Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa haraka napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza viongozi wenzetu walioteuliwa Mama Anjelina pamoja na ndugu yangu Ridhiwan ambaye kule kwenye Bunge Sports Club huwa tunamwita super sub yaani yule mchezaji anayeingia kipindi cha pili akishasoma mchezo, akiingia basi mambo yanakuwa vizuri magori yanatililika na ndiyo maana tukawa mabingwa kwenye michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, naamini hata huko kwenye ardhi, ataendeleza mazuri anayoyafanya tukiwa uwanjani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Katibu Mkuu, mzee Kijazi, ni mtu rahimu pamoja na timu yake na Naibu Katibu Mkuu wake. Pia napenda kuipongeza Wizara hasa ambavyo imeshusha huduma mpaka ngazi ya mikoa. Kwa mfano sisi watu wa Mafinga zamani ilikuwa lazima twende kwenye Ofisi ya Kanda kule Mbeya lakini sasa ofisi iko palepale Iringa, napongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetokea nimepata huduma kwa baadhi ya Makamishna akiwemo Kamishna wetu wa pale Iringa ndugu Mtui, Kamishna Msaidizi wa hapa Dodoma ndugu Kabonge na Kamishna wa Dar es Salaam ndugu Kayela. Ni watu ambao wanafanya kazi vizuri na ni wasikivu, naamini na Makamishna wengine wote wanafanya kazi vizuri chini ya Kamishna wao ndugu Mathew ambaye kwa kweli ni mtu ambaye kama una jambo la wananchi wako anakusikiliza vizuri. Hivi ndivyo ambavyo inatakiwa tufanye kazi katika kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi napenda kusema kwamba migogoro mingi ambayo watu wengi wameisema tunaweza tukaitatua tukiwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi na tukiiwezesha ipasavyo Tume yetu ya Matumizi Bora ya Ardhi lakini na hizo ofisi zetu ipasavyo, kwa sababu bila kupanga kupima na kumilikisha bado migogoro itaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Tanzania tuna square km 945,087 wakati nchi kama Vietnam wao wana square km 391,690 lakini hawana migogoro, maana yake ni kwamba ardhi tunayo bwerere lakini kitu kinachotushinda pengine ni kuipangia matumizi bora ambayo itatuwezesha kupunguza migogoro. Ndiyo maana sisi Halmashauri ya Mji wa Mafinga tumejielekeza pamoja na kupima viwanja lakini tumeona ya kwamba tujielekeze katika kuwa na maeneo kwa ajili ya uwekezaji, kwa ajili ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga sasa eneo karibu heka 700 kwa ajili ya Industrial Park, maana yake ni kwamba sasa tunakuja mbele ya Wizara kuomba mtuwezeshe tuweze kupima, kupanga na kumilikisha, tukishakuwa na hii industrial park maana yake ni kwamba Wawekezaji watakuja, vijana wetu watapata ajira, Halmashauri itapata mapato lakini na Serikali nayo itapata mapato katika ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kwa nini tumeamua hivyo, kwa sababu Mafinga na Mufindi ni Miji ambayo inakua kwa kasi, kuna viwanda vingi, lakini baadhi ya Wawekezaji wamejikuta wakati mwingine wanaingia katika mikono ya watu ambao sio waaminifu, pia wakati mwingine viwanda vinawekwa maeneo ambayo siyo vizuri kiusalama kwa sababu ni maeneo ya karibu na makazi ya watu, ni maeneo kwa sababu hayakupangwa kuwa ni maeneo ya viwanda kama Halmashauri tunashindwa kufikisha huduma muhimu kama za maji, barabara na hata wenzetu wa TANESCO inawawia vigumu kufikisha huduma ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Wizara ituangalie Mafinga kwa macho mawili, katika suala hili la Industrial Park na kwa kweli tumedhamiria, hapa ninapozungumza Mkuu wangu wa Wilaya Ndugu Saada Mtambule pamoja na timu ya Mkurugenzi wapo EPZA kuweza kujifunza, kwa sababu tunataka kuwa modal ambao tutakuwa na Industrial Park ambayo itakuwa suluhisho pia kwa ajira za vijana wetu. Kwa hiyo ninawaomba sana Wizara ituangalie kama itakuwa ni grant, ama utaratibu wowote ambao utaona inaweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga, kupima na kumilikisha kunasaidia mambo mengi, kwa mfano kunaipunguzia Serikali gharama wakati ambapo ingekuwa imepanga hatuwezi kuingia kwenye gharama za kujipa hizi fidia, pia mara nyingi inapunguza migogoro, tukipanga pia tunakuwa na maeneo kwa ajili ya huduma mbalimbali. Kwa mfano, hapa katika eneo letu la Bunge, utaona ya kwamba eneo hili kadri huduma zinavyohitajika unaona kabisa tunahitaji eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukijadili hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili lilijitokeza kwamba tuone umuhimu wa kuongeza au kupanua eneo hili la Viwanja vya Bunge, jambo hili kwa mujibu wa maelezo ilielezwa ya kwamba linapelekwa Wizara ya Ardhi ili wenzetu watusaidie kufanya uthamini ili kuona uwezekano kwa mujibu wa taratibu za Serikali kama wanaotuzunguka tunaweza tukawalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, maeneo haya ya Bunge humu ndani tuna Muhimili wa Bunge, tuna Mheshimiwa Spika ambae ni Kiongozi wa Muhimili, pia yupo Mheshimiwa Waziri Mkuu ambae ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali pamoja na Mawaziri wake, yupo Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Watumishi wa Serikali, kwa mfano leo hii wako Makamishna, wako watu wa Wizara ya Ardhi. Vilevile wakati Mheshimiwa Rais akija hapa kuhutubia Bunge au wakati wa Bajeti Kuu, Viongozi wengi wa Taifa letu huwa wanakuwepo hapa katika Viwanja vya Bunge kwa maana ya kwamba Serikali huwa iko hapa. Wanakuwepo viongozi wastaafu, wanakuwepo viongozi wa vyombo vya dola, wanakuwepo Viongozi Wakuu wa Chama cha Mapinduzi sasa mimi nalitazama hili katika jicho la kiusalama zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa jinsi ilivyo ndiyo maana nashauri kwamba mchakato huu wa kuongeza eneo la Bunge uende kwa haraka kwa sababu gani, tufikirie Serikali yote iko hapa, kama mtu ana nia ya kufanya jambo baya just ukitoka tu hapa mlango wa geti la Waziri Mkuu tayari unakuta pale ni maeneo ambayo ni maghala, kwa mfano mbele pale kuna maeneo ambayo ni bohari ya mafuta ambayo hata kiusalama kama limetokea jambo, is high risk na katika usalama wanasema, katika security huwezi ku-compromise mambo ya gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ninaomba wenzetu wa Wizara ya Ardhi pale ambapo wana wajibu wa kutusaidia kufanya tathimini na kufanya uthaminishaji basi wakamilishe hilo zoezi ili kusudi Bunge yale maeneo ambayo yanayotuzunguka yaweze kuchukuliwa kwa mukhtadha wa hilo jicho ambalo nasema ni jicho la kiusalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jicho la kihuduma wananchi wetu wanakuja hapa kutaka kupata huduma mara nyingi the most you can do wakipata kibali wataingia watakusubiri kule kantini. Nakumbuka wakati wa mgogoro wetu wa nguzo na Serikali walipokuja watu wa nguzo ilibidi tukae pale kantini, lakini tukamuomba OS wa Bunge akatusaidia tupate ofisi tujadili lile jambo na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na baadaye likapata suhuhisho. Kwa hiyo, hata kihuduma vinginevyo utakuta tunakutana na wananchi wetu kule nje kwenye magari ili tusikilize hoja zao, kama wanataka kumwona Waziri kwa hiyo pia kihuduma na kiusalama ninashauri sana kile kipengele au ile section ambayo wenzetu wa Wizara ya Ardhi wanalifanyia kazi walifanyie kazi kwa haraka na tuende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kutoka mwisho ni suala la Baraza la Ardhi. Wananchi wa Mufindi wanalazimika kusafiri kwenda Iringa wanapokuwa na shughuli zao za masuluhisho ya masuala ya ardhi, nimwombe Mheshimiwa Waziri na Serikali, imefika wakati sasa tuwe na Baraza la Ardhi pale Mafinga ambalo litahudumia Wilaya ya Mufindi, kwa sababu mtu kutoka Mgololo, Kitasengwa, Bumilahinga, Itimbo kwenda Iringa ni mbali, kwa hiyo ninaomba wizara ione na sisi kama Wilaya tuko tayari kutoa jengo kwa ajili ya huduma hiyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kwa dakika moja ninaomba Serikali ingalie watu wanapouziana ardhi, zile gharama tunazolipa ili kufanya transfer kwa kweli watu wengi wananunua ardhi, kama mimi nikiuziana na Mheshimiwa Bonnah hapa, kwa sababu tunaaminiana naogopa kuhamisha ule umiliki kwa sababu ya zile gharama, hebu tuziangalie ili watu wafanye transfer na baadae weweze kulipa kodi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nasisitiza tena kama nilivyosema asubuhi Mungu abariki viongozi wetu, Mungu abariki Taifa letu Mungu abariki Mafinga pia. (Makofi)