Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

Hon. Omar Ali Omar

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nianze kwa kusema kwamba Waswahili wanasema, kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Pia kuna Mwalimu mmoja wa Kiswahili, Shaaban Robert katika kitabu chake cha Adili na Nduguze, alisema kwamba, haja ikishughulikiwa kwa matendo, humalizika upesi, lakini ikichelewa, huchelewa kama sadaka ikishughulikiwa kwa maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya matendo. Anawaachia watu wakazungumza maneno; na nime-quote speeches zake nyingi anasema kwamba, “kuna watu watatusikia, watatuona kwa matendo yetu lakini walio wengi watatupongeza na walio wachache watasema watabeza.”

Kwa hiyo, sote tuliomo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeziona juhudi za Mama Samia, amezifanya vizuri kabisa, hata kwenye Jimbo langu najisifia kwamba sasa hivi juhudi za Mama Samia naziona. UVIKO-19, kuna majengo ambayo yanajengwa ndani ya Jimbo langu kwa fedha za UVIKO-19. Zimetoka kwa nani? Kwa Mama. Kwa hiyo, ni kuonesha kwamba Mama ana juhudi kubwa kabisa ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe mfano mmoja mkubwa kabisa ambao huo ni kisa maarufu na kinaendelea mpaka leo duniani. Mama Hajra wakati alikuwa anatafuta maji, alikuwa anakwenda Kusini na Kaskazini, Mashariki na Magharibi kutafuta maji; nani aliyekuwa akitafuta maji? Ni mama. Matokeo yake maji yalipatikana. Kwa hiyo, hii ni kuonesha kwamba mapambano ya mama, ni mapambano makubwa na ataendelea kupambana mpaka dakika ya mwisho kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono azimio hili kwa asilimia mia moja. Ni azimio ambalo lina mashiko, lina mwelekeo; na tumpe moyo Mama yetu aweze kutuongoza vizuri, na kila mtu aliyekuwa ana nia mbaya kwetu sisi na kwa Tanzania hii, basi Mungu ndiye anayejua vipi anaweza kumshughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nina ombi maalum kwa Bunge. Kwa vile tuzo aliyopewa mama ni ya kwetu, tutayarishe jambo maalum la kumpokea Mama katika tuzo hii ili tuone sasa kwamba kweli tunamthamini kwa tuzo hii aliyoipata ni ya Watanzania wote. Kwa hiyo, nasema kwamba Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kasema wanawake waende, lakini na wanaume sote twende tukaipokee hiyo tuzo. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)