Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hii Wizara muhimu sana ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, tarehe 18 ya mwezi huu wa Tano, wiki iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alizindua barabara ya Tabora kwenda Mpanda kilometa 343. Wananchi wa Jimbo langu la Katavi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Katavi wamenituma nitoe salaam kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Wanamshukuru sana na wanaishukuru Serikali kwa kutenga jumla ya Shilingi bilioni 473 na kuhakikisha kwamba barabara hii imekamilika kwa lami kutoka Tabora hadi Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sipendi kukumbuka tulipotoka kwa sababu kabla ya kujengwa barabara hii kwa kiwango cha lami, kipindi cha masika tulikuwa miezi mitatu hadi minne hatuwezi kuitumia hiyo barabara na ndiyo barabara fupi inayotuunganisha na Makao Makuu ya nchi Dodoma pamoja na wakati ule nikiwa Dar es Salam.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa kipindi cha masika ama upite Nyakanazi hadi Kigoma ndiyo urudi na barabara ya Uvinza kuja Mpanda; au upitie kwako Mbeya uende Tunduma, ndio ukazunguke Sumbawanga ndiyo uende Mpanda. Kwa kweli wananchi walikuwa wanateseka, wanatumia gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa angalia mazingira kama hayo, kama kuna mgonjwa, kweli angepona? Sasa hivi ndiyo maana wananchi wa Mkoa wa Katavi wamenituma nimshukuru Mheshimiwa Rais. Ni kweli kwamba Sera ya ujenzi imeahidi kuunganisha Mikoa yote. Sisi kwanza tunashukuru kwamba Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Katavi umeunganishwa. Pili, tunashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri tayari ameshasaini mkataba wa kutoka Kibaoni kwenda Stalike. Maana yake ni nini? Barabara ile ikikamilika tutakuwa tumeunganishwa na Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunazidi kuomba, kazi imeshaanza, tuna kilometa 37.5 za kutoka Mpanda kuelekea Uvinza; namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati atakapohitimisha, hebu atuambie amejipangaje kukamilisha hii barabara ya kutoka Katavi, kutoka Mpanda, kwenda Uvinza ili tuweze kuungana na ndugu zetu wa Kigoma? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia wananchi wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwamba hii miaka iliyopita mitatu au minne, alitoa Shilingi bilioni 48, ametujengea bandari ya Karema. Niwaambie tu wachumi wetu wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Uchukuzi, angalieni wenzetu wa DRC, wiki iliyopita meli ya kwanza imetia nanga Bandari ya Karema pamoja na kwamba imekamilika kwa asilimia 80, na imekuja na mzigo mkubwa wa copper. Wameshaona faida ya barabara ya kutoka Tabora kwenda Mpanda na faida ya kujenga Bandari ya Karema, wameanza kuleta mzigo ili uweze kuja mpaka Bandari ya Dar es Salaam uweze kupekekwa kwenye soko Asia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, usafirishaji wa mizigo kutoka DRC ni ama utapita Bahari ya Atlantic kwa kupita South Africa au upite Bahari ya Hindi. Kusafirisha kupitia Bahari ya Hindi na Asia, ndiyo kwenye soko, ndiyo njia ambayo ni rahisi, ndio maana unaona wenzetu wameharakisha sana kuanza kuitumia hii Bandari ya Karema, kwa sababu lami tayari ipo kutoka Mpanda hadi Tabora, wanaitumia hiyo ili kupeleka mzigo Bandari ya Dar es Salaam, nasi tuweze kuongeza uchumi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tupe neno, sasa hii barabara ya kutoka Mpanda kwenda Karema takribani kilometa 110 una mpango gani na hiyo barabara? Naomba sana utakapokuwa unahitimisha bajeti yako, sina mpango wa kushika shilingi kwa sababu sisi Wana-Katavi tuna furaha sana kwa hilo. Kwa hiyo, tunaimani kwamba utaendelea kutukumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri ana taasisi nyingi. Kuna taasisi ya TANROAD, TPA, Kampuni ya Meli Tanzania, TBA, TEMESA, reli TRC na Mamlaka ya Hali ya Hewa. Ile barabara ya kutoka Mpanda kwenda Karema tunaomba sana pia ijengwe reli. Tuna imani kwamba mzigo wa kutoka DRC utakuwa mkubwa sana. Cha kufanya, kwa sababu tunaendelea kujenga reli ya SGR, naomba kutoka Mpanda kwenda Karema tuweke tuta la SGR lakini reli tuweke ya miter gauge. Baadaye itakapokuwa uchumi umekaa vizuri, tutakuja kung’oa ile reli na kwa sababu tuta litakuwepo, tuweze kuweka sasa yale mataluma ya SGR. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana kulikuwa na uchangiaji hapa kuhusu Mwanza, Ziwa Victoria, kwamba tunajenga meli Ziwa Victoria. Mimi nilikuwa Waziri wa Wizara hii. Uganda kila mwaka kuna mzigo wa tani milioni saba mpaka nane. Kwa hiyo, kitendo cha kujenga meli Ziwa Victoria kiendelee. Katika ile tani milioni nane, sisi huku kupitia Bandari ya Dar es Salaam, inapita tani haizidi 300,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna soko ambalo ni zuri kabisa. Naomba wachumi wa Wizara ya Uchukuzi pamoja na Ujenzi hebu harakisheni, soko la Uganda lipo na hawana sehemu nyingine ya kupitisha.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Spika, naona unaniangalia. Nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)