Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Miundombinu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na manaibu wake ni watu ambao tunajua wapo makini na uwezo wao wa kufanyakazi ni mzuri na niseme tu kwamba binafasi hawa ni ndugu zangu nani rafiki zangu.

Mheshimiwa Spika, nadhani katika undugu huo na urafiki huo ndiyo umefanya waninyime safari hii kila kitu. Yaani safari hii nikienda pale Musoma sina cha kwenda kuwaambia kwasababu kwanza hata kwenye zile fedha za tozo na fedha za UVIKO wenzangu walipata karibu bilioni 1.5 niliambulia milioni 500 nikaambiwa nitapata fedha kwenye miradi ya kimkati na miradi TACTIC kote huko mpaka leo wala hakuna dalili.

Mheshimiwa Spika, basi tumekuja nimeangalia hata ule uwanja wa ndege ambao nilitegemea kwa mwaka wa fedha huu ungeisha, Mheshimiwa Waziri rafiki yangu umechukua miji kumi yaani viwanja kumi umetuweka pamoja yaani kwenye hilo fungu umesema humo ndimo nilimo. Hiyo inaonyesha dhahiri kabisa kwamba huo uwanja tena nao utaendelea kuwa hadithi. Kwa hiyo, hayo yote ndiyo maana nasema kwamba katika upande wowote ule hakuna upande ambao umeonyesha hata dalili kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na reli ya kutoka Tanga kwenda Musoma ambayo ile reli ileā€¦

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nikutahadharishe tu Mheshimiwa Matiko iwe ni taarifa ya ziada kwenye anachokisema siyo uwe unachangia. Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ni taarifa ya ziada kuhusiana na uwanja wa Ndege wa Musoma. Uwanja wa ndege wa Musoma kila ukitokea wanaweka kwenye vitabu vya bajeti lakini hawatekelezi hiyo bajeti yenyewe na pale Musoma ndiyo anatoka Baba wa Taifa kwingine kote viwanja ndege kubwa zinajengwa ukija kwa Baba wa Taifa hawajajenga uwanja. Nampa tu taarifa kwamba wananchi wa Mara...

SPIKA: Ngoja ngoja twende vizuri katika hayo unayoyasema ni lipi ambalo Mheshimiwa Manyinyi hajalisema? kwenye hiyo taarifa yako ambalo yeye hajalisema unamuongezea ni lipi?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, mosi kwa baba wa Taifa anatokea Mkoa wa Mara na huwa wanaweka kwenye bajeti lakini hawatekelezi.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, naendelea tu kusema kwamba upande huo kwenye uwanja wa ndege kwa maneno mengine ule uwanja utachukua zaidi ya miaka mitano kabla haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hata ile reli ambayo imezungumzwa kwa miaka mingi kutoka Arusha mpaka ipite Tanga, Arusha, Musoma sasa leo hata kuzungumzwa haizungumzwi kabisa. Sasa najiuliza kama tunazungumza habari ya kuendeleza mikoa, miji na Mji wa Musoma ni mji ambao uko katikati ya Kenya na Uganda leo ile bandari hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chakusikitisha zaidi na sasa labda hicho Waziri atanifuta machozi kilichokuja kufanyika ni kwamba watu wa bandari kwa maana ya TPA walikuja Musoma katika kipindi cha nyuma wakafanya pale ulaghai wa kuonyesha kwamba wanampango mzuri wa kuendeleza ile Bandari ya Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sasa cha ajabu walichokifanya pale walipewa lile eneo wakalichukua, walichofanya ni kwamba walikuja kuzuia sasa yale mapato ambayo Manispaa tulikuwa tunayapata sasa wao ndiyo wakaanza kutaka kutoza ushuru. Sasa katika hilo hakuna chochote mpaka leo ni zaidi ya miaka minne inapita hakuna chochote ambacho wemeweza kukifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri kwamba maadamu yale yote nimekosa walau hata lile eneo lenyewe la bandari ambalo lilikuwa ni eneo kwa ajili ya Manispaa ya Musoma wala haliusiani na bandari wale wananchi wetu weweze kurudishiwa ili zile biashara zao ziweze kuendelea ambalo ni eneo la Bwigobero. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kusema kweli leo unapozungumza Mji wa Musoma ni mji ambao upo pembezoni mwa nchi. Kwa hiyo, ili ule mji uweze kuendelea lazima tuwe na mipango mahsusi ya kuuendeleza na mojawapo ya mipango mahsusi ndiyo kama hiyo viwanja vya ndege katika kukuza uchumi lakini vilevile bandari kama ile ingeweza kutusaidia. Sasa leo Musoma hatuna kiwanda cha Samaki vimekufa, hatuna kiwanda cha nguo, hatuna kiwanja cha ndege, yaani kwa maneno mengine ni kwamba hatuna chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi ya viongozi ni kufanya mambo yatokee siyo tusubiri mambo yatokee. Kwa hiyo, nilidhani kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri kwa sababu Musoma unaijua vizuri umekuja pale mara nyingi wewe mwenyewe unajua kabisa kwamba ni kwanamna gani unahitaji kuusaidia ule mji ili uweze kukua tofauti na hapo kusema kweli nitasubiri sitaunga mkono hoja mpaka pale nitakaposikia walau hata umenirudishia hilo eneo ili watu wangu waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana ahsante sana. (Makofi)