Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nakishukuru chama changu kwa kunipa nafasi ya kuingia Bungeni na kuwa sehemu ya Bunge kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nianze kuchangia kuwa mimi ni mmoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu ambayo ilikuwa inatembea nchi nzima kuangalia uhalisia wa mambo yanavyoendelea katika Kamati hiyo. Nilichokiona ni kwamba nchi yetu ya Tanzania, kama tuna nia ya dhati, kwa sababu niliangalia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) ambao uliletwa hapa Bungeni. Nikaangalia na Pato la Taifa linakotoka, vyanzo vya Pato la Taifa la kuendeleza mpango huo, nimekuta kuna tofauti kubwa sana kwa sababu vyanzo kama bandari ambayo tulitarajia ilete pato ambalo litaweza kuendesha shughuli za nchi inadidimia na inazama kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Bandari ya Dar es Salaam kama ungewapa waendeshaji wengine ingeweza kutumika kama chanzo kikubwa ambacho kingeweza kuinusuru Tanzania kuishia kuwa na wakopaji wa kila siku, kwa sababu tumefika pale bandarini tumekuta kuna vitu viwili, kuna kitu kinaitwa MCL, tumekuta kuna TPA ambayo ndiyo mama. Katika kuangalia hali ile tumekuta kwamba watu wawili hamuwezi kuendesha kitu kimoja kwa nia tofauti. Kwa hiyo, unakuta kwamba bandari badala ya kupata mapato, ikafanya kazi vizuri, yeye anakuwa mwangalizi wakati MCL ambaye hana kipato anashindwa kufanya kazi vizuri. Na sehemu zote hizi kuna watumishi ambao wako pale wanafaidika na hamna kitu kinachotokea ambacho kinarudi kwenye Serikali kama mapato ambayo yanaweza kuendeleza nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza malalamiko ya watu wengi mikoani wanataka maji, barabara, n.k., lakini nimeangalia mapato ya Tanzania kupitia vyanzo halisi, hakuna. Kwasababu kama ni bandari, nimeenda bandarini nimekuta kuna migogoro na migongano ya kimaslahi. Kuna watu wamefika pale wamefanya ni mahali pa kuchukulia hela wakati nchi haipati pato lolote. Unakuta kuna migongano ya kimaslahi, kuna TRA inafanya yake, kuna TPA wanafanya yao, yaani kuna migongano ya kimaslahi imefikia mahali ambapo hatuwezi kupata kitu chochote. Tumefukuza wadau ambao walikuwa wanaleta hela pale bandarini kwasababu ya migongano ya kimaslahi. TRA anataka vyake, TPA anataka vyake sasa wamefika mahali hakuna kinachoendelea ni wawekezaji kuondoka na kutuacha tukiwa watupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia tulivyofika airport kwenye viwanja vya ndege, nimefika Mwanza; kile kiwanja cha Mwanza nimeona kwenye majedwali inaonesha kwamba wanapewa shilingi bilioni 30, ni kweli tulikuwa Mwanza, tumekuta kuna uendelezaji wa jengo la kuongozea ndege ambalo limejengwa vizuri kwa East Africa nafikiri linaongoza, lakini ukiangalia lile jengo limesimama kwa muda karibu mwaka haliendelezwi kwa sababu halina hela. Na nimeangalia kwenye hotuba ya Waziri inaonesha kwamba anatoa shilingi bilioni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipofika pale tulikuta kwamba kuna shilingi bilioni 20 ambazo Serikali ilitakiwa itoe haikutoa, leo hii unampa shilingi bilioni 30 wakati ana deni halafu mradi ulishasimama. Mobilization ya material mpaka ifike kuanza tena ina maana ni hela zaidi ya hiyo, na hivyo ndivyo vyanzo vya mapato ambavyo Serikali kama ingejikita kwenye vile vyanzo ambavyo ni deal tungeweza tukapata mapato na tukaendesha hizo shughuli zote tunazosema, za maji, za barabara na kadhalika. Hapa hata tupige kelele kama vyanzo hivi tumeshavikalia haiwezekani hata siku moja kutoka hapo!
T A A R I F A...
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante siipokei, naomba akae nayo kwa sababu mimi naelezea kile nilichokiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu kama tutaendelea kupanga bajeti ambazo hazitekelezeki ina maana wananchi wetu tutakuwa tumewatenga mbali sana. Hapa UKAWA na CCM wote tumetoka kwa wananchi, tunahitaji kuwafanyia wananchi ili wapate neema, lakini kama tunafika hapa halafu tunaulizana taarifa wakati mimi nina taarifa sahihi na mimi ndiye niliyezunguka nikaona reality, ninasema haya kwa sababu niliyashuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungekitengeneza vizuri na tukawekeza vizuri kwa hizo hela zilizotengwa siku tulipokwenda Mwanza tungekuta kwamba lile jengo kwenye kiwanja kile liko mbali sana na umaliziaji. Kiwanja cha Mwanza kinajaa maji, ndege kubwa zinashindwa kutua kwa sababu wakati mwingine kunakuwa na ukungu, hamna viongozea ndege ambavyo wakati wa ukungu ndege zinaweza zikatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vyote hivyo kwa shilingi bilioni 30 haiwezekani. Nimesema hayo kwasababu kama tunaimarisha bandari, viwanja vya ndege tunaweza kuwa na pato ambalo tunaweza kuendesha nchi na tunaweza kupata hayo yote ambayo mmeomba, barabara, maji, afya na kadhalika. Fahamu kwamba afya, maji, elimu hivi vyote ni consumer wa mapato kutoka vyanzo kama bandari na viwanja vya ndege. Viwanja vya ndege vikizalisha vizuri ndipo tunaweza tukapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa niunge mkono msemaji aliyepita. Tumepita mawasiliano, tumekuta kweli wanasema kwamba watazima huo mtambo, lakini tukajiuliza nchi yetu ya Tanzania ambayo ina wataalam ambao wanawezakugundua, wapo kwa ajili ya kujua kwamba hizi ni bidhaa fake na hizi ni bidhaa ambazo sio fake. Kama wapo na wanalipwa na wanaruhusu vitu viingie, halafu wateja wanunue, hawa maskini wa kule kwetu, halafu waambiwe mitambo ile inazimwa kwa simu zao fake halafu wakose simu, hivi tunawezaje kulifanya hili Taifa liingie katika uchumi wa kati kama sasa hivi bibi yangu na mama yangu kule kijijini aliyenunua simu fake hatakuwa na simu kuanzia mwezi wa sita? Tunatakiwa tufike mahali tuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuwa wapi wakati simu fake zinaletwa hapa nchini? Kile chombo ambacho kinadhibiti uingizaji wa simu fake kilikuwa wapi? Hao ndio waliotakiwa washughulikiwe, kwamba kwa nini mmeruhusu simu fake zikaingia lakini si yule bibi yangu kule nyumbani ambaye hajui na simu nilimpelekea tu mimi na mimi nikiwa najua nimempelekea simu nzuri. Mnafahamu kabisa simu ndiyo mawasiliano ambayo kila mmoja anaweza akawasiliana na mwenzake. Leo hii tunapowazimia watu karibia milioni 20 hawatakuwa na simu, Taifa tunalipeleka wapi? Na kama Taifa litakosa mapato hayo maji mnayoyaomba humu ndani mtayapata wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba jamani kama kweli tuna nia ya dhati tuhakikishe kabisa Serikali inafuatilia. niishauri Serikali fuatilieni vitu, kama kweli mlikuwepo wakati simu zinaingizwa fake mna kitu cha kujibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninarudi kwenye mawasiliano. Nimeona kwamba kuna watu wanachota hela pale. Kuna makampuni yanachota hela pale kwenye mfuko wa uendelezaji minara…
MWENYEKITI: Ahsante!