Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipatia ili niweze kuchangia mawazo yangu kwenye hoja hii ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hii tuzo aliyoipata kama Azimio la Bunge la leo lililofanyika hapa nami niunge mkono kumpongeza Rais wetu kuwa mwanamiundombinu bora. Tuendelee kumwombea, achape kazi kadri Mwenyezi Mungu atakavyomjalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya na nilifarijika sana leo alipoanza kusoma hotuba yake ndani ya Bunge amesoma kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu. Naamini Roho Mtakatifu atamshukia na haya nitakayoyasema leo humu ndani, Roho Mtakatifu aliyemwomba amwongoze katika kusoma hotuba yake akamwongoze pia katika kuyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa lililofanya nisimame katika Wizara hii leo ni jambo ambalo limekuwa sintofahamu kwa takribani miaka 13 sasa. Jambo lenyewe linahusu uwekezaji wa mwekezaji aliyekuja kuwekeza katika Shamba la Malonje ambaye anaitwa Efatha Ministry. Hili jambo ukiliongelea na akifika kule Mheshimiwa Waziri, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Lukuvi pamoja na yeye akiwa Naibu Waziri, wamepigana nalo jambo hili na miaka mitano hii ilivyopita palikuwa na utulivu kidogo, lakini ninavyoongea sasa hivi jambo hili limefufuka upya na hali ni mbaya sana kutokana na huyu mwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu alikuja mwaka 2009, alipewa shamba lililokuwa la NAFCO, hekta 25,000, aliuziwa kwa Shilingi Milioni 600, kwa maana hekari moja aliuziwa Shilingi 24,000. Alipofika pale yeye alikuja kama mwekezaji anayekuja kufuga na baadaye makubaliano yalibadilika kwamba yeye atafanya shughuli ya kilimo. Sasa shida ilikuja pale ambapo alianza kuingilia mipaka ya wananchi wanaozunguka shamba lake hilo hekta 25,000. Sitaki kwenda mbali kwenye historia, lakini nataka niende kwenye matatizo yaliyojitokeza kwenye uwekezaji huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na shida ya unyanyasaji kwa wananchi, analazimisha kwenda kuingia kwenye vijiji ambavyo mipaka yake haipo. Kijiji kimesajiliwa, kimepewa hati kabisa, huyu mwekezaji anaenda analazimisha hata eneo la kijiji aendelee kulimiliki yeye. Naomba hapa Mheshimiwa Waziri anielewe, siyo kwamba yule ni mwekezaji, namwita dalali na nina sababu ya kumwita dalali kwa sababu hekta 25,000 alizokabidhiwa, hajafanya uwekezaji unaofikia hata hekta 1,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ardhi kwetu ina thamani kubwa sana. Ile ardhi inaweza kusaidia nchi kuondokana na upungufu wa zao la ngano kwa sababu ndiyo ardhi yenye rutuba kubwa. Sasa hivi nchi yetu tunaagiza ngano nje, tunatumia zaidi ya Bilioni 520 na uzalishaji wetu kama nchi tunazalisha tu tani 70,000 na mahitaji ni tani milioni moja. Eneo lile analomiliki yule Efatha Ministry linaweza likazalisha tani 44,000 na kuondoa nakisi. Ina maana nusu ya ngano tunayozalisha ndani ya nchi hii lile shamba linaweza kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye alikuja kuchukua lile shamba, akafanya likawa collateral, akaenda kutafuta financing kwenye financial institution, baadaye aka-deviate zile fund, hamna kinachoendelea, ni mateso kwa wananchi. Kuna wananchi wangu wa pale Sikaungwi, juzi tu ameenda na bulldozer, zaidi ya ekari 70, ameenda kukatakata mazao, tena kwa kutumia vyombo vyetu vya dola, vina-facilitate mtu kufanya uhalifu wa kukandamiza haki ya wananchi wanyonge maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja hapa leo, Wizara iliwapa wale hati na nyaraka zote toka Wizarani ninazo hapa nitakabidhi mezani. Nawaomba jambo moja, kama huyu ambaye anahodhi ardhi ambayo haina manufaa miaka 13 iko idle, wanamwona ana maana kubwa na ana muscles kuzidi Serikali, niwaombe jambo moja, wawachukue wananchi wale 5,722 wa pale Sikaungu wawatafutie eneo kama walivyowatafutia watu wa Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu hawawezi kwenda kuishi pale, hawana shamba la kulima na ni maisha yao, wale siyo wafanyakazi walioajiriwa, ajira yao ni kilimo, sasa wamempa mtu amehodhi, amechukua hati ameenda kuchukulia fedha kwenye mabenki, wananchi wanakaa hawana mahali pa ku-develop mambo yao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe mama yangu Mheshimiwa Waziri, jambo hili lina sintofahamu kubwa. Siyo Kijiji cha Sikaungu tu, kuna Kijiji cha Sandulula, Msanda Muungano, kuna Kijiji cha Songambele Azimio, Malonje kwa ndugu yangu Aeshi na pia Mawenzusi naye atasimama atasema. Hali ni mbaya, wananchi hawaelewi jambo lolote. Mwekezaji huyu kwa nini anafugwa? Amechukua hekari 25,000, haendelezi chochote, hamna kazi inayoendelea, yuko tu pale. Sisi tuna shida, mimi nimepiga hesabu zangu, kama tungepata mwekezaji proper kwenye ardhi ile tungeweza kupata mapato kama halmashauri kwa mwaka shilingi milioni 500. Kwa miaka 13 tungekuwa tumejenga vituo vya afya 13 kutokana na mapato ambayo halmashauri ingepata kwenye shamba lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri na Naibu nimeteta naye sana na jambo hili najua Waziri alikuwa Naibu Waziri analijua. Ilifikia hatua mpaka huyu mwekezaji anakata wananchi masikio, yaani masikio. Kuna mwananchi mmoja anaitwa Martin yuko pale Sandulula mpaka leo ni mlemavu anavyopigwa na yule mwekezaji. Mbaya zaidi kuna wananchi basi kwa sababu wana fedha na anaweza akahonga hapa na pale, aliweza mpaka kusababisha wananchi wakafungwa gerezani miaka mitano, wameenda na mahakama ikakuta hawakuwa na hatia, lakini wale wananchi wamepoteza miaka mitano gerezani. Wananchi wa Sikaungu hawana hatia yoyote, masikini ya Mungu wamerudi ni maskini, lakini kwa sababu wanajua haki yao hawaachi kupambana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suluhu labda kama Wizara itashindwa kuwatafutia sehemu ya Kwenda, wajiandae wale wananchi wako radhi 5,000 wote waje wawaue palepale, wawazike Sikaungu. Kwa sababu haiwezekani, mwekezaji huyu ana ubabe gani? Kumekuwa na vitu fulani vya ajabu mimi naviona pale, mwanzoni mnakuwa timu ya watu wengi mna-fight, baadaye unaona wenzako wanarudi nyuma kwenye mamlaka hizi hizi za Serikali. Ukishaona hivyo ujue wenzako wamepigwa mlungula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi peke yangu, mimi Deus Clement Sangu niliyechaguliwa na wananchi wa Jimbo la Kwela nitasimama peke yangu, hata ikinigharimu Maisha, kwa sababu haiwezekani wananchi wananyanyasika sana. Ule mgogoro umeleta adha kubwa, wananchi mwaka huu hawajalima na kidogo walichokuja kulima amekuja kupita na bulldozer, eti anaweka mipaka. Mipaka si pande mbili mnakaa kama kuna mipaka mnaweka? Hivi wewe unaweza ukatoka peke yako ukaja kujiwekea mipaka? Haiwezekani jambo hili! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli mbaya iliyoniudhi, naomba niiseme na kwa kweli Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Mambo ya Ndani nawaomba sana, kauli ya mwekezaji kuja kuongea, kudharau mamlaka ya nchi hii ambayo imekaa kihalali, sitakubaliana. Akirudia tena ama zangu ama zake kule jimboni. Yeye anasema kwamba, haya, mliyemtegemea amekufa, sasa narudi na kweli miaka mitano yote; Mheshimiwa Lukuvi ni shahidi, palikuwa kimya. Siku tatu baada ya Hayati Magufuli kufa akaja halafu anatamka kauli za kudharau mamlaka halali ya nchi hii, sitakubali. Kama wa kwanza kupigwa risasi kwenye shamba lile la Wanasikaungu nitakuwa mimi Mbunge wao niliyekuja kuwawakilisha ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wamwambie kauli za kukashfu mamlaka za nchi hii iwe mwisho. Aishie huko huko, asije kudharau mamlaka, wananchi wanampenda Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia, wanamuunga mkono, asije akafanya kwamba yeye ni mbabe kuliko Serikali. Tutamalizana huko huko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kwa uchungu mkubwa, naona nchi ambavyo hatupigi maendeleo, tunalia humu Bungeni hata ndugu yangu Mheshimiwa Bashe nilimwambia haiwezekani, sisi tuna ardhi yenye rutuba, ardhi nzuri iko idle mtu mmoja amehodhi tu haendelezi, njooni tufanye maamuzi, nikamshauri Bashe amwandikie barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna vijana wengi graduates hawana ajira, wanahangaika Jimboni kwangu. Tungeenda pale tukafanyia block farming, wakapewa mle mkopo na Benki yetu ya Kilimo. Nimeenda Benki ya Kilimo nikafanya mazungumzo, wakasema tunahitaji ku-finance kwenye sekta ya ngano, lakini watapata wapi ardhi? Kuna mabepari wamehodhi ardhi na hawaendelezi, vijana wetu wanarandaranda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, kwa kweli nitalisimamia hiliā€¦(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Deus Sangu.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha tu, mama sitaunga mkono, nitashika shilingi mpaka aje atupe majawabu yanayostahili juu ya mgogoro wa lile shamba. Wananchi wa Sikaungu, Sandulula na Msanda Muungano wamenituma nije nipaze sauti humu ndani ya Bunge. (Makofi)