Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa na mimi niweze kuchangia katika Bajeti ya Wizara hii, Wizara ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya ili niweze kusimama na kuchangia. Pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa ujumla, kazi kubwa ambayo inafanyika ni kazi inayostahili kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Manaibu wote wawili kwa kazi kubwa nzuri ambayo wanafanya. Nimetumwa na wananchi wa Jimbo la Kalambo nilete salamu za shukrani kwa kuanza ujenzi wa Barabara ya kutoka Matai kwenda Kasesha ambayo inaenda mpaka Zambia Boda. Naomba wapokee pongezi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kupongeza naomba nichangie katika maeneo mawili au matatu. La kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba Bandari yetu ya Dar es Salaam imekuwa ndiyo kitovu kikubwa cha uchumi wa nchi yetu. Takwimu zinaonesha katika mizigo ambayo inapokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam, asilimia 31 ya mizigo ni ile ambayo inaenda Zambia, asilimia 36 ya mizigo inaenda Kongo DRC, asilimia tano inaenda Malawi, ukichanganya katika hizi nchi tatu unapata asilimia 72 ya mzigo ambao unatua Bandari ya Dar es Salaam uko kwenye nchi hizi tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asilimia 19 inaenda Rwanda, Burundi asilimia sita na Uganda asilimia tatu. Kwa nini nimeamua kutoa takwimu hizi? Utaona kwamba katika mzigo mkubwa ambao unapita Bandari ya Dar es Salaam asilimia 36 inaenda Kongo DRC. Hata hivyo, hiyo asilimia 36 nayo lazima tujue kwamba ni Kongo ipi ambayo mizigo mikubwa inaenda. Asilimia 70 ya kopa ambayo inapatikana DRC inapatikana katika Jimbo la Katanga ambako ndiko kuna Mji wa Lubumbashi na Kolwezi.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni wenzetu wamebahatisha kupata mgodi ambao utadumu kwa muda wa miaka 40. Kwa nini nayasema hayo? Ukitaka ku-access Kongo DRC kwa maana ya Lubumbashi na OR Katanga ya Chini na ya Juu ambako ndiyo asilimia 70 ya kopa inapatikana kwa Kongo DRC njia rahisi ya kufika huko ni kupitia Bandari ya Kasanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Serikali imefanya kazi kubwa sana, imejenga lami mpaka Kasanga na kuna kazi kubwa nzuri sana ambayo inafanyika katika maboresho ya Bandari ya Kasanga. Sasa sitaki kwenda huko Karemii lakini hesabu huwa haziongopi. Sisi kama Taifa kwa hii asilimia 70 ambayo inapatikana Katanga tukitaka kui-access ni kwa kupitia Bandari ya Kasanga. Niishauri Serikali na bahati nzuri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekuwa akitembea, huko duniani kuna watu ambao wako tayari kuwekeza kwenye vivuko. Sisi badala ya kwamba tulazimike kuzunguka, tulazimike kwenda mpaka Zambia huko ambako Serikali imewekeza fedha nyingi Bandari ya Kasanga ili tuweze kwenda Lubumbashi tuanze kutumia.

Mheshimiwa Spika, wenzetu Uganda wamefanya kazi ya kujenga barabara ndani ya Kongo kwa sababu wanajua nini wanachokifuata. Ni wakati muafaka kwetu sisi kwa kutumia private sector na Serikali tushirikiane, tuone namna gani tunajenga barabara kipande kifupi cha kuweza ku-access Lubumbashi ili mzigo mkubwa huu ambao utakuwa unapatikana, tuweze kuupata. Hii wala haihitaji investment kubwa, haihitaji mpaka tuje tujenge reli, reli itakuja baadaye, lakini kwa hali ya sasa hivi tunda ambalo unachuma ukiwa umepiga magoti ni kwa kupitia Bandari ya Kasanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie upande wa TAZARA. Katika huu mzigo ambao unapatikana bandari yetu, ifike sasa wakati muafaka kwa Serikali kuhakikisha kwamba tunakuwa na dry port Mbeya ili mizigo ambayo inachukuliwa na TAZARA ikatua Mbeya inakuwa ni rahisi sasa kuichukua kutoka Mbeya kwenda Kasanga halafu kuifikisha DRC Kongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukitarajia kwamba wenzetu wa upande wa pili ambao hawana interest sana na TAZARA watawekeza nguvu kubwa, hivyo tutakuwa tunajichelewesha. Uchumi ni vita na hii vita ya kiuchumi inaweza ikapiganwa chinichini, sisi tukadhani kwamba wenzetu wanatupenda sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kuhusiana na ujenzi wa Uwanja wa Ndege pale Sumbawanga. Ni ahadi ya Serikali ya muda mrefu imekuwa ikirudiwa bajeti na bajeti. Naamini Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atatoa tamko ambalo tukirudi au tukipiga simu tuambiwe tayari tushamwona mkandarasi. Kwa sababu tushaambiwa mara kuna compensation, mara tayari watu washalipwa, mara sijui aliyekuwa amepatikana naye amefika mahali anasema kumekuwa na mabadiliko makubwa nataka revision kwenye mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri its high time Rukwa nayo ipate uwanja wake wa uhakika. Sitaki kusema mikoa mingine, lakini itoshe mtu mkubwa ukisema unasikika, itoshe, its high time kwamba Rukwa tunataka uwanja wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee MV Liemba. Kama ambavyo wenzangu wameongea, wa Kigoma, wa Katavi wameongea na Rukwa tunaongea, tunahitaji MV Liemba ifanye kazi. Ni suala la aibu, nchi zingine wanaleta meli zao eti sisi hata ule ukarabati umeshindikana, its high time tunahitaji meli ya MV Liemba iwepo Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)