Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma aliyenijalia afya njema hadi siku ya leo nikafika kwenye mkutano wetu huu. Pili nimshukuru Mheshimiwa Rais wote ni mashuhuda hakika anaendelea kufanya kazi nzuri ya kuendelea kutuletea maendeleo Watanzania. Niipongeze Wizara kwa maana ya Waziri mwenye dhamana Naibu wake kaka yangu Wakili Msomo Ridhiwan Kikwete lakini pia na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya leo kwa kweli tunaona kuna improvement kubwa kwenye Wizara hii. Kwa sababu hadi mwaka wa fedha uliopita, nilikuwa najaribu kuangalia takwimu, viwanja vilivyopimwa nchini vilikuwa takribani milioni sita, lakini leo hii tumeona hapa kwenye hotuba ya Waziri wa Ardhi sasa tunakwenda milioni saba, tunaona kuna improvement.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa historia tu nieleze, hapa nchi yetu ilianza kupimwa mwaka 1896 ndipo kiwanja cha kwanza kilipimwa hapa nchini, sasa ukiangalia muda hadi sasa tulipofikia unaona bado tunakazi kubwa ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nirejee maneno ya Hayati Baba wa Taifa, alisema nchi yoyote ili iweze kupiga hatua ya maendeleo lazima iwe na siasa safi kwa maana ya utawala bora, lakini watu na mwisho ardhi. Ardhi ni hazina kubwa sana kwa Taifa letu, na kila kitu unachokitaja kipo kama sio chini basi juu ya ardhi. Tukizungumzia madini ardhi, mito ardhi, kwa hiyo ardhi imebeba uchumi wa nchi yetu. Baada ya kueleza haya naomba nifanye comparison hapa na wenzetu jirani wa Kenya; nijaribu kuoanisha takwimu za Kenya na nchi yetu, (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 24 Aprili, 2021 saa Nne usiku Waziri wa Ardhi wa Kenya akihojiwa na Television ya the citizen alieleza kwamba nchi ya Kenya mpaka sasa wana hati miliki milioni 11. Sasa najaribu kulinganisha Kenya na sisi nikirejea kwetu mpaka leo tunapozungumza kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri tuna hatimiliki yaani wananchi waliomilikishwa ardhi ni Milioni 2.3 utaona wenzetu wapo mbali sana, lakini naona kuna jitihada. Nimeeleza, mwaka uliopita hatimiliki nchini zilikuwa 1,500,000 tu lakini leo tunazungumzia milioni 2,000,000, kuna improvement. Sasa ushauri wangu ninaokwenda kutoa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye sekta hii ya upimaji Wizara ya Ardhi kama custodian au kama ndiyo mamlaka ya usimamizi wa sekta ya ardhi nchini, ushauri wangu kwake ingeendelea kubaki hivyo inavyofanya kuratibu na kusimamia sekta ya ardhi, na mamlaka za upimaji kwa maana ya Halmashauri kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya Mwaka 2007 mamlaka za upangaji ni halmashauri. Sasa hoja ninayokwenda kushauri hapa ni lazima sasa Wizara Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ardhi waje pamoja wawe na mpango wa pamoja. Kwa sababu kule kwenye halmashauri, halmashauri ziko chini ya Wizara TAMISEMI lakini ardhi ipo Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara hizi zinatakiwa zifanye kazi pamoja. Kwa mfano ukienda kwenye level za mikoa wasimamizi wa sera na shughuli za Serikali kwenye level ya mkoa ni Wakuu wa Mikoa. Ni muhimu sasa wakashirikishwa, wawe na ownership ya upimaji ili wasimamie vizuri zaidi. Serikali peke yake haiwezi kufanikisha jambo hili, lazima kuwa na engagement ya private sekta. Kuna kampuni za upimaji, hapo awali kulikuwa na hoja ya kwamba kampuni za upimaji hizi zimekuwa zikiwadhulumu wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri atakuwa ni shahidi, tulikosea mahali. Hapo nyuma ilikuwa kampuni zilikuwa zinakwenda moja kwa moja kukutana na wananchi, kamati za ardhi zinaundwa katika level ya vijiji au mitaa, halafu wanaingia mkataba ambao kimsingi hakuna mashiko ya kisheria kwamba anaweza kuwa huyo mkandarasi akikataa kufanya kazi na akiwadhulumu anaweza kuwajibika mahali popote pale. Sasa hivi naona kuna mfumo mzuri sasa, na mimi nishauri eneo hilo. Kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri ndio waingie mikataba sasa na hivi kampuni au kandarasi za upimaji, mwananchi yeye asubiri huduma tu. Hii itatusaidia kudhibiti wizi au dhuluma kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze faida za upimaji, ardhi ikipimwa kwa Serikali lakini pia kwa wananchi. Mwananchi akipimiwa ardhi yake iwe shamba anapata hati anakwenda benki anakopesheka, na jitihada za Wizara ya Kilimo maana yake mwananchi mwenye shamba anaweza pia akakopesheka na akaendelea kulima na nadhani nchi ikaendelea vizuri. Lakini pia si tu mkulima, mwananchi wa kawaida anaweza kufanya biashara. Akiwa na hati miliki anakopesheka, ardhi inapanda thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukiongeza kasi upande wa Serikali, kwenye ardhi kuna tozo mbalimbali. Kwa mfano, mathalani kwa Mkoa wa Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam una idadi ya watu takribani milioni sita. Tuchukue tu, tufanye sampling watu 1,000,000 tuwape hatimiliki za Dar es Salaam, hiyo fedha kiasi gani? tukipata milioni moja tu wenye hati miliki kwa Mkoa wa Dar es Salaam watatusaidia kuwa na sustainability mapato kwenye tozo za adhi. Kwa mfano kuna land rent mtu analipa, akifanya transaction ya kuuza kiwanja au nyumba analipa capital gain tax analipa stamp duty; hivi fedha zote ni maduhuli ya Serikali. Kwa hiyo mimi niendelee kusema tu kwamba pamoja na pongezi zangu kwa Wizara ya Ardhi tuna kazi ya kufanya ili kuongeza kasi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni eneo la mfumo wa ILMIS. ILMIS (Integrated Land Management Information system) ni mfumo ambao una hifadhi taarifa za sekta ya ardhi; na huu mfumo umeleta matunda bora. Leo Mheshimiwa Waziri amezungumza hapa, tunaona mafanikio ya hati hizi za kwenye mtandao; mwananchi akipimiwa; kwa mfano tunazungumzia viwanja milioni saba na tunazungumzia umilikishaji millioni mbili, kuna gape kama milioni tano hawana hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiongeza kasi hapo kwa mfumo wa ILMIS. tuka-integrate nchi nzima; na nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa sababu yupo hapa, na ananisikia; tukiongeza fedha kwenye Wizara ya Ardhi tukawawezesha wakai-integrate mfumo huu wa ILMIS, nchi nzima, na mtanzania akawa na uhakika akipimiwa kiwanja atapata hati miliki tutakuwa mbali sana. Kwa hiyo tuwekeze nguvu hapo kama Serikali ili tuweze kufanikiwa eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka kwenye eneo lingine, eneo la sekta binafsi nimeeleza lakini niombe kitu kimoja; sekta binafsi bado ina hali ngumu tutafute namna bora ya kuiwezesha, hasa kampuni za upimaji; kama kwa ruzuku au njia yoyote bora ambayo tunaweza kupeleka fedha au mikopo nafuu ili mtu akopesheke. Hii kampuni ya kijana wa Kitanzania aliyesajili kampuni yake, amejiajiri na anaajiri watu wengine, akiwezeshwa, kwa maana ya kama si ruzuku basi apewe mkopo nafuu; anaweza akafanya vizuri zaidi na nchi yetu ikapimwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine la migogoro ya ardhi, kumradhi migogoro ya ardhi ni matokeo tu ya failure sekta, tukiri kabisa, wananchi wanakimbia sana kuwekeza wanakimbilia sana kwenye ardhi, sisi kama Serikali bado tupo nyuma. Kwa hiyo migogoro ya ardhi ni matokeo ya failure ya sekta ya ardhi, wala si chochote, kwa hiyo tukisimama ardhi hii tukai-manage vizuri, tukaipima nchi nzima hata migogoro ya ardhi itakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa nirejee eneo moja; nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kulikuwa na migogoro ya ardhi kwenye vijiji 975, Mheshimiwa Rais mwenye mapenzi mema na Watanzania amesema sasa katika vijiji hivi havifutwi vyote Watanzania, vijiji 920 anasema vikarasimishwe, jambo hili ni la kumpongeza Mheshimiwa Rais, katika hili tumpongeze Mheshimiwa Rais; na siasa zetu zingekuwa ngumu kidogo kama vingefutwa hivi vijiji. Kwa hiyo leo hii, nadhani hata wananchi wa Jimbo la Mlimba wananisikia; kuna changamoto moja tu ambayo nimuombe Mheshimiwa Waziri aifanyie kazi. Bado kuna maeneo pale Jimboni kwangu yanashida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata ya Mofu Kijiji cha Ikwambi na Karenga, leo hii watu wa TAWA bado wanawasumbuwa. Kwa hiyo nadhani ni muhimu sasa, kwa kuwa Serikali inakwenda kurasimisha vijiji hivi wenzetu hawa wa maliasili wangetulia kidogo na wananchi watulie kidogo mpaka Serikali itimize wajibu wake kwenye eneo hilo. Sasa, utekelezaji bado. Kwa hiyo pending ya utekelezaji ni muhimu sasa watu wa TAWA lakini pia na wananchi wangu wa Ikwambi na maeneo hayo niliyoyataja watulie kusubiri utekelezaji wa Serikali kwa kuwa Mheshimiwa Rais mwenye mapenzi mema na Watanzania amesema virasimishwe. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuhitimisha. Kata nyingine ni Kata ya Mchombe Kijiji cha Mbasa Kitongoji cha Shamba la Saba, Utengule na Ipugasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja na Mheshimiwa Waziri naona hii chemistry, aa’ bwana, Mungu awabariki tu. Huko tunakokwenda naona tunakwenda kulamba asali. Ahsante sana. (Makofi)