Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata hii fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye Wizara hii muhimu sana ambayo imebeba maslahi mapana ya Watanzania. Kwanza naomba niungane na wewe na niungane na Bunge lako Tukufu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa tuzo ya mafanikio ya ujenzi wa miundombinu na kuwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa duniani. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, tuzo hii anaistahili sana.

Mheshimiwa Spika, pia kuna jambo jingine halijasemwa lakini mimi kwenye kupitia pitia tu mitandao nimeona Mheshimiwa Waziri Stergomena Tax ameonyesha tuzo nyingine ambayo ameipata Mheshimiwa Rais kwenye Pan African Woman Organization, ametambuliwa kama Rais wa kwanza mwanamke katika Afrika Mashariki, Rais mwanamke pekee kwa mwaka 2022 pia kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kufanyakazi kama kiongozi Mkuu wa Serikali. Hayo yote naomba yaunganishwe kama pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kutambua mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nilitaka nichangie na niliombe Bunge lako Tukufu litoe maelekezo kwa Serikali linahusu hali halisi ya eneo letu tunalofanyia kazi eneo la Bunge. Upande wangu huu wa kulia tuna barabara ya Dodoma – Morogoro, Waheshimiwa Wabunge wengi wamepaki magari ng’ambo ya pili ya barabara na siku za karibuni kumekuwa na ajali mbalimbali, siku mbili tatu zilizopita pia Mheshimiwa Francis Ndulane alipata ajali pale, yeye ni mmoja katika Wabunge kadhaa ambao wamekuwa wanapata ajali eneo lile kwa sababu ndani ya eneo la Bunge hatuna maegesho ya kutosha, maeneo ya kuegesha magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia upande huu wa mbele katika geti la Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna barabara ambayo inatoka Hazina inakwenda kuungana na barabara ya Morogoro, eneo hilo wanapita watu wa aina mbalimbali lakini Bunge lako Tukufu kwa mazingira yaliyopo na umuhimu wake na Viongozi waliopo humu wanahitaji ulinzi na usalama wa hali ya juu. Lakini pia leo Wabunge wako ili waweze kushiriki kwenye mazoezi ya kujenga afya zao waweze kulitumikia Taifa hili vizuri wanalazimika kwenda nje ya maeneo haya, wanakodi viwanja maeneo mbalimbali ya Mji, eneo hili lingeweza kutosha kwa huduma kama hizo.

Mheshimiwa Spika, zipo hoja nyingi ambazo zinaonyesha kwamba eneo hili la Bunge halitoshi kutoa huduma za kisasa, tunazo changamoto za ofisi za Wabunge, Wabunge hawana ofisi huku, hata wananchi wangu wa Madaba wakija hapa nakutana nao canteen, mimi ni Mbunge nilihitaji nikae nao katika maeneo ambayo tunaweza kuongea masuala ya maendeleo. Kwa hiyo, moja katika mambo yatakayoliwezesha Bunge lako Tukufu kufanya kazi vizuri ni kuwa na mazingira rafiki salama yatakayowafanya Wabunge wafanye kazi kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninatambua hatua ambazo Bunge limefanya moja ni kwamba limejaribu kutathmini na kuthaminisha maeneo haya ya Bunge yenye majengo na viwanja vilivyo wazi. Hiyo kazi najua Bunge wamemaliza lakini niiombe Wizara sasa ichukue jukumu hili la kuisaidia Bunge kwa haraka zaidi kuyapata hayo maeneo ili tuweze kuwa na Bunge la kisasa linaloweza kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, naelewa tupo kwenye hatua za mwisho za kupitisha bajeti yawezekana jambo hilo kibajeti halijakaa vizuri. Bunge lako lina mamlaka linaweza kuitisha Kamati ya Bajeti ikakaa na Serikali tukafanya amendment ambazo zitaruhusu kuingiza hizo bajeti za kumaliza hili tatizo ambalo litaenda kuboresha utendaji wa Bunge lako na hivi Watanzania watapata huduma bora wanazozihitaji, hilo lilikuwa ombi langu la pili.

Mheshimiwa Spika, ombi la tatu kama kuna Wizara imeweza kuitikia wito wa Watanzania kuhusu migogoro mbalimbali ni Wizara hii ya Ardhi na hizi credit zimwendee kwanza Mheshimiwa Waziri wa sasa, Dada yangu Mheshimiwa Angelina Mabula, pia mtangulizi wake Mheshimiwa Lukuvi, kwa kweli hawa wamefanyakazi kubwa sana nchi hii. Mimi nimepata bahati ya kuhusika katika kupanga na kuleta majina ya watu watakaozungumza kwa mara ya kwanza nimeona mapendekezo machache sana ya watu wanaotaka kuongea kwenye Wizara hii, kwa sababu migogoro mingi imetatuliwa na Serikali kupitia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana mtangulizi wake Mheshimiwa Mabula, yeye mwenyewe Mabula na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ridhiwani wanafanyakazi nzuri sana. Ninazo salamu mahsusi toka Madaba wananchi wa Madaba walipomuona Mheshimiwa Mabula ameenda Mbeya walivyomuona ameenda Mwanza walivyomuona ameenda maeneo mbalimbali akitatua migogoro ya wananchi wakasema tunatamani Mheshimiwa Waziri aje na Madaba kwa sababu wanayo imani nae sana.

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi haiwezi kuendelea kutatuliwa na Mahakama pekee, Mahakama zina utaratibu ambao unachelewesha sana, tujifunze kwa Mzee Lukuvi wakati ule anakwenda ndani ya Mkoa, anakaa na wananchi anatatua mgogoro mpaka leo hatujasikia kelele katika maeneo hayo. Huduma kama hii kwa Madaba na Mkoa wa Ruvuma bado hatujaipata kikamilifu. Mheshimiwa Waziri ninakuomba wananchi wanayo imani kubwa sana na wewe, wananchi wanaimani kubwa sana na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, wananchi wanayo imani sana na Watendaji wako wanaamini ukiendelea kwa mwendo uleule Tanzania hii migogoro itapungua kwa kwa asilimia kubwa.

Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya migogoro ambayo utaikuta kwenye maeneo yetu inachangiwa na taasisi zingine za Serikali, mimi ninaamini dhamana ya ardhi imekabidhiwa Wizara ya Ardhi hii ni Wizara ya kisekta. Mwananchi mwingine yeyote na idara nyingine yoyote na Wizara nyingine yoyote ya Serikali ni watumiaji wa ardhi, wana mamlaka sawa kama mwananchi mwingine mwenye ardhi. Pale inapotokea mwananchi ana matumizi na ardhi, Serikali kupitia Idara zake wanaihitaji hiyo ardhi basi Wizara ya Ardhi isimame kama Hakimu anayetenda haki kwa kila pande. Madaba tuna mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kipingo na watu wa hifadhi lakini watu wa hifadhi wametumia ubabe kuchukua maeneo ya wananchi, utaratibu huu hauwezi kuleta afya.

Mheshimiwa Spika, wewe unajua Mheshimiwa Rais ni kipenzi cha watanzania wanyonge, ni Mama mpenda haki hataki kuona Mtanzania yeyote anaonewa ndani ya nchi hii, Mama Mabula naomba endelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kuwasimamia wananchi kupata haki zao za ardhi wakiwemo wananchi wa Kipingo, wananchi wa Ngadinda, wananchi wa Mkongotema, wananchi wa maeneo yote ya Madaba na Mkoa mzima wa Ruvuma na Tanzania katika ujumla wake.

SPIKA: Sekunde 30, malizia sentensi.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)