Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Francis Leonard Mtega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Niwashukuru sana viongozi wakuu wa kitaifa, nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri, watendaji wote wa Wizara kwa kuwa na sera nzuri ya upimaji ardhi, urasimishaji na utoaji wa hati za ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nioneshe masikitiko yangu makubwa kuhusu migogoro ya ardhi; na kwa kweli mgogoro sugu wa ardhi uliopo Wilayani Mbarali ni GN namba 28. Ninamshukuru Mheshimiwa Bahati Ndingo ametoka kusema muda si mrefu; vijiji ambavyo vilihamishwa rasmi taratibu zote zilifuatwa na malipo yalifanyika. Isitoshe walilipwa mara mbili walipofanya uthamini mara ya pili, kwa hiyo tunashukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipeleka miundombinu sehemu ambazo wana Mbarali wanatakiwa sasa waishi kwa amani na bila bughudha yoyote. Cha kushangaza na kusikitisha, wataalam wamekwenda kinyemela kuongeza mipaka bila ushirikishwaji wowote kwa wananchi. Kwa kweli kitendo hiki kimetuumiza sana, na mpaka sasa hivi ni mateso yanaendelea kwa wananchi wa Mbarali, achilia mbali vitendo vya kutisha, kama vile mauaji; mara tuokote nywele, mara kichwa, mara mifupa na viongozi wetu kupigwa sana na kuumizwa sana.

Mheshimiwa lakini pia ziko athari za kimaendeleo. Kwa mfano Mheshimiwa Rais ametoa fedha za kujengea Shule ya Sekondari Luhanga, shilingi milioni 600, lakini pia akatoa fedha kwa ajili ya vituo shikizi zaidi ya vine. Cha kushangaza ni kwamba wateule wake wamezihamisha zile fedha bila taarifa yoyote kwa wananchi. Wananchi wameshikwa na taharuki kubwa, wanashangaa; Mheshimiwa Rais anavyopenda wananchi wake, ameleta fedha halafu tena zimehamishwa, kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na majibu rahisi huwa wanasema kuwa haya ni maamuzi ya Mheshimiwa Rais. Sasa, matumizi mabaya ya jina la Mheshimiwa Rais kwa kweli hii inasikitisha sana na haikubaliki. Nimetembelea Luhanga, nimefanya kikao pale, nimeshuhudia mwenye wananchi kwa nguvu zao wamejitoa, wamechangishana; na ugumu walio nao lakini wameweza kujenga majengo ya shule ya sekondari, na wamekamilisha vyumba vitatu na ofisi moja; na matundu ya vyoo ilikuwa bado kidogo kukamilisha, mimi nikajitolea mifuko ya saruji ili wakamilishe kwa dhumuni la kunusuru watoto wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu iliyopita watoto 60 hawaku-report shuleni katika kata ambayo iko jirani. Kwa kweli ni umbali mrefu, zaidi ya kilometa 60 kwenda na kurudi; sasa, watoto wanashindwa kuhudhuria. mwaka huu kati ya watoto 2019 waliochaguliwa kwenda kidato cha kwanza ni Watoto 49 tu wame-report, wengine wote wamepotelea mitaani na wanachunga ng’ombe. Kwa kweli wanakosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, cha kushangaza ni kwamba, eneo lile wao wanasema ni hifadhi, mimi wiki iliyopita nilimfuata Mheshimiwa Waziri, kwamba hebu tuangalie kwenye kitabu, eneo lile sikuliona. Wakati huo huo ninafanya kikao pale kuna kijana alisimama, anauliza, anasema, hapa ardhi imeuzwa kwa matajiri, sisi vijana hatujapewa hata ekari moja. Mimi nimewasimamisha wenyeviti wa vijiji pale wajibu hoja, kwamba kwa nini mmeuza ardhi na imekuwaje vijana hawajapewa hata ekari moja. Viongozi wale walianza kuvutana vutana pale; haieleweki nani ameuza. Mheshimiwa Diwani akasema Mheshimiwa Mbunge tunaomba utuachie, hili tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, cha kushangaza, iwapo eneo lile ni hifadhi, imekuwaje matajiri waende wakanunue na kisha watengeneze mashamba? Wao hawaogopi kuhamkishwa?

Mheshimiwa Mwenyikiti, lakini madhara mengine ni kwenye anuani za makazi. Sote tunaelewa, sensa ya tarehe 23 Agosti itajumuisha pamoja na anuani za makazi. Sasa pale Mbarali kuna kata tatu ambazo sehemu kubwa ya vijiji havijawekwa kwenye mpango wa anuani za makazi mpaka sasa hivi ninavyoongea. Hata hivyo, cha ajabu ni kwamba, viongozi wangu walipolalamika kwamba mbona vijiji vingi havijaingizwa kwenye anuani za makazi mimi niliwajulisha kwamba hebu kaeni kwenye kamati ya siasa mje na muhtasari huku Dodoma mtakapokuja kwenye Mkutano Mkuu wa Chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikaa kwenye kamati ya siasa, majibu yakawa ndiyo hayo, kwamba ni maamuzi ya Mheshimiwa Rais. Viongozi wale wa chama wakasema kama ndivyo hivi sisi kesho tunakwenda Dodoma na muhtasari huu tukaoneshe. Cha kushangaza, asubuhi ile tunapigiwa simu kuwa baadhi ya vijiji wametumwa wataalam Kwenda kuandikisha anuani za makazi. Sasa tunashangaa, kwamba Mheshimiwa Rais anaamua kwa namna hiyo, kama si kumchafua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kwamba wanancho walikabidhiwa yale maeneo ili waendelee kufanya kazi zao kama kawaida. Wapo waliojenga nyumba nzuri za maana, wako wanaobabaika mpaka sasa wanashindwa kujenga nyumba ilhali wana haki kabisa. Ingalikuwa wao wamehamishwa au wamelipwa fidia sasa hapo ni kweli wasingeweza kupewa anuani za kamakazi. Taratibu hazijafuatwa, sasa kwa nini wasipewe anuani za makazi? Na kama Serikali itaamua kulichukua eneo hilo basi taratibu zifuatwe. Kwamba wajulishwe, washirikishwe, walipe fidia halafu waondoke, kuliko kubaki wanateseka, kwamba hawana uhakika na maisha yao, kwamba tutabaki au tutaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kinachosikitisha zaidi ni usiri mkubwa katika jambo hili. Tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwadilifu, mzalendo mkubwa kabisa, amekwenda pale Ngorongoro, amekaa na wananchi wale wafugaji, amewaelekeza hali halisi, baadhi yao wamekubali na wanaondoka vizuri tu kwa hiari yao. Kwa nini Mbarali kuna siri? Kuna nini nyuma ya pazia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile tume ya mawaziri nane walikwenda Mbeya; viongozi wa chama walipigiwa simu kwamba kesho wanakuja mawaziri, nami wakanijulisha. Jioni yake wakapigiwa simu kuwa ile ziara imeahirishwa, msije, lakini kumbe wanakuja. Sasa, kwa nini watufiche? Wawakilishi wa wananchi tunatakiwa tuwepo, tusikilize ili tutoke na majibu sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vyombo vya habari ziliandika habari za kutisha wananchi, kwamba sasa vijiji 31 vinakwenda kwenye hifadhi, wananchi wakashangaa. Mimi nimekuja kufuatilia kwa Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Mheshimiwa Waziri alikanusha habari za ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi ya shamba humaliziwa shamba, tunaoumia ni wana-Mbarali. Wanapokwenda Mkoani Mbeya, Mbeya wenyewe wanashangaa kama ambavyo huku wanavyoshangaa. Lakini maumivu tunaopata ni sisi wana-Mbarali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.