Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Ninazo salamu kutoka Jimbo la Tarime Vijijini kwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wakimpongeza kupata tuzo na kutambulika kama kiongozi mashuhuri duniani katika viongozi 100, na bahati nzuri amepeleka fedha za miundombinu barabara ya kutoka Tarime – Mugumu na Mkandarasi yuko site, watalii wataongezeka, watapeleka ujumbe kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii kama ambavyo wenzangu wamezungumza ni Wizara ambayo ingeweza kutuvusha sana na kuwafanya watu wakaendelea, lakini kwa kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba kuna mambo manne ili nchi iendelee, eneo la ardhi bado kuna shida kubwa sana. Mheshimiwa Waziri lazima ajipange na wenzake Naibu Waziri kufanya kazi hiyo kwa kweli. Karibu kila jimbo kila mahali kuna migogoro mingi ambayo imedumu kwa muda mrefu zaidi na palipo na migogoro maana yake hakuna maelewano, hakuna maendeleo, ni ugomvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwangu kule Tarime Vijijini, tunayo madai ya wananchi wangu ya kulipwa fidia, ukienda eneo la Nyamichele tangu 2019. Nenda pale Murwambe, Matongo na Komarera kule kuna shida. Haya mambo ni muhimu yakafanyiwa kazi, kwa sababu eneo la Tarime kwa asili sisi watu ni wengi, ardhi ni kidogo sana haitoshi. Hata vita ya koo ambayo ilikuwa inapigana kule Tarime mnasema Warenchoka na Wanchali mpaka mkatubatiza majina kwa sababu shida kubwa ni ardhi, watu hawana sehemu ya kulima. Sasa kule Tarime ardhi ni finyu, haitoshi lakini wananchi wanajua kwa uhakika kwamba ndani ya ardhi yao kuna dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ambayo inalipwa, eti hekari moja Serikali inalipa Shilingi Milioni tano. Hata Waziri akipewa fedha hiyo akatafute ardhi hawezi kununua kwa kiasi hicho. Bahati mbaya wametengeneza migogoro wenyewe, wanachukua tangazo wanabandika kwamba ardhi hii tutaihitaji, yaani mwananchi akiona umebandika tangazo aache kulima, kujenga au kuendeleza chochote kile kwa sababu utamlipa. Hakuna mkataba, hakuna makubaliano, hivi ikitokea mwekezaji hataki eneo la mtu na hakuna makubaliano, unafanyaje? Hayo ndiyo madai yaliyopo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyamichele waliwaambia wasubiri watawalipa, hawakulipwa mpaka leo. Matokeo yake wale Wazungu wa Mgodi wa Barrick wamechimba underground. Watu mazao yao yalikatwa, nyumba zilibomolewa, watu wana shida muda mrefu sana. Katibu Mkuu Kijazi alipita kule Nyamichele, akanikuta Tarime, nikamwambia watu wa Nyamichele wanataka kauli ya kiongozi, tathmini inafanyika lini? Unajua walimsimamisha hata hakusalimia kabisa akafunga vioo akaondoka, nikapata wakati mgumu kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waambie viongozi kazi mojawapo ya Mheshimiwa Rais kumsaidia ni kutatua kero za wananchi, hata kama huna majibu. Wananchi wanalalamika, simama uwasikilize, utapokea hoja zao, utasema nimezibeba, naenda kuzifanyia kazi. Hayo maeneo ni vizuri fidia ikalipwa, Nyamichele, Komarera na Murwambe. Katika maeneo haya kuna mazao ya watu mengine nimeambiwa yalikatwa, kuna majina pale yapo. Mheshimiwa Waziri alikuwa Naibu Waziri kwenye Wizara hiyo, walikuwa na Mheshimiwa Lukuvi, walifanya kazi nzuri sana, siyo vibaya akiiga au akaendeleza walikoishia, kwa sababu anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapendeza sana wananchi wakilalamika, kiongozi aende awasikilize. Asiende Musoma Mjini, aenda awasikilize, kuna malalamiko mengi ambayo wananchi hawana majibu. Sasa kuna uchonganishi unafanyika pale Tarime kwenye eneo la mgodi. Wale valuers wanaowatuma, wanawaambia gharama ni ndogo imepangwa. Ukienda kwenye mgodi wanasema fedha zipo za kuwalipa, wanatuchelewesha. Wanaona viongozi wa Serikali hatuwasaidii, Wabunge hatuwasemei, mgodi una fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara waende ili waondoe changamoto hiyo, waongee lugha moja. Kile ambacho mgodi unasema lazima pia kauli hiyohiyo iende kwa wananchi. Wasiamini kwamba hatuwezi kuwasaidia ili waweze kulipwa fedha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni muhimu sana kama kuna makubaliano wanataka waingie na wananchi wenye maeneo yao na kumekuwa na tabia ya kuchelewa kuwalipa, kuwe na mkataba kwamba kama unachukua eneo langu unakaa nao miaka miwili, miaka mitatu, ikitokea wewe hujanilipa fidia na mimi sikujiendeleza unalipa compensation ya kuchelewesha muda. Mtu anakaa miaka 10, enelo lake hajawahi kulipwa mpaka leo na hakuna chochote kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanalalamika sana wananchi, ni muhimu kuwa na makubaliano. Nchi hii inaongozwa kwa sheria, tufuate sheria za ardhi. Kama unataka eneo langu tukubaliane, unalipa fidia, hulipi fidia, unipe muda ambao umenichelewesha kufanya kazi za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, mipaka ya hifadhi. Katika watu ambao kwa kweli wana mambo mengi ya kulalamikia ni pamoja na Tarime Vijijini. Eneo la Kata ya Nyanungu, Kata ya Gorong’a, Kata ya Nyarokoba, Kata ya Kwihancha ni maeneo ambayo kumsikia mtu amepotea, siyo ajabu. Kwamba watu wamechukua ng’ombe za watu wameenda kupiga mnada mchana kweupe, siyo ajabu, kwamba mtu ameliwa na fisi, siyo ajabu, kwamba Kamati imeundwa na hakuna majibu, siyo ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli alikuwa na nia njema na Mheshimiwa Rais Mama Samia ameunga palepale, ametoa maelekezo akafanya maamuzi. Yaani Mawaziri Nane wanashindwa kwenda kusikiliza wananchi wenye migogoro, wanaenda kukaa Musoma kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kweli? Wanashindwa kwenda site, wanasoma beacon ambazo yaani wamepokea taarifa ya SANAPA. Yaani mimi Waitara namlalamikia hapa Amar, halafu wewe unakuja unachukua taarifa za Amar, unanihukumu nazo. This is not fair, siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitarajia kwamba katika kutatua hii migogoro, viongozi waende wakae chini, Mbunge, Diwani, Mkuu wa Mkoa, DC na wananchi wote wawepo ndiyo watu waseme migogoro na tutatue hizo changamoto. Hii habari ya kujifungia na kutuandikia taarifa siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wemekwenda Musona na Mheshimiwa Waziri alikuwepo, lakini hawakwenda Nyamungo, Gorong’a, Kwihancha au Nyarukoba, lakini wataalam wake wamewaambiwa wananchi Mbunge wenu alikuwepo, alishirikishwa, je, Mheshimiwa Waziri anataka nyumbani kwangu wachome moto? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wakienda wakaweka beacon, wakahamisha watu, Mbunge maana yake ameridhia watu wahamishwe, lakini kama ningekuwepo na wananchi wakawepo, wale wananchi wamezaliwa pale miaka ya 1980, miaka 1970 wanajua mipaka yao, wangesaidia maelezo kwa Mheshimiwa Rais kwa nia njema ili afanye maamuzi, watu waishi. Kwa kweli hakuna maendeleo kule, sasa kumekuwa na chuki kati ya watu wa hifadhi, wananchi, viongozi, hapaeleweki, duniani hatupo, ahera hatupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima watusaidie vizuri, siyo sawasawa kwa kweli na migogoro imekaa muda mrefu sana. Ukiona kila Mbunge hapa analalamika kila kona, hawa Mawaziri ni muhimu sana. Pia ni muhimu hili Bunge, mambo yote ambayo yamekaa muda mrefu, malalamiko ya majimbo mengi, ya wananchi wengi, Bunge litoe muda maalum wa changamoto hizo kutatuliwa. Tusiwe hewani hewani, kama tunawapa miezi sita, Mheshimiwa Waziri akafanye kazi na wenzake, alete majibu kwenye Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ilivyo kila mtu anajisikia. Nilisikia wanasema eti hawana hela ya mafuta kwenda kule Nyamongo, eti mtaalam hana hela ya kwenda kule kuangalia migogoro ya wananchi. Wananchi hawa ili tuwaongoze vizuri lazima tuwasikilize, lazima tutatue changamoto zao, usipofanya hivyo itakuwa siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, migogoro ya wakulima na wafugaji. Hii Wizara kama nilivyosema Mheshimiwa Waziri akifanya kazi vizuri na wenzake na uwezo huo anao labda maamuzi tu, ni muhimu sana kwa sababu haiwezekani Wabunge wa Bunge hili, unajua watu wanauana kule, mwenye ng’ombe ni adui wa mkulima, mkulima ni adui wa mfugaji na sisi ni viongozi, Serikali ipo, sheria ipo, ardhi haipangwi, hii haikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima watu wetu waishi kwa ustaarabu. Kama kuna mtu anafuga tujue wapi wanafuga ng’ombe, mbuzi, kondoo, maeneo yatengwe. Kama kuna sehemu watu wanalima tujue wanalima sehemu hiyo, iende, ndiyo uongozi wa nchi. Haitakuwa sawa kama tunakaa hapa watu wanauana, Watanzania wenyewe kwa wenyewe wanauana. Watu walewale, jamii ile ile halafu kuna Mbunge, kuna Diwani, kuna Viongozi, siyo sawasawa. Lazima tukubaliane, maeneo yapimwe, wale wafugaji wale siyo maadui wa wakulima, ila viongozi hatujachukua nafasi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi tupange mpango vizuri, watu wanaofuga ng’ombe wafuge, au mfugo wa aina fulani wafuge, anayelima alime ili tuuziane. Hawa wanahitaji nyama, huyu anahitaji chakula, kuna shida gani? Tupangeni, jambo hili ni muhimu sana. Mbunge kusimama hapa anakutajia watu waliouwawa, hawajaugua, siyo bahati mbaya, kwa mapanga na sisi viongozi tupo, hilo lazima lifanyiwe kazi na Bunge hili kwani kazi yake ni hiyo kulinda watu wake, kuwasimamia Watanzania waishi kwa ustaarabu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, yeye alikuwa Naibu Waziri na ameenda kutatua mgogoro pale Mlitolegebasi. Watu walipigana mishale, wakapigana mapanga kwa sababu ya ule mgogoro, mpaka leo Mheshimiwa Waziri hajawahi kwenda pale na ule mgogoro upo. Kwa hiyo, wakati wa uchaguzi tunafanya kazi ya kugombea na kusuluhisha migogoro. Tumalize migogoro sasa kabla ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda wakati wa uchaguzi unaambiwa wewe umekuja kwa sababu unataka kula, Hapana. Tumesema mara kadhaa, tunawakumbusha tena, mahali popote katika majimbo yetu, kwenye mikoa yetu, kwenye wilaya yetu, kwenye vijiji vyetu, vitongoji vyetu, tarafa zetu, Waziri aainishe migogoro hiyo waifanyie kazi, tusifanye kazi ya kuzima moto, muda wanao, nafasi wanazo, dhamana wamepewa, watatue changamoto za wananchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili, Mheshimiwa Mwita.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika eneo hili ningependa nijue Mheshimiwa Waziri fidia ya Nyamichele, Komarera, Murwambe ni lini? Nitashika shilingi na nitakatalia mpaka Tarime Vijijini aifuate kule Nyanungu kwenye mgogoro wa ardhi, ahsante. (Makofi)