Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa Duniani na kupewa Tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais. Kweli Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia uongozi wa Mama Samia ukizingatia kwenye wakati tuliopita ni wakati mgumu sana, lakini hata baada ya kuondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Magufuli, tumempata Rais ambaye ameenda kuonesha Afrika kwamba Tanzania ni nchi ambayo inadumisha amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza mchangiaji mmoja dada yangu Mheshimiwa Tendegu na mimi nimekuwemo Bungeni huu unaenda mwaka wa saba, ni azimio la kwanza kwenye Bunge linaungwa mkono na vyama vyote hata na upinzani ikiwemo CHADEMA, lakini amezungumza vizuri sana dada Mheshimiwa Tendegu kwamba wanawake wanaweza hasa wakiamua jambo lao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikwambie, kwa uongozi wa Mama Samia, sio wanawake tu wanaoufurahia hata sisi wanaume tunamfurahia sana, hata Vvyama vya Upinzani, hebu angalia leo Mbowe ndio anaongoza kwenda Ikulu, najua alipa-miss sana, lakini amepata nafasi ya kuingia na kutoka zaidi ya mara tano. Hongera sana kwa Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na ushindani wa nchi zaidi ya 54, lakini Mama Samia ameongoza, nafananisha na ligi ya Tanzania, kama alivyosema mama wa afya ya akili kwamba tumemnyang’anya Nigeria ambaye ndio alikuwa na tuzo hiyo. Ni sawa na Tanzania tu, tunatarajia kumnyanganya mnyama very soon labda Jumapili na ningemwomba Mama Samia huko aliko anisikilize, najua atakuja, nimkaribishe sana Mwanza tumpe zawadi ya Kitanzania. Najua aliyopewa kule ni tuzo aje tumpe mnyama kesho kutwa hapa tunavyomchinja, apate zawadi. Najua tulimpa uwanja wa Taifa alipokuwa mgeni rasmi, aje na Mwanza kule Jumapili tutampa zawadi kama alivyozoea kupewa hata akiwa kule Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukizunguka kila jimbo hapa utakuta mtambo unatengeneza barabara. Nimekuwa Mbunge miaka saba, nimelia lami humu miaka saba, leo hata Jimbo la Geita Vijijini tuna kilomita 25. Kwa niaba ya wananchi wa Geita Vijijini, tunamwombea mema sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukienda vijijini pamoja na kwamba hatuwezi kujenga lami kila mtaa, kila kijiji, lakini leo tuna pesa za kutosha kujenga barabara zinazopitika mchana na usiku.

Mheshimiwa Spika, sasa utanisamehe sana sisi Wasukuma huwa tukifurahi hatuna maneno mengi, ningekuomba mimi sitaruka sarakasi, wala sipigi magoti, tukifurahi sisi Wasukuma wamo humu wenzangu watanisaidia tunafanyaje?

WABUNGE FULANI: Tunaimba.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Tunafanyaje.

WABUNGE FULANI: Tunaimba.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, sasa naomba niimbe wimbo, utaniruhusu? Tuna imani na Samia…

WABUNGE FULANI: Oyaa, oyaa, oyaa.

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma! Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Musukuma magoti na sarakasi haviruhusiwi humu ndani ni pamoja na kuimba, hairuhusiwi. (Makofi/Kicheko)