Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya Makadirio na Mapato ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha hotuba hii katika Bunge lako tukufu. Wizara hii ni miongoni mwa Wizara kubwa katika nchi hii lakini hotuba hii ime-cover mambo yote ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo; nikianza na Shirika la Ndege ATCL. Napenda kuipongza Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake inayochukua katika kuendeleza kuboresha shirika hili. Hili ni Shirika muhimu katika nchi katika dhana ya kuimarisha huduma nyingi pamoja na za biashara. Miongoni mwa madhumuni ya shirika hili ni huduma kwa wananchi. Lakini bado wananchi wa nchi hii wanashindwa kutumia fursa ya kutumia usafiri huu kutokana na ukubwa wa bei. Bei za ndege zetu katika nchi hii kwa usafiri wa ndani ni kubwa sana kiasi ambacho si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuweza kutumia usafiri huu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu katika jambo hili kwa Serikali yetu sikivu ni kuangalia uwezekano wa kupunguza bei za ndege hizi hasa kwa usafiri wa ndani ili wananchi wengi waweze kutumia ndege zao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Chuo cha Usafiri wa Anga; napenda kuipongeza Wizara hii kwa kuweka Chuo cha Usafiri wa Anga. Miongoni mwa kazi za chuo hiki ni kuwafunza vijana wetu kuwa marubani. Hii ni dhana nzuri ya Serikali yetu. Hivi sasa wananchi wengi wanakimbilia nchi za nje kujifunza urubani. Hivyo kuwepo kwa chuo hiki nchini kitawapunguzia gharama zisizokuwa za lazima.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu katika jambo hili kwa Serikali yetu ni kukiboresha chuo hiki kwa kukiwekea miundombinu bora inayofanana na hadhi ya chuo hiki kama vilivyo vyuo vya wenzetu nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, kuhusu udhibiti wa usafiri wa barabara; usafiri wa barabara ni muhimu sana kwa huduma za wananchi. Kutokana na kupanuka kwa huduma wananchi wamekuwa wakisafiri kila wakati kwa kufuatilia huduma za kimaisha. Safari zao zimekuwa za mchana na usiku pia. Lakini kwa sasa Serikali imezuia usafiri wa mabasi usiku. Jambo hili limekuwa likiwasumbua sana wananchi katika kuunganisha safari zao za kutoka mkoa mmoja kwenda kwenda kuwahi muda.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali katika jambo hili ni kuiomba Serikali yetu tukufu kurejesha usafiri wa mabasi ya safari za usiku ili kuwarahisishia wananchi shuhuli zao za kimaisha.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.