Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuwa miongoni wa kuchangia Wizara hii ya Ujenzi muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Kwanza nianze kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya kuendelea kusaidia kufungua fursa hasa za mtandao wa barabara katika maeneo yetu mbalimbali, nimpongeze sana Waziri anafanyakazi kubwa kwa sababu hii Wizara ni kubwa sana, ina vitu vingi sana. Ninawapongeza viongozi wa mashirika hasa TPA na TRC kiukweli mashirika haya ni makubwa sana lakini ma-DG hawa wamekuwa wakifanyakazi kubwa ili kuhakikisha mashirika haya hayatetereki.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimesimama hapa kuipongeza Serikali, ukiangalia katika mtandao wa barabara katika Jimbo langu la Igalula ilikuwa kero kubwa ni barabara ya Chaya – Nyauwa, juzi Mheshimiwa Rais tarehe 17 amekuja kuizindua barabara ile na sasa wananchi wanafurahia matunda hayo, kwa hiyo sitokuwa na barabara nyingine ya kuweza kupata malalamiko bali nilikuwa nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mkoa wa Tabora unakwenda kufunguka kiuchumi lakini kuna barabara ambayo wakiiangalia kwa bajeti zijazo, barabara ya kutoka pale Mpumbuli ukaenda Izumba, Mwisole ukatokea mpaka Ndala, ukaunganisha na ile barabara ya Puge, Ziba baadaye itokee Nzega barabara hii wakiitengeneza itaokoa zaidi ya kilometa 70, ambapo mtu akipita Manyoni - Itigi, Nzega na yule atakayepita barabara ya Manyoni - Itigi kutokea Puge na Nzega mpaka Mwanza atakuwa ameokoa kilometa 70. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri kwa awamu ijayo naomba mfanye tafiti ili muweze kuiangalia hii barabara kwa sababu tutafungua Mkoa zaidi hasa wananchi wangu wa Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia mambo matatu au manne. Kwanza, tuna mradi mkubwa wa SGR ambao asilimia 80 ya mradi wa Makutupora - Tabora unapita katika Jimbo la Igalula, juzi nimeshuhudia Waziri alikuja kufungua ule mradi kuashiria kazi ianze, wananchi wangu wa Jimbo la Igalula kwanza wameupokea mradi kwa kiasi kikubwa na sisi tuko tayari kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha ile azma ya Serikali kufungua mtandao wa reli kutoka Dar es Salaam mpaka Kanda ya Ziwa Mwanza na hatimaye Kigoma na nchi jirani unakwenda kutimia.

Mheshimiwa Spika, wananchi wangu wamenituma yafuatayo, kwanza kwa kuwa mradi umekuja tumeshauzindua wataalam wako site wananchi wa Kata ya Tura, Malongo, Goweko, Igalula pamoja na Nsololo wanaomba sana wataalam wawahi kwenda kubainisha maeneo wapi reli itapita. Kwa sababu kumekuwa na uvumi mwingi na wananchi wameshindwa kufanya shughuli za kimaendeleo hawajui wapi wajenge wako sahihi. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali twendeni kule tukawape maelekezo wananchi wetu wapi reli itapita na muzuie kama yuko ndani ya zile mita 30 basi wapewe maelekezo mapema kuliko kwenda kuwafanyia fumanizi, lakini kama wako nje ya sheria ile ya reli yaani reli itakuwa imefuata wananchi basi muangalie utaratibu wao wa kuanza kuwaambia wasiendeleze majengo kwa sababu isije baadaye ikatokea mgogoro, kwa hiyo nilikuwa naomba hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naiomba Wizara kuna wananchi wangu hasa wa Kata ya Goweko na Nsololo wako kwenye zile mita za Serikali ambayo ninyi wenyewe mliziweka hapa ya kuwa mita 30 walijenga tangu miaka 30, 40 iliyopita, wananchi wale walikuwa na kilio kwa sababu kama sheria ilikuwa hivyo sasa hivi wanaoishi pale ni Watoto, wazazi wao asilimia kubwa walishapoteza maisha basi walikuwa wanaomba pale mtakapoenda kuwatoa basi muweze kuwapa kifuta machozi ili sasa wakaendeleze maisha kwa sababu wengi walioko pale ni yatima kuliko kwenda kuwaondoa kwa haraka haraka kwa sababu wao wamerithi wazazi wao ndiyo walijenga pasipo kujua.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuniahidi kunijengea daraja la Loya, kwa sababu ilikuwa ni changamoto kubwa na TARURA kama tungeweza kuwapa huu mzigo tusingeweza kuutatua. Kwa hiyo kwa ujenzi wa daraja la Loya utasaidia sana wananchi wangu kupata huduma na kutokupoteza maisha kila kipindi cha masika.

Mheshimiwa Spika, kuna suala moja ambalo Mheshimiwa Waziri tarehe 17 kuna ugeni wa Rais nililisema na hapa naomba niliseme, Mheshimiwa Waziri ile barabara mlioizindua hiyo tarehe 17 niliomba siku ile matuta hamkunielewa. Mheshimiwa Waziri kumekuwa na vifo vingi sana, watu wanagongwa wanapoteza maisha kwa sababu ya mwendokasi wa magari. Naomba unisaidie kwa haraka, uniwekee matuta hata kwenye zile center za Tula, Kizengi na Kigwa kwa sababu hizi center kubwa watoto wanatoka upande mmoja kwenda upande mwingine wanapoteza sana Maisha.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)