Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia Bajeti ya Wizara iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye imempendeza ameweza kuendelea kutulinda na kutupa uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayofanyika kwenye Bandari ya Tanga. Tunaishukuru Serikali kwa kuboresha bandari ile ya Tanga kwa kuongeza kina cha bandari ile kutoka mita tatu za zamani zifikie sasa mita 13. Ilikuwa ukileta mzigo kwenye Bandari ya Tanga meli ilibidi ifunge gati umbali wa kilomita 1.7. Kwa hiyo, ilikuwa ni gharama kubwa kushusha mzigo kwenye Bandari ya Tanga, lakini kwa hiki kilichofanyika sasa na kinachoendelea kufanyika tunaishukuru sana Serikali. Kazi ile ikikamilika tunategemea kuongeza ukubwa wa mizigo kutoka tani 700,000 za sasa kwenda tani 3,000,000. Ni mabadiliko makubwa, tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukisema hayo, yapo mambo ambayo nadhani hayako sawa na ni vizuri tukachukua hatua za haraka ili maboresho yaende sambamba ili tutakapokabidhiwa bandari ile shughuli zitakapoanza kusiwe na msongamano.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la sasa la bandari ile ni hekta 17. Kwa ukubwa wa mizigo tunaoutegemea, eneo hili halitoshi kuweka mizigo, lakini bahati nzuri tuna eneo kule Mwambani la hekta karibu 176. Vilevile tuna eneo kule Chongoleani la hekta 207. Tunachokiomba, tufanye kazi haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ni kwamba tuboreshe kule Mwambani kwa sababu ni umbali wa kilomita sita tu kutoka bandari ya sasa. Tukiweza kufanya maboresho, maana yake mizigo itakuwa ya uhakika kuweza kutunzwa na kupokelewa. Tusianze shughuli za Bandari ya Tanga bila kuwa na uhakika na sehemu ya kuhifadhi mizigo hii kwa sababu tukienda hivyo, halafu wizi ukitokea, maana yake tunaharibu jina zuri la Bandari ya Tanga. Kwa hiyo hilo lilikuwa ni eneo langu la kwanza. Tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukipongeza haya, nachelea kusema kwamba bajeti hii sitaiunga mkono. Sitaiunga mkono kwa sababu watu wa Mkinga tumekuwa wahanga wa ahadi zisizotekelezwa. Tuliwahi kupata uwekezaji wa takribani bilioni moja US Dollar kwa ajili ya kujenga Kiwanda cha Saruji pale Mtimbwani. Watu wale walitaka kujenga gati kule Kwale, lakini kwa sababu zisizoeleweka, maamuzi ambayo hayakuwa na faida kwa Taifa hili, watu wale walizuiwa kujenga lile gati na matokeo yake sisi watu Mkinga tukapoteza ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha Saruji katika Afrika Mashariki. Jambo lile limekuwa na maumivu makubwa sana sisi watu wa Mkinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema sitaunga mkono kwa sababu kuna dalili nyingine tunazoziona za barabara yetu ya kutoka Mabokweni, Maramba, Mtonibombo, Magoma kwenda mpaka Korogwe. Mwaka 2021 tuliahidiwa hapa kwamba imetengwa shilingi 1,200,000,000 kwa ajili ya kuanza usanifu wa mradi ule. Ninapozungumza hakuna kinachoendelea kwa maana ya usanifu kufanyika. Taarifa nilizonazo mpaka leo ninapozungumza, tupo kwenye hatua ya evaluation ya kumpata Mhandisi Mshauri. Yaani tumetumia mwaka mzima kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kwenda kufanya usanifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haiwezi kuwa sawa. Nimeangalia vitabu hapa nione kama kuna fedha nyingine imetengwa kwa ajili ya kazi hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, sioni. Kwa hiyo, nasema sitaunga mkono bajeti hii mpaka Waziri atakapokuja kutueleza ni lini evaluation ile itakamilika na kazi ya usanifu itaanza kufanyika ili watu wa Mkinga tuwe na matumaini kwamba barabara hii inaenda kufanyiwa kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema tumekuwa wahanga wa ahadi zisizotekelezwa kwenye upande huu wa bandari kwa sababu tuliahidiwa kwamba kule Mkinga kwenye bandari zile bubu tungeweza kurasimishiwa bandari ya Moa iweze kufanya kazi vizuri, tuweze kufanya biashara vizuri na wenzetu wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aliyekuwa Meneja wa Bandari wa Mkoa wa Tanga alikuja kufanya ziara kule Mkinga mwaka 2018 akatuhakikishia kwamba jambo hili sasa linaenda kufanyika; leo ni miaka mitano hakuna a single cent imetolewa kwa ajili ya kuboresha ile bandari bubu. Tunaendelea kupoteza mapato ya nchi hii kwa sababu bandari ile sasa imegeuka kuwa ni uchochoro wa kuingiza bidhaa za magendo na sisi tunaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hatutaunga mkono bajeti hii mpaka mje mtuambie ni lini mnarasimisha Bandari ya Moa iweze kufanya kazi vizuri na lini shughuli ya usanifu wa barabara ile ya Mabokweni – Maramba - Mtonibombo mpaka kwenda Korogwe itafanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru.