Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze tu kwa kusema kwamba hii Tuzo ya Babacar Ndiaye ambayo Rais alitunukiwa juzi ni kielelezo kwamba Afrika na Dunia inatambua kwamba viongozi wetu wa Chama cha Mapinduzi na Serikali ya Tanzania wanafanya kazi zao kwa maslahi ya wananchi walio wengi. Hongera sana Rais Samia pamoja na Serikali nzima kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tamko la Azimio la Arusha lililopitishwa kule Arusha tarehe 29 mwezi wa Kwanza mwaka 1967 na kutangazwa na Mwalimu Nyerere pale Dar es Salaam tarehe 5 mwezi wa Pili mwaka 1967 kama uamuzi wa Watanzania kuondoa unyonge wao kiuchumi bado baadhi ya mauzui yake yana umuhimu sana hadi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Azimio la Arusha, sura inayozungumzia wananchi na kilimo ukurasa wa 22; Mwalimu Nyerere anasema, nanukuu: “Maendeleo ya nchi huletwa na watu, hayaletwi na fedha. Fedha ni matokeo, siyo msingi wa maendeleo.” Anasema, ili tuendelee twahitaji vitu vinne; kwanza watu; pili, ardhi; tatu, siasa safi; na nne, uongozi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imepita miaka 55 tangu Azimio la Arusha, na kadri miaka inavyosonga mbele ndani ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa yaliyoanza katikati ya miaka ya 1980, nchi yetu kama sehemu ya dunia kwa sasa inazidi kutambua nguvu ya mtaji katika maendeleo, na hasa katika uwekezaji, mitaji ya uwekezaji kwenye sekta za kilimo, viwanda na biashara. Polepole tunaanza kutambua kwamba tunahitaji mitaji ili tufanye kazi za maendeleo hasa kwenye uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi ya uwekezaji nayo ipo minne. Msingi wa kwanza wa uwekezaji ni gharama nafuu za usafiri na usafirishaji na ndiyo maana Serikali inawekeza sana kwenye miundombinu, sitaki kuitaja. Msingi wa pili ni gharama nafuu za huduma za uendeshaji wa mitambo, maana yake hapo utahitaji mafuta; upatikanaji wa mafuta wa uhakika, utahitaji maji ya uhakika, umeme wa uhakika na mambo mengine yanayofanana na hayo kwa ajili ya kuendesha mitambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa tatu wa uwekezaji ni upatikanaji wa uhakika wa malighafi viwandani kwa mwaka mzima na hapo ndipo unakuta kuna umuhimu wa kuwekeza kwa ajili ya kuongeza uzalishaji katika Sekta ya Kilimo. Kilimo kinalimwa vijijini, hakilimwi mjini; hapo ndiyo point yangu ipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa nne wa uwekezaji ni nguvu kazi yenye ujuzi ambayo ni ya uhakika. Ndiyo maana Serikali inatakiwa kuwekeza sana kwenye vyuo vya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwa na misingi hiyo minne kwenye uwekezaji tutafanya vizuri. Sasa tatizo liko wapi? Kama alivyosema Mwalimu Nyerere, tunahitaji watu, ardhi safi na uongozi bora, tatizo kubwa lipo kwenye ardhi mpaka sasa hivi. Ni rahisi mtu kusema mbona ardhi tunayo ya kutosha? Unawezaje kui-transform ardhi ilete nguvu ya kiuchumi katika nchi? Iweze kusisimua uchumi wa nchi? Ndiyo maana huwa naamini kila siku kwamba Waziri wa Ardhi ndio Waziri wa Uchumi, kwa sababu hakuna activity yoyote inayoweza ikafanyika katika dunia hii nje ya ardhi. Hata kama ni madini, lazima uyachimbe kupitia ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ardhi ndipo penye tatizo la msingi. Hadi sasa Watanzania wanaomiliki ardhi ni chini ya asilimia 10. Hili ni tatizo kubwa. Tuna sheria zetu kuu mbili za ardhi; Sheria Na. 4 ya vijiji na Sheria Na. 5 ya Ardhi ya jumla kwenye miji na maeneo mengine yaliyohifadhiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kwenye miji lina unafuu kidogo kuliko tatizo lililopo vijijini, kwa sababu mjini mtu akikomaa katika kufuatilia ardhi yake atapatiwa hati, lakini kijijini hata ukikomaa, kama kijiji chako hakijapimwa mpango wa matumizi bora ya ardhi, huwezi kupata hati ya kimila. Hapo ndiyo tatizo lipo. Kwa sababu tuna fursa nyingi sana sasa hivi za mitaji kupitia benki, hata Serikali imewezesha benki kama CRDB na NMB zinatoza 9% tu kwenye mikopo ya kuwekeza kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fursa kama ipo kwenye kilimo, na kilimo kinalimwa vijijini, watu watawekezaje kwenye kilimo kama hawawezi kukopa kwenye benki? Hapo ndiyo tatizo la msingi lipo. Watu wanaomiliki ardhi kwenye vijiji ambavyo havijapimwa, hawawezi kuitumia fursa hiyo kwa sababu sheria ya mikopo inayohusu kuweka rehani chini ya masharti maalumu; “The Mortgage Financing (Special Provisions) Act, ya mwaka 2008 inaweka utaratibu ni namna gani mtu atumie hati yake kuweka rehani nyumba, ardhi au kitu chochote kisichohamishika. Sheria hii inawapa unafuu watu wa mijini. Watu wa vijijini hawana unafuu wowote kama kijiji hakijapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naweka point yangu vizuri, na ninaomba sana Serikali iweke kipaumbele katika kupima ardhi ya vijijini. Aidha kupima au kuweka provision nyingine kwenye sheria ambazo zitamruhusu mtu wa kijijini aweze kupata hatimiliki ya kimila kwa haraka iwezekanavyo na siyo kusubiri ile milolongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Taifa ya Upangaji wa Ardhi Vijijini inasema kwamba tuna vijiji 12,665 na taarifa ya Tume ya Ardhi inasema mwaka huu wa fedha 2021/2022 walipangiwa kwenye bajeti Shilingi bilioni 1.5 peke yake; na hadi Februari mwishoni walikuwa wamepewa Shilingi milioni 800. Katika hizo milioni 800 wamepima vijiji 239.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Sheria ya Ardhi ipitishwe mwaka 1999, hadi leo nilivyosimama hapa Bungeni kuzungumza, Wizara ya Ardhi imeweza kupima vijiji 2,560 peke yake, kati ya vijiji hivyo nilivyovitaja. Ina maana hii ni asilimia ngapi? Ni asilimia 20, bado vijiji 11,005. Kama kasi hii ya kupanga fedha, Shilingi bilioni 1.5 itaendelea hivyo, Wizara ya Ardhi itachukua miaka 140 kupima ardhi yote ya vijijini. Sasa hii ni hatari. Maana yake ni kwamba tutachelewesha maendeleo ya Watanzania kwa muda wa miaka 140. Iina maana upimaji utakamilika mwaka 2,160, nani atakuwa anaishi hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo ndipo kwenye tatizo kubwa. Naomba sana wananchi wa vijijini, Serikali iweze kuwapa haki ya kumiliki ardhi tena kwa haraka, tusipoteze muda. Ninashauri hatua mbili Serikali itekeleze. Hatua ya kwanza Serikali ifanye marekebisho ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji ili mtu yeyote mkazi wa kijijini ambaye anatambuliwa na register ya kijiji kama mwanakijiji, kama atataka ardhi yake ipimwe apate hati ya kimila, asisubiri mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji yote. Kwa hiyo, apate nini? Apate mambo matatu; kwanza, apate Muhtasari wa Mkutano Mkuu wa Kijiji kwamba anaruhusiwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji kupima ardhi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, muhtasari huo wa Mkutano Mkuu wa Kijiji uidhinishwe na Kamati ya Ardhi ya Baraza la Madiwani. Ukishaidhinishwa upate approval ya Mkuu wa Wilaya husika ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi ya Wilaya. Akishapata hivyo vitu vitatu, huyo mtu apimiwe ardhi yake bila kusubiri. Hiyo ndiyo itakuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia sentesi yako Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia. Hatua nyingine ya pili ambayo napendekeza kwa wale watu ambao wanalenga kuitumia ardhi kwa ajili ya kuweka rehani, kwa ajili ya kupata mikopo vijijini Waziri wa Fedha na Mipango, alete marekebisho kwenye Finance Bill ya mwaka huu 2022 ambayo itaruhusu sasa Watanzania wanaotaka kukopa kwa kuweka rehani mali zao vijijini, wapimiwe ardhi zao kwa approval ambazo nimesema hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ninaomba Serikali itekeleze hayo maoni ambayo nimeshauri. (Makofi)