Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya heshima kubwa ambayo ameiletea nchi yetu. Tuzo hii ya Babacar N’Diaye, 2022 imetolewa kwa mtu mashuhuri. Nilikuwa naangalia tofauti kati ya mashuhuri na maarufu. Mashuhuri ni mtu ambaye amejulikana kwa jambo jema, maarufu anaweza akawa hata maarufu kwa mambo mabaya. Kwa hiyo, sasa tuna Rais ambaye ni mashuhuri duniani amejulikana pamoja na mambo mengine ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipoapishwa mojawapo ya kauli mbiu zake kubwa sana ni kuifungua nchi na kukuza uchumi. Uchumi na miundombinu ni sawasawa na chakula na vyombo vya kulia chakula. Miundombinu ndiyo inayofikisha uchumi kwa wananchi. Kwa hiyo, mtu unaweza ukakuza uchumi wa nchi yako. Sasa, kama miundombinu hakuna faida zile zitashindwa kufika kwa wananchi wako. Kwa hiyo, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwasababu amedhamiria kwamba uchumi huu unaokuzwa uwafikie wananchi hasa wale wa maeneo ya vijiji; na ndiyo maana tunapata fedha nyingi kwa ajili ya barabara za vijijini na maeneo mengine. Nchi hii ni pana sana, ina eneo kubwa, inahitaji mtu mashuhuri kuweza kutengeneza miundombinu ya kufikia nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli pamoja na yote ambayo yamesema juu ya miradi tunayoiona kwa macho yetu, miradi ya reli, ndege, meli na kadhalika lakini hayo sisi Watanzania tunayaona kabisa na wala hatuna haja ya kuambiwa na mtu. Kinachonifurahisha ni kwamba hata dunia imeona haya yanayofanyika na kuweza kumfikisha Mama hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, ningependa, kwa vile makao makuu ni hapa Dodoma na Bunge hili tunazungumzia kutoka Dodoma; nilisoma taarifa ya tathimini ya ile Tume iliyotoa zawadi hii, mojawapo ya vitu ambavyo walivizungumzia ni barabara hii ya ring-road ya Dodoma. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba watendaji wetu watahakikisha kwamba inamalizika kwa wakati ili mwaka ujao tupate zawadi nyingine kubwa zaidi kuliko hii ambayo tumepata kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie tu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anapokea tuzo hii jinsi ambavyo imetuma ujumbe kwa dunia. Jambo la kwanza ambalo nimeli-note kwa umuhimu sana, ni kwamba Mheshimiwa Rais wakati anapokea tuzo hii alitambua mchango wa watangulizi wake katika kufikia hapo alipofikia. Kipekee kabisa alitambua mchango wa Serikali ya Awamu ya nne chini ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akatambua Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu ni ujumbe kwa Afrika, kwamba nchi inapokuwa na utaratibu wa kubadilishana madaraka kwa amani na kwa katiba na sheria wananchi wanapata faida kubwa ya muendelezo wa mambo mema ambayo yalikuwa yakifanyika tofauti na pale ambapo tunabadilishana kwa kupambana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili liko jambo ambalo limejibiwa kwa vitendo na tuzo hii. Pamekuwa na dhana kubwa kwamba tunahitaji maono ya Kitaifa. Fine, lakini sasa hapa kuna majibu ya vitendo, kwamba kuna uendelezaji wa mambo ya awamu zilizopita, na siyo kwamba kila awamu inapokuja ina jambo lake. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kipekee kabisa, nalipongeze Bunge lako Tukufu kwa kuja na azimio hili, nampongeza kipekee dada yangu Mheshimiwa Zainab Katimba, kwa kutuongoza kwenye hili na ninaunga mkono hoja hii na ninaomba Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono hoja hii kwa nguvu zetu zote, ahsante sana. (Makofi)