Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya msingi katika nchi yetu. Natamani nitumie nafasi hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais kikamilifu kwa namna ambavyo kwa Mkoa wangu wa Songwe wameweza kutujengea barabara ya kutoka Mpemba – Isongole. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwapongeze vile vile kwa kutujengea kile Kituo cha Forodha pale Mpemba ambacho ni kituo cha mpakani Tunduma ambacho kina heshima kubwa kuliko kile kituo cha upande wa Zambia, kiasi kwamba hata Wazambia wakati mwingine huwa wanakuja kupiga picha huku kwetu kwa namna ambavyo kimeboreshwa na kimekuwa cha kisasa sana.
Mheshimiwa Spika, pia niweze kuishukuru Wizara hii, kwa kweli wamekuwa ni watu wa msaada na ni watu wasikivu ambao mara nyingi tukiwafuata wamekuwa wakisikiliza changamoto zetu na kuzifanyia kazi. Pia niweze kuishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa kujenga hii barabara ya Igawa – Songwe mpaka Tunduma. Kipekee kwa kweli kwa Mji wa Mbeya wameutendea haki kwa kiwango cha pesa walichotenga kwa ajili ya barabara kutoka Uyole kwenda Ifigi. Nadhani hii pia itaweza kukupa heshima kwa Jiji la Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika barabara hii nilitamani kuwashawishi Wizara waone umuhimu au udharura wa kuijenga barabara hii kwa upande wa Tunduma pia. Ni kweli wataboresha Mbeya, lakini tujue kabisa Tunduma pia hali ni mbaya tunaona namna ambavyo foleni imekuwa ikizidi kila siku zinavyozidi kwenda na Mheshimiwa George alivyochangia jana alionyesha masikitiko yake ni kwa namna gani Tunduma kulingana na umuhimu wake katika uchumi wa nchi hii haijapewa kipaumbele, kwa hiyo niwaombe wizara kwa namna ya kipekee kabisa suala la kupanua hii barabara kutoka Mlowo kwenda Tunduma waone kama kipaumbele cha msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupitia bajeti hii nitatamani nimsikie Waziri akieleza ni nini mkakati wake wa kidharura kuhakikisha barabara hii upande wa Tunduma inapanuliwa, hata kama watashindwa kuanzia Mlowo basi waseme neno kuanzia eneo la Chimbuya kwenda Tunduma hali ni mbaya hali sio nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unafahamu barabara yetu hii haina sehemu ya mchepuko, kama ikitokea ajali, moto au changamoto nyingine yeyote barabarani hakuna namna ambavyo magari yanaweza yakafika Tunduma, na tunafahamu kabisa magari mengi yanayoenda Tunduma ni magari yanayotakiwa yavuke nchi ya Zambia, Congo na nchi za SADC kwa ujumla, lakini wananchi wa Tunduma inakuwa ni adha tunafahamu kabisa Mbeya na Tunduma ni watu wanaoingiliana sana, kama kukatokea jam ina maana watu wa Mbeya hawawezi kuja kufanya kazi Tunduma, kitu ambacho katika hali ya uchumi kwa upande wa nchi tunakuwa tunazidi kuyumba.
Mheshimiwa Spika, kwanini ninasisitiza kuhusu barabara ya mchepuko, ni kulingana na hali ya mambo ambayo yametokea katika kipindi hiki cha kuanzia mwezi wa 12 mpaka sasa hivi. Kumekuwa na ajali nyingi sana katika barabara hii na kiukweli wananchi wameteseka sana kama alivyokuwa ameongea Mheshimiwa Stella pale jana.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuongelea suala la barabara hiyo ya kutoka Igawa kwenda Tunduma ningependa niweze kuongelea suala la barabara ya Mbalizi - Galula - Mkwajuni na Makongolosi. Tunafahamu Wilaya ya Songwe ina rasilimali za msingi, tunafahamu kabisa kule madini ya dhahabu ambayo yanashimbwa ile inaingiza pesa katika nchi hii, kule tunatarajia tupate madini ambayo ni ya msingi kabisa rare earth ambayo hayapatikaniki sehemu nyingine lakini mazingira ukiangalia ya barabara hii ni magumu. Mheshimiwa Mlugo amekuwa akilia kila siku lakini mpaka sasa hivi sioni uelekeo au utaratibu ambao Wizara imetenga kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara ya lami katika hili eneo.
Mheshimiwa Spika, niseme tu ukweli Songwe kama kweli ikafunguliwa Wilaya ya Songwe ni potential kwa nchi hii kwa maana ya kuweza kusaidia kipato cha nchi kiongezeke. Kwa hiyo mimi ninaomba Wizara itakapokuja kwenye hili waweze kusema neno, na kwenye hili nitashika Shilingi kwa sababu Songwe inakuwa sahaulika sana na ni Wilaya pekee ambayo kwa upande wa Mkoa wa Songwe tunaitegemea kwa mapato makubwa ukiacha Tunduma, kwa hiyo kwenye hili Waziri nitaomba mje na maelezo ya kutosha kueleza ni lini barabara hii itaanza kujengwa.
Mheshimiwa Spika, pia ninatamani kuongelea kwenye suala la TAZARA tunajua Mkoa wa Songwe na Mbeya hauwezi kuutenganisha na kwa namna hiyo ina maana tunategemeana sana na tunafahamu kabisa suala la TAZARA ni letu wote.
SPIKA: Sekunde moja.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iweze kuweka mkakati maalum wa kuhakikisha TAZARA inaanza kufanya kazi ili pale Mpemba watakapojenga hiyo dry port ambayo tumeitengea eneo mambo yaweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)