Mhagama.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.