Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru nami kupata nafasi ya kutoa pongezi kwa ajili ya tuzo ya Rais aliyoipata. Sisi kama wanawake kutoka Beijing Platform tulikuwa tunatamani sana wanawake kuwa viongozi kwenye ngazi za juu za maamuzi. Mheshimiwa Rais kwa kupata nafasi hiyo, ninaamini anaitendea haki na ndiyo maana leo tunazungumzia habari ya kupata tuzo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulikuwa tunasikia zamani Corazon Aquino kutoka Philippines kama Rais wa kule, tulikuwa tunasikia habari za akina Margaret Thatcher, lakini leo hii katika nchi yetu tuna Rais ambaye ni kiongozi. Vilevile leo tunapotoa pongezi hizi, kiongozi huyu amekuwa kiongozi wa 12 na inaonesha ni mwanamke wa kwanza kabisa kupata tuzo hii katika benki hiyo. Hii peke yake inamfanya yeye kuwa Balozi wa Afrika ili aweze kupata pesa za kuweza kujenga miundombinu tena Tanzania zaidi ya ile tuliyojenga, tuweze kupata maendeleo ya Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwamba yeye kama ni Balozi na amekuwa mwanamke wa kwanza kupata tuzo hiyo, basi nafahamu nchi za kwanza za dunia na za pili zitaona umuhimu wa kuleta fund katika nchi yetu ya Tanzania na kuweza kumsadia kumalizia majukumu yake hasa ya miundombinu ambayo bado kama Taifa tunahitaji kuijenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia kiongozi kupata nafasi, ni kusimamia kile ambacho watu wamekuamini wewe kukifanyia kazi. Nasi wanawake tuko vizuri sana kwenye maamuzi; tunapoamua kufanya kazi ya maamuzi tunasimamia kweli kweli. Mwanamke ana nguvu ya kuamua, mwanamke anapoamua kufanya kitu chake anaweza kufanya na akalisaidia Taifa kwa ajili ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe ni mwanamke, tunaona maamuzi unayofanya na kazi unavyoisimamia. Vivyo hivyo na sisi Wabunge wanawake tunapoamua; tukiamua, wako wanawake ambao hawaamui, lakini wanawake wanapoamua mambo yao, wakiona yana msingi kwa Taifa lao, wanasimamia wanachokiamini. (Makofi/Vigelegele)
MBUNGE FULANI: Haleluya! (Vigelegele/Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, niseme hivi; Mheshimiwa Rais, sisi kama wanawake unachokisimamia, kisimamie; simamia Watanzania, tuzo uliyoipata ni ya kwako, lakini ni ya Watanzania, hususan wanawake. Tunakuamini kwa kile unachokifanya lakini hiyo iwe ni chachu ya kusimamia mambo makubwa ambayo yako mbele kama Taifa na kama wanawake tunaenda kuyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nampongeza kwa tuzo hii na atakapofika airport ninaamini wanawake watakuwa wa kwanza kwenda kuipokea tuzo hiyo maana ni ya kwao. (Makofi)