Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nimepata ridhaa ya kuchangia Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo, kwa hiyo, nianze tu kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na namna ambavyo wamejipanga kuhakikisha yale ambayo wamekusudia kwa maslahi mapana ya wananchi yanatimia. Mwenyezi Mungu awape nguvu ili mwendelee kuitumikia Wizara hiyo vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili kabla sijaanza kuchangia. Kwanza nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipa majosho saba kwenye kata saba kwenye bajeti ya mwaka uliopita; Bukwe, Kigunga, Kinyenche, Nyamagaro, Kitembe, Nyahongo na Mirare. Pamoja na kunipa majosho haya niseme tu Mheshimiwa Waziri, hitaji langu lilikuwa ni zaidi ya hii, kwa sababu shughuli kubwa ya kiuchumi ndani ya Wilaya yangu ukiacha kilimo, shughuli ya pili ni uvuvi, na ya tatu ni mifugo. Kwa hiyo, natamani sana Kata zifuatazo: Kata ya Baraki, Kinyenche, Komugarabo, Nyaburongo, Ikoma, Kisumwa, Kirogoloche na Nyaburongo ziingizwe kwenye Mpango. Nitakuandikia vizuri ili angalau tuone namna gani unatusaidia kwa mwaka wa bajeti unaokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kunipatia fedha hizi za majosho, Mheshimiwa Waziri nikwambie kwamba mpaka sasa hazijaanza kufanya kazi. Sina imani kama wataalam wanakwambia. Hazijaanza kufanya kazi kule vijijini kwa sababu ya namna mlivyozitengenezea utaratibu wa utekelezaji wake. Haya ndiyo tulikuwa tukisema hapa kwamba fedha mnapeleka vizuri, lakini utekelezaji wake unakuwa mgumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mmewaambia Halmashauri itafute Mkandarasi. Inampata Mkandarasi, josho moja mmetenga Shilingi milioni 18; Mkandarasi anatakiwa afanye kwa kiwango kidogo kidogo, ana-rise certificate, Halmashauri inaleta kwenu Wizara, Wizara mnaanza kuandaa malipo, na mpaka uende kumlipa Mkandarasi imechukua muda mrefu. Wamegoma kutekeleza hili. Kwa hiyo, naomba ule utaratibu ubadilike. Pelekeni fedha kwenye Halmashauri kama ambavyo Wizara ya Afya na Wizara nyingine zinavyopeleka fedha, zipelekeni kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuogopa kupeleka shilingi milioni 18 na wakati Wizara nyingine zinawapelekea mpaka shilingi milioni 500. Unashindwaje kumwamini Mkurugenzi kwa shilingi milioni 18 peke yake? Niliona wakala umeandikwa na Katibu Mkuu, naomba huu muu-review. Wapelekeeni wao wapange namna ya ujenzi wa haya majosho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mmepeleka program ya hereni, kuvalisha hereni kwenye masikio ya ng’ombe, sina shida na utekelezaji wake, lakini bei mliyoweka kwa mwananchi wa kawaida shilingi 1,750 ni kubwa sana. Naomba sana muu-review hii ili angalau wananchi wote waweze kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo ni muhimu sana, Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikisema, mpaka wa Kirongwe ambao unatuunganisha kati ya Kenya na Tanzania, zaidi ya kilomita 60 ndani ya mpaka ule, kwa maana ukitoka Bukura kule, Roche, unakwenda mpaka Tarime Vijijini, lile eneo liko wazi. Ukimuuliza leo Afisa Mifugo, mpigie simu, atakwambia kwa siku moja ng’ombe wanaopita bila kulipa ushuru siyo chini ya 300 mpaka 500. Wanapita, wanavuka wanakwenda. Hakuna mnada wowote na hakuna Afisa Mifugo yoyote anayesimama, na hata akisimama, eneo la kilomita zaidi ya 60, anasimama wapi ambapo anaweza kutengeneza control?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukaleta ushauri hapa kwamba eneo kubwa kama hili muweze mnada wa pili ili angalau mnada ule uweze ku-regulate na kusimamia mapato yenu mnayopoteza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napiga hesabu hapa, kwa mwaka fedha mnayopoteza kama wanapita ng’ombe 300, ushuru mliotakiwa mpate shilingi 25,000 kwa ng’ombe, maana yake kwa mwaka mzima ninyi Wizara mmekubali na mmeridhia kupoteza zaidi ya Shilingi bilioni mbili na kitu kwa kila mwaka ambayo ni fedha mngeweza kuikusanya kwa kujenga soko la shilingi milioni 200 au shilingi milioni 300.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri hii aichukulie very serious. Mnaweza mkawa mnakuja mnasema Serikali haina fedha, lakini pale fedha inapotea hadharani. Naomba sana hili, nje ya kujenga soko, muende mka-review bei ya ng’ombe hiyo mnayofanya shilingi 25,000 kwa mfugo mmoja. Wale wananchi wanalalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujue ukitaka kuchukua fedha, tengeneza friendship. Tengeneza mahusiano kati yako na yule unayechukua kwake. Shilingi 25,000 kwa mfugo ni kubwa. Mtu ana ng’ombe zaidi ya 500 au 600, atatafuta mbinu tu za kuwakwepa ili msichukue ile fedha. Kaeni nao muone namna ya kuzungumza kutengeneza friendship ili waweze kulipa hii kodi ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, niende sasa kuchangia kwenye Wizara ya Uvuvi. Niseme tu kabisa Mheshimiwa Waziri, kiukweli tunashindwa namna ya kukukamata wewe, na kwa sababu Waziri wa Fedha yupo, tumegundua namna ambavyo hatujawa serious sana kwenye sekta ya uvuvi. Hii ndiyo inatu-cost leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya ambayo asilimia ndogo sana ya maji ya Ziwa Victoria ina asilimia tano mpaka asilimia sita imeingia kwao, lakini wao wana-export sangara wengi kuliko sisi Tanzania. Rorya peke yake, mzunguko wa maji ndani ya wilaya, nimezungukwa na maji zaidi ya asilimia 76. Yaani Kenya wana asilimia tano, lakini wana-export sangara wengi kuliko mimi niliyezungukwa na maji kwa asilimia 76. Hatujawahi kujiuliza ni kwa nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Uganda wale nao leo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anachangia hapa asubuhi, wao wameamua, wako serious kwenye uvuvi, wameona namna ambavyo samaki wanavyoendelea kukosekana, wameanzisha uvuvi wa vizimba. Sisi kama Serikali hatujaamua namna gani tunaondoka hapo, hata nikiwauliza, toka tumeanza program ya uvuvi haramu 2015/2016 ni nini tume-archive? Kwa sababu lengo lilikuwa ni kuwanusuru sangara wasiendelee kwisha ziwani. Mbona sangara hawaongezeki badala yake wanapungua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali, Mheshimiwa Waziri umefanya presentation lakini hujatuambia sasa nini kinachosababisha sangara hawaongezeki, pamoja na kudhibiti na kuwa wakali kwenye uvuvi haramu? Ni kwa nini? Ni kwa sababu hatujaamua kuwa serious. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wavuvi wangu ndani ya Wilaya yangu ya Rorya, Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikikwambia sana; nje ya u-seriousness wale masikini wa Mungu, wanapanda ziwani, wanakaa zaidi ya siku nne au siku tano anatafuta samaki. Anakuwa ameingia gharama zote kuwapeleka wale wavuvi, kununua mashine, chakula na kitu vingine. Akimaliza uvuvi, anashuka chini anakamatwa na watu wanaitwa mama yao. Sijui kama Mheshimiwa Waziri unaifahamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wanaitwa mama yao, hawana utofauti na wale panya road wa Dar es Salaam. Wanawapiga, wanawanyang’anya hizi mali zao, wanawanyang’anya samaki, wavuvi wanarudi bila kitu, wanalia. Kuna watu Mheshimiwa Waziri wamefilisika; kuna watu kule wametumia mikopo yao kwa ajili ya ku-invest kwenye uvuvi, hawaeleweki; kuna watu wamehama. Leo ukienda Sota pale Shirati, mitumbwi ilikuwa zaidi ya 200 mpaka 300, wamekimbia, kuna mitumbwi 20 tu. Nafiriki Mheshimiwa Naibu Waziri analifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye hili, Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Mambo ya Ndani na wote ambao wanahusika katika pandikizi hili, mwingilie kati muone namna ya kuwasaidia wavuvi wetu. Wenzetu, ukienda Kenya na Uganda kila leo kule ziwani wanalinda. Wako serious wanalinda rasilimali. Hawa ndiyo ukiwauliza wale wavuvi, utasikia tumepigwa na Waganda, tumepigwa na Wakenya, wanataja hadharani, lakini hatujaona u-seriousness wa Serikali kuwasaidia wale wavuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tunasema tuko serious kusaidia sekta ya uvuvi, tunaisaidiaje? Kama watu wanafilisiwa, kama watu wanaondoka, wakija huku wanakamatwa na kanuni za uvuvi haramu, hatuwezi kuwasaidia. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye hili atafute namna ambayo tunaweza tukawasilikiza wale wavuvi na namna ya kuwasaidia wale wavuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu kwenye hilo, tunazungumza kwamba tuko tayari kuboresha na kuimarisha ulinzi kule ziwani; mtakubaliana nami kwamba katika mali ambayo hailindwi ni samaki. Leo ukienda kwenye madini, tumeweka walinzi kule wanalinda; ukienda pale Tanzanite inalindwa day and night; ukienda kwenye sekta nyingine zozote zile ambazo zinazalisha maliasili zinalindwa; ukienda TANAPA, wanalinda. Leo ninyi ni mashahidi, ukienda ziwani hakuna ulinzi wowote unaolinda malighafi tunazozalisha ziwani ili zisisafirishwe kwa njia haramu kwenda nje ya nchi, hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, anasema operation zilifanyika mara tatu. Wenzetu kule Kenya na Uganda brother, hawafanyi operation, wako ziwani wamepiga kambi, wanahakikisha wanachokichuma kinarudi ndani ya nchi yao, wanakizalisha, wanakipeleka nje. Sisi tunafanya operation mara tatu, na operation nyingi mnazozifanya ni za kushughulika na hawa wavuvi haramu peke yake. Hamshughuliki na malighafi ambayo inatolewa, wenzetu wanakuja wanachukua ndani ya Tanzania wanapeleka nje, hakuna ulinzi kule ndani, hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namba, lazima tubuni, tutafute namna ambayo itaimarisha ulinzi kwenye malighafi zetu tunazozalisha ndani ya nchi. Tudhibiti wale ambao wanakuja kwetu wanachukua samaki wanapeleka nje. Mtawapa wengine sifa ya kuonekana wana-export zaidi kwenda nje ya nchi kuliko sisi. Leo tunazungumza, Kanda ya Ziwa, zaidi ya asilimia 75 ya product earning ambayo tunaipata kama mapato ya nje, inatoka Kanda ya Ziwa, lakini wale ndio kila siku mnasikia wanalia, wanapigwa, wananyang’anywa mali zao, hawana vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vizimba tunavyozungumza, vinazungumzwa kwenye karatasi, kule ukienda vizimba halisia hakuna. Namna gani tunawasaidia wale wananchi wa Kanda ya Ziwa? Mkoa wa Mara, nje ya kilimo shughuli kubwa ya kiuchumi kwenye Mkoa ule ni uvuvi. Sisi tunatamani tuone namna gani Wizara mmejipanga kusaidia kwenye sekta ya uvuvi Mkoa ule wa Mara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye hivi vizimba ambavyo tunapitisha kwenye bajeti yake leo, ahakikishe angalau asilimia 60 mpaka 70 inakwenda kule kuwasaidia wananchi wetu, kwa sababu vinginevyo tutaendelea kutegemea uvuvi wa baharini, uvuvi wa kwenye maziwa lakini hauko productive. Kule wanakokwenda masikini ya Mungu mnajua namna ambavyo wanakutana na zile changamoto. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuwasaidia hawa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Jafari. Kengele ya pili hiyo.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)