Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii naomba pia vilevile nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mashimba Mashauri Ndaki na kwa namna hiyo pia vilevile naomba nichukue fursa hii kuwashukuru Makatibu wetu Wakuu, Ndugu Tixon Nzunda na Dkt. Rashid Tamatamah lakini na watendaji wote katika wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee niwashukuru wajumbe wa Kamati yetu wakiongozwa na Mwenyekiti Dkt. Christine Ishengoma; lakini vilevile niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametuchangia kwa kutupa mawazo, fikra na maoni mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Mkuranga kwa kuweza kuendelea kuniunga mkono wakati wote na kuhakikisha kwamba shughuli zinakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wamejadili na katika mijadala iliyokwisha kupita; la kwanza, limekuwa ni jambo linalohusu uwezeshaji wa wavuvi. Naomba niwaeleze kwamba jambo hili limetamkwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi; lakini pia limetamkwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa utayari wa kukamilisha ahadi hizi zilizotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Wabunge wengi wameonesha wasiwasi, nikianza na Mheshimiwa Mwantumu Zodo, ambaye alieeleza juu ya miradi iliyokwisha kupangwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 na haikutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ile ilihusu vichanja, cold rooms, ilihusu mambo mbalimbali yaliyowahusu wavuvi ikiwemo na zile alizoziita matumbawe feki ambayo sisi tunaita FADS, yaani Fish Aggressive Devices. Nataka nimuhakikishie ya kwamba fedha zote zile zilizoandikwa katika mwaka ule tumehama nazo, ilipatikana changamoto ambayo tumeieleza katika risala yetu iliyosomwa na Mheshimiwa Waziri na ninataka nimuhakikishie yeye na Wabunge wote ya kwamba vile vichanja vilivyosemwa vitapatikana katika vijiji alivyovitaja vya Mkoa wake wa Tanga kuanzia Moa, Mwandusi, Tawalani, hiyo Mkinga yote itapata lakini vitakwenda mpaka kule Mtwara alipoishia kusema Mheshimiwa Tunza Malapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakae mkao wa utayari waendelee kuwahakikishia wavuvi wetu hasa wakulima wa Mwani na tena kwa umuhimu zaidi mwaka huu tumeongeza si vichanja vile 52 vitakavyotawanyika mkoa wote katika kilomita zote 1400 lakini tumeongeza zaidi. Katika mpango tulionao mpaka mashine za kukaushia Mwani zipo zimeandikwa katika bajeti hii; na moja ya fedha Bilioni 60 zilizoongezeka zitakwenda kufanya kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, lengo letu ni kuongeza thamani ya mazao yetu na katika kuongeza huku thamani wizara imejipanga vyema. Tumepata wadau ambao wapo serious kwa mfano wadau tuliowataja katika risala kama vile DHL tumekwenda kwa pamoja mkakati wetu wa masoko marketing strategy ambapo tunawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kwa pamoja; vile vikundi lengo letu kila kikundi kimesajiliwa, kipate TBS certificate.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia vilevile kiwe na Barcode yake. Mkakati wetu vikundi vyetu hivi viede kidigitali ndiyo uchumi wa Bluu, uchumi wa kidigitali kwa sababu masoko ya nje yamefunguka na yapo moja kwa moja, tunataka tuukate ule mnyororo wa madalali ili mzalishaji aliyeko kule Moa au Tanganyika anayetengeneza dagaa lake, awe na uwezo wa moja kwa moja kulitangaza soko lake na aweze kuuza bidhaa ile pasipo na shaka yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, ili niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge ambao wameonesha kuwa hawana hakika kwamba kama je hizi fedha zitarudi tena au ziliandikwa halafu ndiyo zimepotea, hizi fedha zipo na nataka niwahakikishieni ya kwamba zitakwenda kufanya ile kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu spika, wapo watu waliozungumzia Bima. Nataka niwaambie kwamba bima ya mifugo na bima ya wavuvi tayari kwa kushirikiana na wizara dawati letu la Sekta Binafsi limeshaanza kufanya kazi na ndiyo maana tumepata mikopo, mikopo imepatikana kwa wavuvi wengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naweza kutaja hapa baadhi ya vikundi ambavyo vimeanza kupata mikopo hiyo. Kule Ukerewe ambako Mheshimiwa Mkundi amesema kipo Kikundi cha Bukasiga kimepata mkopo wa zaidi ya Shilingi Milioni 200. Lakini vilevile pale Sengerema kwa maana ya kikundi cha Kasalazi kimepata mkopo wa zaidi ya Shilingi Milioni 300 na kimeanza kufanyakazi hii hapa; pale Kikumbaitale Geita kwa maana ya Chato wamepata mkopo wa zaidi ya Milioni 200; na kule Kigoma Katonga wamepata zaidi ya Milioni 100; pale Kigoma tena Ujiji kwa maana ya kikundi cha Sangara Beach Amcos kimepata zaidi ya Milioni 70; kwa hivyo, tukichukua fedha hizi za TADB na mkakati tulionao wa hivi fedha tulizopata kwa jitihadi kubwa iliyofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, nina hakika kwamba sasa kazi yetu itakwenda kuwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, unaweza ukaona Wabunge wengi wameshauri kwa sababu kila mmoja anaona namna ambavyo stock inapungua katika maji yetu ya asili; na kwa hivyo tuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika ufugaji wa Samaki na ndiyo maana Serikali imedhamiria kuwekeza katika kuwa-train vijana na wale vijana wote wanakwenda kuwezeshwa kupata mikopo isiyokuwa na riba kupitia Benki yetu ya Kilimo ya TADB kupitia hizi fedha zilizoongezeka ambazo ni takriban Bilioni 60; kwa hivyo, tutakuwa na vituo atamizi zaidi ya 200 katika maji ya Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia tumeona tuanze huko kwa kuwa utafiti umekwishakufanywa na uwezeshaji sasa utakwenda kuwezesha vizimba zaidi ya 900 ambavyo vitakwenda kuwaajiri vijana zaidi ya 1500.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge naomba mtuunge mkono kwa sababu kazi kubwa na nzuri inakwenda kufanywa. Baadhi yenu hapa mmetushauri juu ya kwa nini mavuvi bado ni ya kienyeji? Program yetu inakwenda kuwezesha kununuliwa kwa boti zaidi ya 320, zitakazokwenda kuenea baharini kote kule, hizi boti ni za kisasa zitakuwa na fish finders, GPS, na tayari TAFIRI wameshafanya hii kazi, kazi ya kujua wapi Samaki wanapatikana na program imeshatengeneza tunaita PFZ kwa maana ya Potential Fishing Zones. Kwa hivyo, naomba muwe na Imani na muhakikishe ya kwamba tunaungwa mkono katika bajeti hii na kwa kweli kabisa mambo haya ya Uchumi wa Bluu sasa yanakwenda kufanyiwa kazi. kwa upande wa mifugo pia vilevile kwa ufupi sana tumejipanga na tutakuwa na atamizi za vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulianza hii kazi pale Kongwe TARIRI. Kwa mumalizia naomba kwa heshima kubwa na taadhima Waheshimiwa Wabunge muendelee kutuamini, mtuunge mkono, mtupitishie bajeti yetu hii na Inshaallahu Taallah nawahakikisha ya kwamba kazi hii kubwa na nzuri inakwenda kufanywa. Ahsanteni. (Makofi)