Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa mara nyingine tena. Nasimama kwa masikitiko makubwa sana kwenye Wizara hii ya Ujenzi. Kwa bahati mbaya sana Mheshimiwa Waziri aliyepo leo ndiye aliyekuwepo Bunge lililopita, Bunge la Kumi na Moja, nikipoingia humu ndani. Katika Ubunge wangu wa miaka saba sasa nakwenda, kila nikisimama kwenye Wizara hii naisema barabara ya kutoka Kibirashi mpaka Kwa Mtoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mwaka jana kwa mara ya mwisho walituambia wametenga kilometa 50, lakini kwa kuanza wanakwenda kuanza na kilometa 20 na nikawaambia kwa nini kilometa 20 na zisiwe kilometa 50? Cha ajabu walichokwenda kukifanya ndani ya mwaka mzima tuliowapitishia bajeti ya kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa Watanzania, walichoenda kufanya kwenye Barabara ya Kibirashi mpaka Kwa Mtoro, wamesaini mkataba wa kwenda kuanza kazi, mwaka mzima wanasaini mkataba. Hii barabara nilishasema humu ndani, ina ahadi ya Mheshimiwa Hayati Mkapa, ahadi ya Mheshimiwa Kikwete na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 na 2020 – 2025 sasa, lakini barabara hii kila siku wanatupa hadithi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakienda na staili ya kilometa 20, barabara hii ina takribani kilometa 460, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ili iweze kukamilisha barabara hii inahitaji miaka 23. Hiyo miaka 23 wanayoihitaji, ni kama kila mwaka watajenga hizo kilometa 20, lakini kwa kuwa wanatumia mwaka mmoja kusaini mkataba wa kujenga kilometa 20 wanahitaji miaka 46 ili waweze kuikamilisha hii barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa barabara na ukubwa wa Taifa hili, barabara tu ya kilometa 460 wanahitaji miaka 46, nashindwa kutafakari, yaani nashindwa kuelewa kwenye suala zima la hii barabara. Nilishasema hapa kwamba, kama Serikali inaona barabara hii sio kipaumbele na haina tija kwa Watanzania wa Mikoa minne, Tanga, Manyara, Dodoma na Singida, waifute tujue hatuna barabara kuliko kuwa wanatuandikia kwenye barabara kila mwaka. Barabara inakuja ina maandishi, wanatenga fedha halafu hawaendi kutekeleza, wakija wanatupa maandishi, watuondoe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachosema hiki wakati mwingine tunaumia, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hapa wamesema, kuna watu wanabandua lami wanabandika lami. Sisi Mkoa wa Dodoma ukiangalia maunganisho tuliyounganishwa, jimbo ambalo angalau lina barabara za kutosha za lami ni Jimbo la Dodoma Mjini, ukienda katika majimbo yote ya vijijini hatuna lami. Leo kwenye kilimo, Mkoa wa Dodoma ni mkoa ambao ndio unaokwenda kulima zao la alizeti na wilaya pekee kwa Mkoa wa Dodoma ambayo ndio inatekeleza kilimo cha mkakati cha zao la alizeti ili tuondokane na uhaba wa mafuta nchini ni Wilaya ya Chemba, lakini barabara yake haitengenezwi. Hiyo alizeti Watanzania wa Wilaya ya Chemba wakilima wanaifikishaje sokoni? Inafikaje sokoni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii, hizi kilometa 20 ambazo unaanzia Kibirashi, kama wameamua kuanza na kilometa 20 niombe, Mkoa wa Dodoma kuanzia Oloboroti pale twende na sisi wakatutengee kilometa 20, otherwise hatutaelewana na Mheshimiwa Waziri. Ameanza kilometa 20 Kiberashi ameshapanga wamesaini mkataba, twende akatutengee na sisi Chemba, Mkoa wa Dodoma, kuanzia Oloboroti mpaka Kwa Mtoro pale tumalizane salama, otherwise humu ndani leo, labda Kiti kininyime nafasi, la sivyo hatutaelewana. Uzuri ni yeye huyohuyo kwenye hii Wizara na kwenye hiyo barabara, wakija wanatoa tabasamu nzuri, wanaonesha sura za huruma, Watanzania wanaumia kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mto umepita pale Songoro, ule mto ni mkubwa haujawahi tokea. Watu wanakufa, watoto wa shule wanakufa katika mto ule wakati wa mvua masika; wao wako hapa wanafurahi kwa kuwa familia zao hazipati changamoto hizo ambazo Watanzania maskini kule chini wanazipitia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende katika suala zima la ulipaji wa fidia. Barabara hii wananchi wa Kata za Mrijo, Chandama, Songoro, Goima, mpaka Kwa Mtoro waliwazuia wananchi hao wasifanye maendelezo ya nyumba zao. Miaka 17 sasa hawajawalipa fidia, barabara hawajengi, Serikali ya watu maskini, wako wapi hao maskini? Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha hoja yake aniambie wanajenga barabara au hawajengi? Fidia wanalipa ama hawalipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hawalipi fidia wawaruhusu wananchi wa Wilaya ya Chemba waendeleze viwanja vyao kuliko kuendelea kuwapotezea muda na kuwaweka kwenye umaskini ambao haukuwa ni hitaji lao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Makole. Mwaka 2016 walikuwa wanafanya upanuzi wa uwanja wa ndege wakiwa wanasubiri kuanza ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Msalato. Mwezi wa Mei, 2016 wakawathaminisha watu nyumba zao kwamba, zinaondoka ili wafanye upanuzi. Tangu mwaka 2016 mpaka leo hawajalipa fidia za watu wa uwanja wa ndege, wamelipa baadhi wengine wamewaacha. Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha hapa aniambie fidia ya uwanja wa ndege pale analipa au halipi? Kama halipi, awaruhusu wananchi wa Kata ya Makole waendeleze nyumba zao, wafanye innovation za nyumba zao. Msiendelee kuwatia watu umaskini, umaskini sio sifa, wasitupotezee muda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja nimalizie. (Makofi)