Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite sana upande wa mawasiliano. Mkoa wa Mara mawasiliano ni shida hasa tukienda kwenye kata za Bunda upande wa Neruma, Nachonchwe, Vigicha, Ving‟wani na upande wa Tarime kuna Muriba na Yanungu. Hii ni asilimia kubwa sana ya watu ambao hawana mawasiliano na total yake inakuja ni 15,894 watu hawana mawasiliano. Mtu ukitaka kufanya mawasiliano inabidi uende kwenye mti yaani tunarudi kule kule enzi zile za Mwalimu Nyerere. Kwa kweli upande wa mawasiliano kwa Mkoa wa Mara inatia aibu. Naiomba Serikali ielekeze nguvu zake huko na kuhakikisha wale watu wanajione wako kwenye nchi yao na kwamba wanapata mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye upande wa uwanja wa ndege. Mkoa wa Mara tuna uwanja wa ndege mmoja tu na Mkoa wa Mara una historia kubwa sana ambayo haitafutika. Ni Mkoa ambao ametoka Baba wa Taifa, lakini uwanja wake wa ndege unatia aibu na unasikitisha sana. Tulitegemea uwanja wa ndege Musoma ndiyo uwe uwanja ambao ni wa mfano katika nchi yetu ya Tanzania. Hata kama tuna local airport basi iwe ni local airport yenye kiwango lakini uwanja wa Mara jamani unatia aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali ielekeze nguvu zote kwenye uwanja wa Musoma. Imefikia hatua tunasema sasa wana Mara na sisi tumechoka ina maana kwamba tunapohitaji kupanda ndege kwenye uwanja mzuri ni mpaka uende Mwanza au Dar es Salaam ina maana watu wa Mara hatufai kupanda ndege kwenye viwanja vizuri kwa hapa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nakuja upande wa barabara. Nitazungumzia barabara itokayo Manyamanyama kuelekea Musoma Vijijini. Barabara hiyo inapita katika vijiji vya Kangetutya, Kabulabula, Bugoji mpaka kufika Musoma Vijijini, kwa kweli hairidhishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea katika bajeti hii barabara hii angalau ingekuwa ya kiwango cha lami lakini gharama zake zimewekwa kwenye kiwango cha changarawe. Zile changarawe zinazowekwa ni za kiwango cha chini sana mvua inaponyesha barabara zile zinakatika. Kwa hiyo, hakuna mawasiliano ya barabara kutoka kule Musoma Vijijini kuja Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama mkulima anataka kuuza mazao yake ni lazima mtu atoke kule Musoma Vijijini aje Bunda, usafiri inakuwa ni shida sana kwa sababu watu wengi wenye magari wanaogopa kuweka magari yao yafanye biashara kwenye hizo barabara kwa sababu mtu anaona gari yake inaharibika.
Kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwamba barabara hii inayotoka Manyamanyama kwenda Musoma Vijijini kwa kipindi kijacho inajengwa kwa lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa Kabulabula akitaka kuiona lami ni mpaka aje Bunda au mpaka aende Musoma Mjini, kwa kweli tunaomba na tunasema kwamba wananchi wa kule wamechoka na wanasikitika sana. Mkoa wa Mara mzima barabara ya lami ni ile inayotoka Mwanza - Tarime - Kenya, zile barabara zingine zote hazina lami na nilitegemea kwenye bajeti yetu hii angalau ningeona vipande vya lami lakini sivyo. Lami tumewekewa kilometa mbili tu, ni ndogo sana na ni shilingi bilioni mbili.
Kwa hiyo basi, naomba na naendelea kuishauri Serikali, kwa hizi kilometa mbili zilizowekwa kwa upande wa Mkoa wa Mara kusema ukweli haziridhishi, hazitoshi ziongezwe. Mkoa wa Mara una population kubwa sana kwa nini Serikali isihakikishe inaweka lami katika baadhi ya barabara za Wilaya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na kuishauri sana Serikali iwe makini inapokuwa inakaa kujadili na kupanga bajeti zake. Kwa sababu unapokaa na kupanga ili mradi tu umepitisha bajeti, kaa uangalie ni watu wangapi unaowaumiza. Ina maana wale watu wa vijijini hawatakuwa na maendeleo mpaka lini? Hiyo pia inazidisha kudidimia kwa uchumi wa mahali husika kwa sababu watu wameshazoea ile hali ya kila siku kwamba mimi ni mtu wa kijijini, barabara ni ya vumbi, hakuna lami, hizo lami tutaziona mjini mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ajikite sana katika Mkoa wetu wa Mara, tunaomba lami hasa kutoka Bunda kwenda Wilaya ya Musoma Vijijini na pia barabara ya Nata kwa Serengeti, kwa kweli tunaomba mtusaidie barabara za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwa upande wa Serengeti ni Wilaya ambayo ina uchumi mkubwa kwanza tuna mbuga ya wanyama na pia watu wengi wanatoka Arusha kuja Serengeti, lakini barabara zile hazipitiki. Hamuoni kwamba tunapoteza asilimia kubwa sana ya uchumi wa Tanzania kwa kupoteza watalii kuja Tanzania kutembelea mbuga ya Serengeti?
Kwa hiyo basi, naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)