Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenya hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Sina hakika kuhusiana na mambo niliyoandika yalivyo mengi kwa hiyo nitaenda moja kwa moja kwenye hoja yangu, kama muda utaniruhusu nitaleta pongezi zangu mwishoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza kwa nukuu kutoka kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anasema: ‘‘Ili nchi iendelee na ipate maendeleo inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.” Kwa kichwa kizuri kama cha Mwalimu Nyerere ambacho tunakubaliana kwamba hata ambao hawakubaliani na siasa zake huko duniani wanakubaliana na ubora wa kichwa chake, kuiweka ardhi miongoni mwa vitu vinne muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa siyo kitu kidogo hiki wote tunakubaliana nacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo mimi ninachoona ni kwamba kwanza suala la ardhi kuwa miongoni mwa vitu vinne muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa, ni zawadi na laana. Ni zawadi kwa sababu ardhi tunayo kubwa na kama itatumika ipasavyo kwa sheria tulizojiwekea na wasimamizi wake wakafanya vile ambavyo tumewatuma kufanya, itatuelea maendeleo bila wasiwasi wowote, lakini ni laana kama yatafanyika kinyume chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa ardhi unafanya uwezekano wa kuepuka kabisa migogoro ya ardhi kutokuwepo, migogoro ya ardhi ni kitu ambacho tunatakiwa kuishi nacho, tuifanyie kazi tuisuluhishe kila wakati kuhakikisha kwamba wananchi wanyonge wanapata haki zao kama wananchi ambao wana nguvu kuliko wengine. Kwa hiyo, ni ongoing nisichokubaliana nacho ni jinsi ambavyo tunatengeneza migogoro na mingine ambayo pengine tungeweza kuitatua wakati ni midogo tunaiacha inakuwa milima mikubwa ambayo inakuwa migumu kuitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mbunge hata mmoja kwenye Bunge hili tufuku wa Jimbo ambae hana mgogoro kimeo wa ardhi kwenye Jimbo lake, hiyo inakuonyesha jinsi ambavyo kuna matatizo makubwa ya ardhi kwenye nchi hii. Sasa pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri alisema kwamba mikutano 1,800 kwa ajili ya usuluhushi wa migogoro ya ardhi ilifanyika mwaka uliopita, lakini bado nimuombe Mheshimiwa Waziri afanye mikutano zaidi aendelee kwa nguvu nyingi asichoke mama yangu na ndugu yangu Ridhiwani pia muendelee kwenda site kuhakikisha migogoro ya ardhi inaendelea kutatuliwa siku hadi siku, siamani kwamba kuna siku tutafika hatuna hata mgogoro mmoja wa ardhi kwenye nchi hii lakini angalau tuibadilishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro iliyokuwapo juzi na siku kabla ya juzi isiwepo leo na kesho. Katika Jimboni la Muheza tuna matatizo makubwa ya ardhi, mathalani naweza kuorodhesha migogoro karibu 15 hapa, lakini kwa sababu ya muda nina miwili ambayo ya mfano, kwanza kwenye Tarafa ya Amani, tuna mwekezaji East Usambara Tea Company ambaye anamiliki hekari 35,000 za ardhi, kati ya hekari 35 kulikuwa na viwanda vitano vyakuchakata chai ni viwanda viwili tu vinafanya kazi sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vitatu vilivyobaki vimebaki kuwa magofu ambayo yanafungwa yamekuwa majumba ya kifahari pamba na nyoka kule Amani. Kati ya hekari 35,000 ambazo Mwekezaji huyu anazimiliki ni hekari 5,000 tu ambazo zinatumika kulimia chai. Sasa kule Amani kila kitu kinaota, tunayo mashamba mpaka ya mpira huu unaotengeneza matairi, tuna mashamba ya iriki, mdalasini karafuu na kadhalika. Wananchi wa Kata zote Sita za Tarafa ya Amani wanamiliki robo heka, robo heka kwa sababu Mwekezaji ameshikilia ardhi ambayo haifanyii kitu kwa zaidi miaka 25 sasa! Unashirikia hekari 30,000 ambazo huzifanyii kitu katika ardhi ambayo Kata zote Sita hakuna hata hatua moja kwa ajili ya kujenga shule. Kwa mfano, Kijiji cha Magoda Kata ya Kisiwani wanataka hata eneo la kujenga Ofisi ya Kijiji hakuna ardhi ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanataka eneo la kujenga Shule ya Msingi na Zahanati hakuna eneo la kufanya hivyo na kuna mtu ameishikilia hekari 30,000, my good guess ni kwamba amelichukua eneo ameenda kulitumia kama collateral kwa ajili ya kupata financing kufanya biashara zake nyingine wakati wananchi wa Tarafa ya Amani wanapata shida! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Misalai katika Kijiji cha Misalai hakuna hata hatua moja kwa ajili ya kufanya shughuli za makazi. Shamba Ngeda wanataka eneo kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo lakini hawawezi, hakuna hata hatua moja. Mbomole wanataka kufanya ujenzi wa shule ya sekondari hakuna ardhi, wanataka kujenga zahanati na shughuli za kilimo lakini hakuna ardhi hata hatua moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilisema mwanzoni, ardhi hii inasitawi kila kitu. Sasa mwekezaji anapoiwekea ardhi eka 30,000 ambayo haifanyii chochote huku ni kuwaonea wananchi wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye, naomba niitafute ili nisikosee, ukisoma kweney misingi mikuu ya ardhi kitaifa, ukiacha wa kwanza ambao unasema ardhi yote ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini na msimamizi mkuu kwa niaba ya Watanzania wote, wa nne unasema kudhibiti kiasi ambacho mtu mmoja au taasisi yaweza kumiliki na kutumia kwa mahitaji yake bila kuwaathiri Watanzania na wanajamii wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapofika mahali wananjamii wengine hawana sehemu hata ya kujenga ofisi ya kijiji ama darasa moja la shule ilhali kuna mtu ana ekari 30,000 ameziweka tu amekwenda kuzichukulia mkopo sehemu huku ni kuwaonea wananchi wanyonge na Kwenda kinyume na misingi ya umiliki wa ardhi ambayo tumejiwekea kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taifa ambalo serikali yake inasimama kwa niaba ya wanajamii wote, na inasimama kwa niaba ya watu, linapotokea suala la ukinzani kati ya watu na maendeleo basi Serikali inachagua upande wa watu. Sasa hili limekwenda mbali zaidi, hili ni watu na wanataka maendeleo halafu upande mwingine kuna mtu mmoja anayehakikisha watu hawa hawapati maendeleo.

Mimi niwaomba wawakilishi wa Mheshimiwa Rais kwenye upande huu wa ardhi, Mheshimiw Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu mfanya mnavyofanya, twendeni site mkawasikilize wananchi, mkawasikilize wasaidizi wenu kwenye halmashauri, na ikiwezekana na Kamishna wa Ardhi wa Mkoa ili kuona namna ambavyo tunaweza kuwasaidia wananchi wale wanyonge.

MheshimiwaMwenyekiti, wito wangu ni kumshauri Mheshimiwa Rais, kwamba mashamba haya ambayo hayatumiki yafutiwe hati na wananchi wagawiwe ili waweze kufanya shughuli zao za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano wa pili katika ya 15 ambayo ningependa kuitoa lakini nikasema nitasema miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili ni kuhusiana na jinsi ambavyo watu ambao tumewapa mamlaka ya kutafsiri sheria za ardhi kwa ajili ya jamii nzima wanavyotukosea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 laliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, Mungu amrehemu, alipita Mkoani Tanga. Miongoni mwa vitu alivyovifanya ni kufuta hati sita za yaliyokuwa mashamba ya mkonge kwa sababu yalikuwa hayatumiki. Kwenye mkutano wa hadhara pale Mkanyageni aliamrisha kwamba shamba lililokuwa la Geiglits ambalo lilikuwa katika Kijiji cha Muungano ligawiwe kwa wananchi wa maeneo yale; kwamba kila mwananchi apate eka tatu, na mwenye uwezo wa kuendeleza apate ekari tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 mpaka sasa hivi ni mwaka 2022, nikuambie kwamba zoezi hili halijafanyika hata kwa asilimia 20. Sasa unapata walakini, maelekezo yalikuwa wazi, kwamba kuna eneo kuna wananchi, idadi ya kaya inafahamika kwa sababu Mheshimiwa Rais hawezi kufuta, na akaamrisha kwamba kila kaya ipate eka tatu. Vivyo hivyo mchakato ule haujaweza kutimia hadi leo. Sasa una watu, una ardhi, kila kimoja unajua ukubwa wake lakini zoezi hili linashindikana kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili pia nimuombe Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri na wasaidizi wao twende tukawasikilize wananchi. Moja, tupate vielelezo kutoka kwa wananchi, maafisa wa ardhi kule chini na tuone kitu ambacho tunaweza kukifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule chini kuna kamati ya wazee tisa kwenye Kijiji cha Muungano pale Kilapula, mzee mmoja anaitwa Dkt. Mhada amenitumia email 22, yaani imepita juzi tu, na Mheshimiwa Mnzava ni shahidi wangu, sija-exaggerate kituo chochote. Email 22 zenye vielelezo za kwa nini anahisi wananchi wanyonge wanaonewa na wanataka kudhulumiwa ardhi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi kwamba iamuliwe tu kwamba wakagawiwe, lakini twende tukawasikilize na tuone vielelezo ambavyo wanavyo na tuamua kwa conscience zetu zikiwa clear kabisa, tukiwa tumejitosheleza na vile vielelekezo ambavyo wanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi iko mingi sana Wilayani Muheza, na ninaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri wanipe angalau siku tatu za kuambatana nao kule kuhakikisha kwamba tunakwenda kuitatua yote. Sina mpango wa kushika shilingi, kusema kweli kama mtaniahidi hilo wakati mnakuja kufanya majuisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niwapongeze na Mheshimiwa Rais, na ninaamini mtafanya kazi nzuri. Niwahakikishie, sisi tuko pamoja nanyi. Wananchi wa Wilaya ya Muheza wana Imani kubwa na Serikali yao ya Awamu ya Sita, chini ya Mama, Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Niwahakikishie kwamba kama tutawaondolea kero hizi ndogondogo basi mtashangaa na matokeo ya kuungwa mkono ambayo mtayapata kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, ninaomba kuwasilisha.