Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naungana na wenzangu wote kwanza kutoa pongezi nyingi na kuunga mkono hoja iliyoletwa hapa ya kumpongeza Rais wetu kipenzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipotaka nianze mimi, ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kuwaandaa viongozi. Mama Samia Suluhu Hassan aliandaliwa kuwa kiongozi. Kwa hiyo, pongezi za kwanza kabisa tukipe chama ambacho kilimwandaa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa kiongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa nataka tukumbushane kwamba mwaka wa 2000, Mama Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na akapewa kuwa Waziri wa Afya katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mwaka wa 2005 akaendelea na nafasi hiyo ya uwakilishi na akawa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mwaka wa 2010 akapewa kuwa Waziri katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anayehudumu kwenye shughuli za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengi tunakumbuka hapa mwaka wa 2014, wakati tunahangaika na suala la Katibu mpya, Mama Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Ilipofika mwaka 2015, Mama Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa nini nimeyasema haya? Ukiona vimeelea ujue vimeundwa. Mama Samia Suluhu Hassan aliandaliwa na sasa ameonesha umahiri mkubwa sana katika uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nije katika tuzo. Afrika peke yake ina nchi 54, lakini kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi zilizoko duniani ni 233. Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatajwa kuwa kiongozi mwenye ushawishi na maarufu katika dunia ambayo ni viongozi 100 tu ndiyo wamepata sifa hiyo katika Mataifa 233 duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwakumbushe Watanzania, huu ushawishi Mama Samia ameuonesha kwa kiwango kikubwa wakati tunahangaika na mapambano ya COVID-19. Alikwenda katika Jumuiya ya Kimataifa kuomba fedha, wengine wakaomba fedha za barakoa, wengine wakaomba fedha za sanitizer, yeye akaomba fedha kwa ushawishi, wakamkubalia fedha hizo zisambae katika kupambana na COVID kwa kupeleka kwenye elimu, kwenye afya na kwenye maji. Kwa hiyo, tukawa tumepata faida mara mbili, kwamba tunapambana na COVID lakini tunasaidia kutatua changamoto katika sekta ya elimu, afya na maji. Huu ndiyo ushawishi unaozungumzwa kwa kiongozi wetu, anaweza akakaa na chombo chochote duniani akasema na akasikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanikiwa katika miundombinu, wala hili halina ubishi. Nitumie nafasi hii kusema kwamba naunga mkono hoja iliyotolewa hapa ya kumpongeza Rais wetu na kwa kweli tujiandae kumpokea na kuendelea kumpa ushirikiano mkubwa, ahsante sana. (Makofi)