Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkoa wa Kigoma kitu ambacho kimeifanya Kigoma iwe hivyo ilivyo ni ukosefu wa barabara. Barabara ndizo zimetufanya tuonekane hatuna thamani yoyote, mfanyakazi akipangiwa kazi Kigoma anajiuliza mara mbili mbili niende au nisiende, akienda unamuuliza umekujaje na umefikaje hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu ambavyo mkoa wa Kigoma lazima utendewe haki ni kuufungua ule mkoa na kuutoa kwenye minyororo ya ukosefu wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Kigoma - Nyakanazi tangu nilipoanza kusikiliza na kuangalia Bunge imekuwa ikitwajwa mpaka leo na mimi na umri huu nimeingia humu naikuta barabara hiyo inaendelea kutajwa. Watakuja na wengine huenda wakaikuta tena barabara ya Nyakanazi inatajwa, kuna tatizo gani na Nyakanazi na Kigoma? Tuna dhambi gani watu wa Kigoma mpaka barabara hii inayotuunganisha na Mwanza na Kagera isifunguke, barabara hiyo moja tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia pesa zilizotengwa kwenye barabara katika vipande vile viwili ni shilingi kama shilingi bilioni 40 ambazo tuseme zinaweza zikatengeneza kilometa kama 40, lakini kuna wakandarasi wa kilometa hamsini hamsini, Kidawe – Kasulu na Kabingo – Kakonko kwennda kwenda Nyakanazi kuna shilingi bilioni 40, zitafanya kazi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine kikubwa kabisa cha kuiunganisha barabara hiyo hatuoni eneo linalotoja Kabingo, Kibondo, Kasulu, Manyovu, kilometa 258, hakuna kitu kinachozungumzwa pale. Kwa maneno mengine hii barabara bado ina safari ndefu ya kwenda. Tunaambiwa kuna fedha za ADB zimetengwa, labda Waziri akisimama atatuambia ziko sehemu gani kwasababu kwenye vitabu vyake vyote fedha hizo hazionekani, na kama hazionekani maana yake ni nini? Hiyo barabara haitatengenezwa kwa mwaka huu wala kesho wala lini. Na kwa kipande kilichopo tukikitengeneza kwa shilingi bilioni 40, sijui tunahitaji miaka mingapi kumaliza barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ya kuifungua Kigoma ni Kigoma – Uvinza, Kaliua – Urambo – Tabora. Hiyo isipofunguka bado tuna taabu. Sisi Kigoma ndio tunaolisha Tabora na wao wanafahamu ndiyo maana watu wa Tabora wala hawatuchokozi maana tukifunga hiyo barabara msosi Tabora itakuwa shughuli. Kwa hiyo, lazima hiyo barabara itengenezwe. Kuna pesa zimetengwa tena pale ili kukamilisha vipande vya kuanzia Uvinza kwenda Malagarasi na Kaliua hadi Urambo bado kuna shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo lazima ifunguliwe ni ya kuanzia Uvinza kwenda kwa watani wetu Mpanda hadi Sumbawanga. Barabara hizo zikifunguliwa utaona tu kwamba kila mtu anatamani kuhamia Kigoma, kwa sababu katika mikoa ambayo haijachakachuliwa ardhi ni Mkoa wa Kigoma, na barabara hizo zikishafunguka tutapata wageni wengi kuja kuwekeza katika mkoa wetu. Hatuwezi kupata wawekezaji kama hakuna barabara. Hata vile viwanda vilikuwa vinazungumzwa na Mheshimiwa yule mtani wangu, nilikuwa najiuliza wale wawekezaji watapita wapi? Na hata wakiwekeza viwanda bidhaa za viwanda wataziuzaje hakuna barabara? Ni land locked region, huwezi kutoka, ukiingia unashukuru Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuzungumzia reli hujazungumza kitu chochote katika nchi hii. Na tukitaka kujikomboa lazima hii reli tuitengeneze. Nchi makini zinatengeneza reli, nchi makini zinasafirisha bidhaa kwa kutumia treni, sisi tumerundika malori barabarani rundo. Kuna mtu mmoja aliwahi kusema haya malori ni ya nani? Mbona tukizungumzia kujenga reli hakuna ile motive ya ujenzi wa reli, kuna watu wanalinda linda haya malori haya? Maana mimi sikuona hata sababu kwa mfano Dar es Salaam – Mbeya malori yote yale ya nini wakati TAZARA iko pale na iko vizuri tu? Lakini ukizungumzia malori yale yatoke barabarani unatafuta matatizo. Mtu mmoja aliwahi kulizungumzia hili nadhani lilim-cost alipokuwa Waziri wa Uchukuzi – lilitaka kumgharimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu zangu niseme reli ya kati kwa standard gauge ni jambo ambalo haliepukiki kwa gharama yoyote. Kama tulishakopa vitu ambavyo huenda hata havikutusaidia sana tunatafuta mkopo sasa wa kujenga reli ya kati na matawi yake yote kuingia nchi zenye rasilimali Burundi, Rwanda na Congo kwa tawi litakaloishia Kalema ili tuweze kujikomboa kiuchumi. Reli hizo zitatusaidia katika maisha yetu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata umasikini kwasababu hatuna infrastructure za uhakika. Yaani wakati fulani unaweza ukajiuliza hivi anaetufanya tuwe maskini ni nani? Tumerogwa na nani nchi hii? Kumbe ni wakati fulani inawezekana hata kufikiri kwenyewe kwetu si kuzuri zaidi. Tunahitaji kufikiri vizuri zaidi ya leo. Na ndugu zangu tunapozungumza suala la Kitaifa kama hili tunaondoa itikadi zetu, tunakomaa pamoja. Hii reli hakuna reli itakayojengwa ya UKAWA, reli ikijengwa kwa standard gauge hapa ni nchi nzima tutaona matunda yake na faida zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie bandari. Kuna nchi ambazo zina bandari ndogo ndogo tu lakini zimetengeneza uchumi wake vizuri.
Wakati fulani ni aibu nchi kuwa maskini wakati ina bandari kubwa. Una bandari ya Dar es Salaam, una bandari ya Tanga, una bandari ya Mtwara, bandari kubwa zinazoingia na kutoka nchi nyingine za nje. Kinachotu-cost kwenye bandari yetu hii, hatujawekeza vizuri zaidi. Ushauri umetolewa kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani ukilinganisha na bandari za wenzetu wanavyo improve kuweka gat za kutosha; sisi sijui tuna politic! Wakati fulani huwa napata hata jina zuri la kutumia; lakini niwaambie kufanya biashara na bandari ya Dar es Salaam si rafiki kwa wafanyabiashara wanaopitisha mizigo pale Dar es Salaam, kuna red tapes kibao. Yaani urasimu mwingine hata usio na sababu, watu wanapoteza muda mwingi wa kutoa mizigo bandarini wakati bandari zingine mzigo unatoka kwa njia rahisi sana. Hiyo inatupotezea mapato mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri ukitaka hili likuokoe komaa na bandari, punguza urasimu pale bandarini. Yaani mimi nashindwa kuelewa bandari ya Dar es Salaam, mna-operate yaani hakuna electronic system ya kutoa mizigo na kulipia na kufanya nini. Unakuta watu wamebeba makaratasi anatoka TRA anakimbia kwingine, kwa nini usilipe TRA na karatasi lako likaonekana bandarini kwa electronic system? Tuna operate kama wakulima tu wa kijiji fulani hivi, wasomi wakubwa, maprofesa na madaktari tunashindwa kuweka system ambayo mtu akilipa TRA akienda bandarini anakuta inasomeka na inampunguzia muda. Panda, teremka, ukifika kule wanakwambia hatujapata karatasi kutoka TRA, ukienda TRA wanasema tuliyemtuma yuko njiani anapeleka hizo karatasi. Haya maisha ni ya kizamani kabisa kabisa na ni ya ujima kabisa! Sijawahi kuona kitu kama hicho katika nchi ambayo inaendelea ya sayansi na teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie simu fake. Hizi simu fake zilipongia mlichukua ushuru na mliendelea kupata kodi kwenye voucher zinazoingia kwenye simu fake. Leo mnatangaza sijui tarehe ngapi mnazizima, kwanza mmesha- calculate mtapoteza kiasi gani kwenye mapato ya nchi hii? Kwa sababu watumiaji wengi ni wale wanaosema walinunua simu fake, na aliejua simu fake ni ninyi, mliziuzaje zikiwa fake? Yaani ni kama mchezo wa kuigiza mnasema leta hizi simu mnaingiza zinauzwa halafu baadaye mnawaambia; jamani mna habari hizi zilikuwa fake? Sasa zilikuwa fake sisi tungejuaje? Mimi mnunuzi nina haja ya kuuliza hii ni fake? Na ukiuliza hii ni fake muuzaji anakwambia hii ndiyo original! Mimi natoka kijiji cha Kasuga, hivi kule Kasuga Kakonko najua original ni ipi na fake ni ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.