Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakwenda kuchangia Bajeti ya Wizara ya Miundombinu ya Mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na Barabara ya Mtwara Pachani inayopita Luchili, Lusewa, Magazini, Nalasi mpaka Tunduru yenye urefu wa kilomita 325. Ni barabara ya mkakati, kwa hiyo, tunaomba, nimeangalia kwenye list ya barabara zile sijaona kama imetengewa pesa. Naomba sana itengewe pesa ili barabara hii iweze kujengwa na ni barabara ya kimkakati. Siku zote nimekuwa nikisimama nikihitaja hii barabara, Mheshimiwa Mbarawa sijui anaona kama sauti yangu ni nzuri sana, kwa hiyo, naimba tu, wimbo unamfurahisha lakini haitengei pesa ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Barabara Makambako - Songea yenye urefu wa kiomita 300 ambayo inahitaji ukarabati toka ilijengwa enzi ya mkoloni. Barabara hii inahitaji ukarabati, imeharibika sana. Tunaomba sana na tumekuwa tukisema sana na hata leo nimetazama hapa Mheshimiwa Mbarawa hajaitengea pesa yoyote, lakini ajue kwamba ile barabara ndiyo atakayopita kuja Songea kule, yale makorongo na yeye yanamhusu. Kwa hiyo, kwa athari ambazo zitatokea hata kwa watu wengine zitamhusu pia hata Mheshimiwa Waziri. Naomba sana hii barabara itengewe pesa ili iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nina mambo matatu tu. Jambo la mwisho linahusu Kivuko cha Mitomoni. Kivuko hiki cha Mto Moni ni kivuko chenye changamoto kubwa sana. Naomba unisikilize kwa makini lakini pia unisaidie pengine labda kwa sauti yako sisi tunaweza kupata pesa ya kujenga kivuko hicho cha Mitomoni ambacho kinaunganisha Wilaya ya Songea Vijijini na Wilaya ya Nyasa na kwamba ni kivuko ambacho kinaenda kuweka mkakati mzuri sana wa kiuchumi. Pia ni kivuko ambacho kinapita katika Mto Ruvuma. Kivuko hiki kimesababisha wananchi wengi sana wamepoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, wananchi wamepoteza maisha kwa sababu Mto Ruvuma una mamba wengi sana na kwamba wanatumia magome ya miti ili kuvuka, hakuna kivuko. Wakati fulani Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyasa na Jimbo la Peramiho wamejitahidi sana kufuatilia lakini nami nataka niseme kwa mara nyingine tena. Mheshimiwa Naibu Waziri Kesekenya mwaka jana ambapo watu watano walipoteza maisha kwenye kile kivuko nilimfuata na nikampa simu akaongea na wananchi ambao wamepoteza familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata alivyozungumza nao, bado hakuona uchungu wala hajaona huruma na wala hajatenga pesa kwa ajili ya kwenda kujenga kivuko hicho. Nataka nikusomee watu ambao wamepoteza maisha kwenye kile kivuko, inatia huzuni, inatia huruma, watu wale ni wananchi wa Tanzania. Tunapolalamika hapa inaonekana kama vile sijui ni ng’ombe tu au ni wadudu gani? Hawa ni binadamu ambao wana haki ya kuishi, lakini tunalalamika kwamba kivuko pale hakitengenezwi na hakuna hatua zinazochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kivuko hata kama kingetengenezwa cha muda cha shilingi Milioni sita kingesaidia kuokoa maisha ya wananchi wale. Milioni sita wanataka kuniambia Wizara hii haina milioni sita ya kujenga kile kivuko?

Mheshimiwa Spika, nataka nikutajie uone kwanza nachangia huku natetemeka namna ambavyo wananchi wamepoteza maisha. Nakutajia mwaka 2016 wananchi tisa walipoteza maisha kwenye kile kivuko. (Makofi)

MHE. ENG. STELLA MNYANYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Stella Manyanya.

MHE. ENG. STELLA MNYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, dada ungeniacha tu nitiririke leo jamani. (Makofi/Kicheko)

TAARIFA

MHE. ENG. STELLA MNYANYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na jithada ambazo zimeshafanyika za kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga daraja la kudumu katika Mto huo Ruvuma. Kwa kweli naungana na mdogo wangu kuomba sana angalau kipindi hiki tunachosubiri, basi tupate hicho kivuko.

SPIKA: Mheshimiwa Manyanya hiyo siyo taarifa. Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naomba unilindie dakika zangu. Mwaka 2016 watu tisa walipoteza Maisha; Zulfa Mtauchila, Awetu Mohamed, Fadhili Hamis, Rajabu Said, Bahati Mustafa, Khadija Said, Seleman Abdallah, Said Waziri, Omary Mohamed. Hao walipoteza maisha mwaka 2016, Wizara inajua watu hawa wamepoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 Omary Bandawe alikuwa anavuka anaendesha mtumbwi, mtumbwi ule ulipinduliwa na mamba akatumbukia huko na hakuonekana mpaka kesho. Mwaka 2017 hiyo hiyo Wizara inajua ndugu Omary Chinguo nae alipoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, 2021 mwezi Mei tukiwa kwenye Bunge la Bajeti, Mheshimiwa Waziri anajua watu saba walipoteza maisha kwenye kivuko kile kile. Mimi leo sipandi juu ya meza, lakini nataka niseme hawa ni Watanzania wanahaki ya kuishi. Niruhusu nipige magoti kuomba kivuko kile kikajengwe. Tafadhali sana naomba kivuko kile kikajengwe kwa sababu wananchi hawa ni Watanzania na wana haki ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba leo nitaondoka na mshahara wa Waziri, sitaurudisha na siungi mkono hoja. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Ngonyani ulivyotoka tu hapo kwenye kiti chako ukaenda kupiga magoti yote uliyoyasema yale hayajaingia kwenye Taarifa Rasmi za Bunge.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naomba, napiga magoti leo hii. Siungi mkono hoja, siungi mkono hoja leo hii.