Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya. Pia nimpongeze Waziri pamoja na timu yake yote pia kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, niendelee kumshukuru Rais kwa kutupa kilometa moja kila mwaka kwa ajili ya barabara ya kuanzia Magamba hadi Mlola, ambayo ni kilometa 43, hivyo basi kwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa ajili ya uchumi wa Lushoto, kwa hiyo niiombe Serikali yangu tukufu iongeze kilometa hizi zifikie hata kilometa tano kwa kila mwaka, na kama nilivyokwishaandika hapo juu kuwa barabara hii ni muhimu na inaingiza mapato mengi kwenye Halmashauri pamoja na Taifa kwa ujumla. Kwa hiyo niiombe Serikali itenge bajeti kwenye Bunge hili ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, pia Wilaya ya Lushoto ina barabara moja tu ya kuingia Wilayani Lushoto ambayo ni ile inayoanzia Mombo hadi Lushoto ambayo ina urefu wa kilometa 32, lakini pia barabara ile inachangamoto ya wembamba wa barabara, hivyo inasababisha magari makubwa kutopita na kupelekea wananchi kununua mahitaji yao kwa bei za juu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kuna barabara mbadala ya kuanzia Dochi kupitia Ngulwi hadi Mombo ambayo ina kilometa 16 tu, hivyo basi niiombe Serikali yangu tukufu iweze kuona umuhimu wa barabara hii kwa kuitengea fedha za kutosha barabara hii ili wananchi wa Lushoto waondokane na kadhia hii wanayoendelea kuipata kwa sasa. Sambamba na hilo kuna barabara ya kuanzia Nyasa kupitia Gare hadi Magamba ambayo ni kilometa 13 tu na pia ukiangalia ukubwa wa barabara zinazomilikiwa na TANROADS ni kilometa chache mno katika Jimbo la Lushoto, lakini cha ajabu barabara hizi bado hazitengenezwi kwa wakati na hivi ninavyoandika taarifa yangu hii barabara ya Nyasa - Gare ni mbovu mno kiasi ya kufikia kukwama kwa magari hasa wakati wa mvua.

Pia niishauri Serikali zile barabara zinazounganisha Wilaya kwa Wilaya zichukuliwe na TANROADS hasa barabara ya kuanzia Dochi hadi Mombo ambayo ni kilometa 16 tu. Ninaishauri Serikali kuitoa TARURA kwenda TANROADS kwa sababu TARURA haina uwezo wa kuhudumia barabara hii, kwani ni miaka mitano hadi sasa haijatengewa fedha na kuzidi kuendelea kuwapa hasara wananchi wanaozungukwa na barabara hiyo na mazao yao kuzidi kuharibika mashambani.

Mheshimiwa Spika, uwanja wa ndege wa Tanga bado haujapanuliwa kwa sababu ya kutengewa fedha kidogo na ndiyo maana hadi sasa hakuna ndege kubwa inayotua Tanga na ukizingatia Tanga ni mkoa wa kibiashara na ukizingatia bandari yetu imeongezwa kina chake, hii tafsiri yake ni kwamba meli kubwa zitatia nanga sasa. Kwa hiyo uchumi wa Tanga unaenda kufunguka kwa kiwango kikubwa na sambamba na hayo bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda kuja Tanga, mradi huo utamalizika muda sio mrefu. Kwa hiyo miradi yote hii iende sambamba na utanuzi wa uwanja wa ndege wa Tanga, bila kusahau ujenzi wa reli ya kutoka Tanga - Arusha hadi Musoma, miradi yote hii iende kwa pamoja ili kukuza pato la Taifa kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, mwisho Lushoto Mjini kuna eneo linalomilikiwa na TBA, eneo hili limewekezwa na Halmashauri kwa asilimia mia moja na TBA hawa wanainyanyasa Halmashauri kwa kuwadai kodi kwa nguvu na bila utaratibu unaofuata haki na sheria.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu niiombe Serikali irudishe eneo hili kwa Halmashauri ya Lushoto.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.