Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nami kwa kunipatia fursa ya kutoa mchango wangu. Nianze kwanza kwa kuwapongeza sana mtangulizi wa Wizara hii, Mzee wangu, Mheshimiwa Lukuvi alifanya kazi kubwa, lakini nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mama yangu Angelina Mabula na Naibu wake Ridhiwani, mnafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri ambazo zinafanyika ndani ya Wizara hii, baadhi ya mambo yanatia dosari, hata ule uzuri wa mambo makubwa ambayo yamefanyika unakuwa hauleti ladha. Jambo hilo ni migogoro ya ardhi. Kila maeneo ndani ya Taifa hili huwezi kukosa migogoro sugu ya ardhi. Pamoja na kwamba kamati zinaundwa, lakini huwa migogoro ya ardhi ndani ya Taifa hili inachukua muda mrefu na hakuna suluhu, wala huoni kama kuna mwaka wa kuleta suluhu kwenye migogoro hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano. Nichukue mfano wa mgogoro mmoja ambao nadhani ni mgogoro kongwe ndani ya Taifa hili ni GN 28 ya kule kwetu Mbarali. Huu mgogoro tangu mimi niko binti, sasa hivi naelekea utu uzima, mgogoro huu bado na hatuelewi hata nini hatima yake. Kwa masikitiko makubwa zaidi, hii Kamati ya Waheshimiwa Mawaziri nane, imefika Mbeya mara mbili na wananchi walikuwa wanaisubiri kwa hamu mno wakijua kwamba sasa ile neema iliyotangazwa na Mheshimiwa Rais kujua ni vijiji gani vitarasimishwa virudi kwa wananchi au vibaki kwenye hifadhi vitatajwa, Mbeya kamati hii imekuja mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza walipofika waliishia Mbeya Mjini, wakasema tutarudi tena. Wamefika mara ya pili mwezi uliopita, hakuna majibu. Wamesema sasa hivi tunauachia mkoa, watakuja kupitia upya. Kwa kweli inatia uchungu. Leo hii ukifika kule nyumbani kwetu Mbarali, muulize hata mtoto wa miaka mitano, akutajie matatizo matatu ya wilaya hii, atakwambia la kwanza ardhi, lapili ardhi, la tatu ardhi, atasahau hata shida za maji wala barabara. Ni kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mgogoro huu tumepoteza ndugu zetu. Wanawake wamepoteza waume zao, watoto wamepoteza baba zao kupitia mgogoro huu, watu wanapoteza maisha. Siku moja alikuja Mbunge wa Jimbo letu la Mbarali, Mzee Mtega, alileta Taarifa Binafsi humu ndani, Waheshimiwa Wabunge walitokwa na machozi jinsi unyama unavyofanyika kisa mgogoro huu. Inasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa takribani miaka 15, kila siku wananchi hawajui hatima yao. Halafu wananchi wa Mbarali siyo mara yao ya kwanza kuhamishwa. Walihamishwa; vijiji 10 vilishahamishwa na watu hawapo maeneo hayo waovu, lakini sasa hivi ngoja nikutajie; maeneo kwa mfano, Msangaji, Upagama, Ukwaheri, Idunda, Ikoga, Kapunga, huku kote watu walishaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zilizoonyeshwa, ni kwamba wakibaki watu maeneo haya wataathiri Mto Ruaha, na maeneo hayo hakuna watu, sehemu kubwa watu waliondoka. Baada ya watu kuondoka maeneo hayo, walikubaliana kati ya mamlaka zilizokuwepo na wananchi. Hawa watu waliondoka bila mtutu, wakaambiwa na wakaelewa. Baadaye wakakubaliana mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limekuja kutoka tangazo la GN 28, wamekuja hata lile eneo ambalo hawa wananchi walihamishiwa Luhanga na kwenyewe kukaonekana tena kuko ndani ya hifadhi; vijiji 33 vingine vipo ndani ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi wana-Mbarali hatima yetu ni nini? Kwa kweli tunaumia. Kila siku tunapata misiba. Kweli Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ishindwe kufanya maamuzi kwenye jambo hilo ambalo linatesa watu hivi! Siyo sawa. Wamekuja Waheshimiwa Wabunge mbalimbali humu ndani, kila siku GN 28, kila siku linaongelewa na taarifa zinaletwa, lakini hakuna. Yaani tunachukulia rahisi tu. Siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekit, tunaamini kabisa viongozi wetu wa juu ambao ni Waheshimiwa Marais huwa wanakuwa ndiyo wamiliki wa ardhi kwa niaba ya wananchi, na kwenye hili tayari kuna matamko mbalimbali ya viongozi wetu ambayo yametolewa kwa kuwaambia; ngoja nianze kwanza kunukuu. Februari, 2015 aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Mheshimiwa Lazaro Nyalandu alifika Mbarali, alitumwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, alisema haya yafuatayo, nakukuu: “Mheshimiwa Rais wetu ameridhia, baada ya wananchi wa kata hizo zilizoondolewa, hakuna mwananchi yeyote atakayeondolewa katika vijiji vilivyobakia.” Kwa hiyo, wananchi endeleeni na shughuli zenu za maendeleo, akaendelea: “ninaagiza viongozi wa Mkoa wa Mbeya, Njombe na Iringa muanze kuchukua hatua za haraka za kurekebisha tangazo hilo lililoleta mabadiliko ya mipaka ya eneo hili kwa ajili ya kupeleka Bungeni, kwa ajili ya kubadili sheria hiyo.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 4 mpaka tarehe 6 mwezi wa Kumi 2018 Hayati Rais wa Awamu ya Tano aliagiza Makatibu 11 waende Mbarali wakiongozwa na Katibu Mkuu aliopo Ofisi ya Waziri Mkuu, Mambo ya Sera na Uratibu Prof. Faustine Kazomola, huyu ndio alikuwa kiongozi wa kamati hiyo, walikaa Mbarali kwa siku hizo tatu; tarehe 4 mpaka tarehe 6 kushughulikia suala hilo. Baada ya hapo, Januari, 2019 tarehe 15, naomba ninukuu maneno ya Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. Magufuli ambaye ndio alikuwa guarantor wa land hii hapa, alisema: “Vijiji vyote vilivyobainishwa viko ndani ya hifadhi, visiondolewe. Ninaagiza mamlaka husika zianze kufanya mchakato wa kuvirasimisha vijiji hivyo. Natoa mwezi mmoja mchakato wa kuanza mabadiliko ya sheria ili yapelekwe Bungeni.” Tarehe hiyo hiyo ndiyo aliyoteua kamati ya kwanza ya Mawaziri nane kushughulikia migogoro hii na migogoro mingine ambayo haijapatta ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekit, sisi tulitarajia baada ya kauli ya Mheshimiwa Rais hii, kazi ya kwanza ya Kamati pamoja na migogoro mingine ambayo ipo maeneo mengine, kazi ya Kamati kwa Mbarali ilishatolewa maelekezo na maeneo ambayo ni hatarishi watu walishaondoka. Kuna shida gani Mbarali? Kuna shida gani Mbarali? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)