Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya ya kukutana hapa katika Bunge lako Tukufu na kujadili hoja hii iliyowasilishwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini ili niweze kumsaidia katika nafasi ya Unaibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia nikupongeze wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge hili. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa jinsi ambavyo tunaendelea kushirikiana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana kaka yangu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii, mama yangu Mheshimiwa Anna Kilango Malecela, na ninaomba tu nimhakikishie kwamba tutazingatia ipasavyo yote waliyoyaeleza kwenye Kamati kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba sasa kwa uharaka nitoe ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyojitokeza sana hasa yaliyojikita kwenye sekta ya ujenzi. Labda tu niwakumbushe Wabunge kwamba mtandao wa barabara za lami wakati tunapata uhuru zilikiwa ni kilometa 1,360, ambazo ni sawa tu na barabara moja upande mmoja, kutoka Dar es Salaam pengine mpaka Mwanza, nchi nzima, lakini leo tunapoongea tuna kilometa 11,512 za lami. Hili ni ongezeko kubwa sana. Ukiangalia kama tulikuwa tuna barabara ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza halafu sehemu yote hiyo ni rough road, unaweza ukapiga hesabu leo tuna barabara kiasi gani.

Mheshimiwa Spika, wakati naangalia ramani ya barabara za India wamechora barabara ya kaskazini, kusini, mashariki na magharibi. Ukituangalia na sisi Tanzania tuna barabara sasa za lami, unaweza ukatoka kusini mpaka kaskazini, ukatoka mashariki mpaka magharibi, lakini pia tuna ring road ambapo unaweza ukaanza Mwanza, ukaenda Musoma, ukaenda Arusha, ukaenda Tanga - Dar es Salaam - Mtwara ukaja Songea, ukaja Bambabay, barabara ambazo tunazijenga; ukaja Tunduma – Sumbawanga – Mpanda - Nyakanazi mpaka Bukoba. Kwa hiyo, tunaweza tu kuona jinsi Serikali za awamu zote hizi sita ambavyo zimeendelea kutengeneza miundombinu.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amejipambua kwamba anataka kuifungua Tanzania, na tumeona jinsi miradi yote iliyokuwa inaendelea, miradi mikubwa hakuna iliyokwama, na hata ukiongea na Wakandarasi wameendelea kulipwa na miradi mingi imeendelea kuanza.

Mheshimiwa Spika, amefungua Tanzanite, amefungua barabara kubwa ya Mpanda – Tabora, Airport Msalato, Ring Road Dodoma, na tunaona BRT zinavyojengwa na barabara nyingi ambazo zinaendelea. Kwa hiyo, tunaomba tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameamua kuifungua Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kila Mbunge angependa barabara yake ijengwe kwa kiwango cha lami, lakini pia niwaeleze tu Waheshimiwa Wabunge kwamba katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka hii tumekubaliana kukamilisha kilometa 1,700 ambazo zilikuwa zinaendelea kuanza ujenzi mpya kilometa 6,000, kufanya ukarabati kilometa 1,465 lakini kufanya upembuzi yakinifu kilometa 7,540 na hasa unaweza ukapiga hesabu ukaziunganisha hizo kilometa ukaona fedha ni kiasi gani. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ni kwamba siyo rahisi tukajenga barabara zote kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakwenda kujenga kwa awamu kadri ilani inavyotueleza. Moja ya mkakati ambao tunakuja nao pia hasa kwenye barabara ambazo ni za changarawe tunakubaliana kwamba katika kipindi cha bajeti inayokuja, tutaainisha maeneo yote katika barabara yale ambayo mara nyingi ndiyo yanatukwamisha kupita, tuweze kuyatengea fedha kuyakarabati. Nadhani moja ya agenda kubwa ya wananchi ni barabara zipitike kwa mwaka wote na ndiyo maana utaona katika kipindi cha kiangazi tunachokwenda, hutakuta wananchi wanalalamika kwamba tumekwama, na watapita; lakini kipindi cha masika ndiyo kelele zinakuwa nyingi. Kwa hiyo, kumbe ni kweli barabara za lami ni muhimu lakini wanachotaka wananchi, waweze kusafiri katika barabara zao mwaka mzima. Kwa hiyo, hilo nadhani tutakwenda kulifanya na litapunguza watu kukwama katika njia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaje barabara chache ambazo tayari zipo kwenye hatua mbalimbali; barabara ya Babati – Mbulu – Hydom. Barabara hii ilitangazwa kipande cha Mbulu – Hydom kilikosa Mkandarasi, tumetangaza tender. Kwa hiyo, tender zipo zinafunguliwa na kipande kinachofuata pia tunaendelea, zabuni zipo. Barabara za Handeni – Kibirashi, lot ya kwanza tayari imeshasainiwa tarehe 11 mwezi wa Nne na Mkandarasi ni Henan Highway Engineering Group ambaye tayari anaanza kazi. Kipande cha Ifakara - Kihansi kilometa 50 ipo kwenye taratibu zinaendelea. Mkiwa - Itigi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, Igawa – Mbeya, kutokana na changamoto ambayo tunayo katika barabara ile, Uyole – Ifisi kilometa 29 tupo kwenye maandalizi ya kutangaza tender lakini Uyole – Songwe – Bypass halikadhalika Iwambi – Bypass na barabara ya Shigamba tunaanza kufanyia Usanifu. Hii yote ni kwa sababu kweli Mbeya mizigo inapita, na ni mji mkubwa ambao pale sasa imekuwa huwezi ukapita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makambako – Njombe – Songea tayari tuna World Bank wamekubali kuanza kuijenga hiyo barabara na tuna hakika hiyo barabara sasa itajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye vivuko. Kisorya – Lugezi – Nyakariro – Kome – Mafia – Nyamisati – Bwiru – Bukondo – Ijiga – Kihangala – Magogoni – Kigamboni – Buyaga – Mbarika, hivi vivuko katika bajeti inayokuja tunakwenda kuvinunua. Hoja ya Mheshimiwa Msongozi kuhusu Mitomoni tumeisikia, lakini mpango uliopo, tumeshapitisha huu mto, tunakwenda kujenga barabara na daraja ni sehemu ya hilo.

Mheshimiwa Spika, vimezungumziwa viwanja vya ndege vya Sumbawanga, Tabora, Kigoma na Shinyanga. Viwanja hivi vimeshapata fedha, tunachosubiri ni no objection kwa sababu tuna price adjustment, tulisanifu muda mrefu lakini kwa sasa tumeomba tuongeze fedha ili tuweze kukamilisha kwa sababu ya tulifanya usanifu, fedha AID walishatuletea na Musoma Mkandarasi yupo site.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. GODFREY KASEKENYA MSONGE): Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)