Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi mchana huu ili nichangie mada iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyopambana kuhakikisha ile miradi ya kimkakati inakamilika. Hili ni jambo jema sana na ni jambo la kutia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru na kuwapongeza sana watendaji kwenye Wizara hii wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote. Leo naomba nianze mchango wangu, nitaanza kwanza jimboni halafu nitakuja kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale iko kwenye Mkoa wa Lindi ni wilaya ya muasisi Mzee Kawawa. Wilaya ile iko tangu mwaka 1975, Wilaya ya Liwale inafikika kwa njia mbili tu, ni njia ya Nangurukuru – Liwale na Nachingwea – Liwale, nimeshazizungumza sana barabara hizi mbili. Hotuba iliyopita mwaka jana nilizungumza mambo mengi sana, sitaki kuyarudia, namwomba Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuijenga barabara hii, Barabara ya Nangurukuru – Liwale na Nachingwea – Liwale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokwenda kuizungumza Barabara ya Nachingwea – Liwale, haiyumkiniki tunaweza tukajenga lami kuanzia Nachingwea tukaelekea Liwale kabla ya kuijenga barabara ya Masasi – Nachingwea. Barabara ya Masasi – Nachingwea upembuzi yakinifu umekamilika mwaka 2014, miaka mingapi leo imepita barabara hiyo haijawahi kujengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya jumla; naiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuifunge Kanda ya Kusini kama ambavyo Benki ya ADB wameamua kujenga Barabara kutoka Mtwara – Newala kwenda Masasi, hiyo barabara wasiiache hapo Masasi waende nayo mpaka Liwale, watakuwa wametusaidia kuifungua Kanda ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiko kipande cha reli kinachozungumzwa kutoka Mtwara - Mbamba Bay, ukiona kwenye vitabu wanasema reli hii itajengwa kwa PPP. Akili yangu inakataa kwa nini imechaguliwa hii wakati nyingine zinajengwa na pesa za kwetu? Kwa nini hii iwe PPP? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuifungue Kusini. Ujenzi wa hizi barabara wakiniambia kwamba, tunatafuta fedha, ukiuliza hapa, majibu unaambiwa upembuzi yakinifu umekamilika, Serikali inatafuta fedha, si kweli! Hapa ninachokiona mimi ni utashi. Kwa sababu, kama ni suala la kutafuta fedha inawezekanaje barabara ilipofanyiwa upembuzi yakinifu 2018 na 2019 leo zinajengwa, lakini ya 2014 unaambiwa bado fedha inatafutwa? Hapa sio suala la kutafuta fedha, hapa suala ni utashi, ni ipi barabara ianze kujengwa na kwa faida ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tujenge hii barabara Nangurukuru – Liwale, Nachingwea – Liwale na Masasi – Nachingwea. Hizi barabara ni za muda mrefu sana, hebu waifungue Kusini. Sitaki kusema mambo mengi sana kuhusu barabara. Barabara ya Nachingwea – Liwale, Nangurukuru – Liwale, nimeshaizungumza sana. Naomba niishie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye ujenzi wa reli, SGR. Niishukuru sana Serikali, kwanza hapa nimpongeze CEO, ndugu yangu Masanja kwa uzalendo mkubwa anaouonesha katika ujenzi wa barabara hii, lakini nisiache hapa kuchangia kabla sijagusia uzalendo wa mchangiaji mwenzetu. Kuna Mbunge mwenzetu mmoja mzalendo amesema yeye anazo documents zinazoonesha kwamba, upo udanganyifu, taarifa tunazopata sisi kama Bunge, taarifa tunazopata sisi kama Kamati hazina uhalisia. Yeye ana taarifa ambazo ni halisia. Nisikitike huu uzalendo, alitakiwa aanzie kule kwenye Kamati, haya mambo yasingefika huku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwenye Kamati tumeambiwa hicho kipande cha Tabora – Kigoma bado hakijapata mkandarasi kiko kwenye hatua ya manunuzi. Leo mzalendo mmoja anatoka anasema yeye ana taarifa kwamba, kipande hicho tayari kimekabidhiwa. Kwa hiyo, ina maana hata taarifa tulizopewa kwenye semina ya Wabunge, tumedanganywa na sisi tuliopewa taarifa kwenye Kamati tumedanganywa na hata ripoti tuliyoileta hapa kama Kamati tumedanganya. Hapana, nahoji huo uzalendo uliopatikana. Naomba sana, kama kweli hizo documents zipo kwa nini hazikuanza kwenye Kamati? Nahoji uzalendo wa mchangiaji mwenzangu aliyechangia kuhusu ujenzi wa reli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ya ujenzi huu wa reli. Ushauri wangu hapa vyovyote itakavyokuwa, kama ni kwa single source au kwa kushindanisha watu, napendekeza haiwezekani hii reli kutoka Dar-es-Salaam mpaka Kigoma mpaka huko tunakokwenda mpaka Burundi ijengwe na mkandarasi mmoja, mimi napata wasiwasi kwa usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunakwenda kwa single source au kwa kushindanisha, lazima tuhakikishe hawa wakandarasi tunawagawanya vipande kama vipande vilivyogawika na hawa wakandarasi ni hivyo hivyo tusimpe mkandarasi mmoja. Tulishafanya kosa hili MSCL kama mnakumbuka, kule tunajenga zile meli tumempa mkandarasi mmoja, tumeona performance yake na sisi kwenye Kamati tukashauri, ujenzi wa hizi meli kuwe na ushindani, pasiwe na mkandarasi mmoja na sasa leo panatokea watu wengine wanasema kwamba, huu ujenzi wa reli SGR apewe mtu mmoja, hii si sawasawa. Naomba ushauri wangu uzingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine naupeleka kwenye ujenzi wa bandari. Serikali inafanya jambo kubwa sana kupanua bandari na kupanua bandari ni kuongeza uchumi wa Taifa letu. Ushauri ninaoutoa kwa Bandari ya Dar-es-Salaam ni ukweli usiopingika, Bandari ya Dar-es-Salaam sasahivi hata uipanue kwa kiwango gani haiwezi kuhimili maendeleo yaliyofikiwa sasa hivi. Kwa hiyo, wazo la kuwa na bandari mbadala Dar-es-Salaam ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaachia watendaji, hebu waangalie kwenye hizi bandari tatu ipi ianze kabla ya ipi, kuliko kwenda na zote tatu, kuna Bandari ya Mtwara, Bandari ya Tanga na Bandari ya Bagamoyo ambayo inazungumzwa. Hata hivyo, ukiniuliza mimi kwa jiografia ya nchi yetu nitasema tuanze na Bandari ya Mtwara. Bandari mbadala wa Dar-es-Salaam iwe Bandari ya Mtwara, kwanza Bandari ya Mtwara ina kina kirefu kuliko hizo bandari nyingine ambazo wanakwenda kuzitengeneza. Ushauri wangu ni kweli kabisa Bandari yetu ya Dar-es-Salaam imeshazidiwa. Waipanue watakavyoipanua haitawezekana, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, lazima twende kujenga Bandari ya Mtwara iwe mbadala wa Bandari ya Dar-es-Salaam.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Naomba tu kumpa mchangiaji Taarifa kwamba, kwa mujibu wa Port Master Plan inaelekeza kwamba, ili Tanzania tuweze ku¬-maximize competition ni lazima Tanzania tuamue kila Bandari ipewe jukumu lake maalum. Kwa maana Bandari ya Tanga iwe dedicated kwa ajili ya mzigo fulani, Bandari ya Dar-es-Salaam iweze kuwa dedicated kwa ajili ya mzigo fulani na Bandari ya Mtwara iwe dedicated kwa ajili ya mzigo fulani. Hiyo ni taarifa kwa mujibu wa Port Master Plan to unlock the economical potentials of this country.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Taarifa yake, lakini narejea kwenye ushauri wangu kwamba, ili tusiende na bandari zote tatu kwa pamoja zikatuchelewesha tuchague ipi itangulie kabla ya ipi. Nikasema kwa kuipanua nchi yetu tuanze na Bandari ya Mtwara ambayo tayari ina-advantage kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kuchauka kwa mchango mzuri.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)