Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Serengeti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote nampongeza sana Rais wetu kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya hasa ya kuhakikisha pesa inapatikana kwa ajili ya sekta ya uchukuzi katika nchi yetu. Pia Wizara hii wanaendelea na kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu ya uchaguzi nawapongeza sana.
Mheshimiwa Spika, ili nchi iendelee ni lazima kila wakati ihakikishe inakuwa na vipaumbele sahihi. Wizara hii kwa takribani miongo mitatu imejikita sana katika kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango vya lami, tunapongeza sana jitihada hizi. Lakini jambo ambalo nimeliona kwa kiasi kikubwa vipaumbele kwa maana ya barabara gani ijengwe ni jambo la msingi sana, kwa wakati mwingi huko nyuma tulijikita sana katika kuhakikisha tunajenga barabara pamoja na viwanja vya ndege kwa ajili ya malengo ya kiutawala, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jamii inaweza kukutana. Hii ni jambo zuri lakini nadhani kwa wakati huu ambapo Taifa letu linahitaji kuweza kuendelea kiuchumi tena kwa haraka ni muhimu sana tuende kuzingatia barabara ambazo zinaweza zikatuletea manufaa makubwa kiuchumi tupeleke fedha nyingi huko kwanza.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano wa barabara hii inayotoka Makutano, Sanzate, Nata, Mugumu inaenda mpaka Tarime na kutuunganisha na nchi ya Kenya pia inaenda mpaka Arusha. Barabara hii imekuwa ikitengewa fedha kidogo sana, ni zaidi ya miaka 10 barabara hii haikamiliki, lakini ukiangalia barabara hii ina manufaa makubwa sana kiuchumi. Katika hifadhi ya Serengeti ambayo sote tunafahamu inatuingizia fedha nyingi sana, product kubwa sana ya kiutalii inayouza ni ile migration na ku-cross Mara River ambayo iko upande wa Magharibi wa hifadhi ya Serengeti, sasa upande ule hakuna barabara zinazoenda.
Mheshimiwa Spika, ningependa kushauri Wizara itambue hili, tunaweza tukadhani kwamba Serengeti ni maarufu watu watakuja Hapana! hawawezi kuja kama hatujaweka miundombinu mizuri. Kwa hiyo, ninashauri sana lazima Wizara sasa iangalie zile barabara ambazo zinaenda kutusaidia kuingiza fedha nyingi sana hasa barabara hii ni lazima tuzikamilishe kwanza ili pesa ipatikane tuweze kupeleka sehemu zingine na nchi ipate maendeleo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Mrimi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.
T A A R I F A
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninampa taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti, ni kweli barabara hii ni muhimu na imechukua muda mrefu sana, hivyo ni vema sana
SPIKA: Taarifa ya ziada kwa alichokuwa anakizungumza.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa ya ziada ni kwamba Serikali itoe pesa barabara hii imechukua muda mrefu sana zaidi ya miaka Kumi.
SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mrimi.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Bulaya kwa taarifa.
Mheshimiwa Spika, barabara hii sasa ni muhimu ikamilike. Siyo tu kwamba wananchi wa Serengeti wanapata adha na Mkoa wa Mara kwa ujumla, lakini pia tunalikosesha Taifa mapato makubwa sana. Leo kuna barabara kwenye nchi hii ukipita, zaidi ya masaa kumi wanapita tu mbuzi, ng’ombe, mbuzi, ng’ombe, hazina manufaa makubwa sana kiuchumi lakini bado leo tunaona barabara ambazo zingetusaidia sana katika uchumi hazijengwi, hazikamiliki fedha inapelekwa kidogo. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iende kuhakikisha barabara hii sasa inakamilika, tunaiomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia uwanja wa ndege ujengwe katika ule Mji wa Mugumu ili tuweze kupata watalii pale moja kwa moja. Rais amejitahidi, ameitangaza nchi yetu kwa maana ya Royal Tour, ni vizuri uwanja wa ndege ujengwe pale kama wenzetu wa Masai Mara wanavyojenga uwanja kule kwao. Tujue kwamba Masai Mara ni substitute ya Serengeti, kwa hiyo, tukichelewa tutakosa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, pia niikumbushe Wizara hii, huko nyuma kama factor kubwa ilitumika kwamba tunaunganisha barabara zote zinazounganisha Mikoa. Mheshimiwa Rais Kikwete mwaka wa 2021 tukiwa Chato alisema ilibaki barabara ile inayounganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha ambayo ndiyo inayopita hapo na Nata mpaka Mugumu hadi Arusha. Mpaka leo barabara hii haijawahi kukamilika. Kwa hiyo, naomba sana Wizara kama basi factor ni kuunganisha Mikoa yote, Mkoa wa Mara pamoja na Mkoa wa Arusha bado haujaunganishwa.
Mheshimiwa Spika, mwisho nimalizie kuomba Wizara hii iende kutoa fedha kwa ajili ya kulipa fidia. Ukienda pale wananchi wa Isenye, wananchi wa Nata, Nyichoka na sehemu nyingine barabara hizi ambapo zinapita, mpaka sasa wananchi hawajawahi kulipwa fidia, wanalalamika na barabara ukienda pale Mkandarasi sehemu nyingine amesimama, hajengi, ameruka kwa sababu wananchi hawajalipwa fidia. Kwa hiyo, tunaomba sana wananchi wale wameacha shughuli zao kwenye maeneo yale na wanahitaji walipwe fidia ili waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)