Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Ardhi. Nianze tu kwanza kwa kuungana na wenzangu ambao tangu asubuhi wameshiriki kwa pamoja kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa tuzo na zawadi ambazo wenzetu wameweza kumuona na kumtunuku. Kubwa mimi niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo kwenye kila sekta ameweza kuweka mkono wake ili kusaidia, lakini lengo likiwa ni moja tu, kuwasaidia wananchi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Wizara hii tu peke yake Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya bilioni 50 kwa ajili ya kuhakikisha angalau ardhi ya nchi hii inapangwa, kupimwa pamoja na kumilikishwa. Haijawahi kutokea kwenye ziada ya bajeti kutoa fedha nyingi kiasi hicho ka bajeti ya mwaka jana ambayo angalau imetumika kuanza kupanga, kupima na kumilikisha kwenye baadhi ya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana fedha ikawa ni ndogo na tukawa hatuoni impact yake, lakini haya yote hatuwezi kuyaona ni kwa sababu ya ukubwa wa eneo la ardhi hii ambalo halijawahi kupangwa, kupimwa na kumilikishwa. Tunazungumza zaidi ya asilimia 75 ya nchi hii haijawahi kupangwa, kupimwa na kumilikishwa. Asilimia 25 pekee ndiyo iliyopangwa, kupimwa na kumilikishwa. Na zaidi ya asilimia 60 ya nchi hii haijapangwa. Kwa hiyo unaweza ukaona kwamba yawezekana fedha imetoka, Wizara ikaichukua ikafanya kazi lakini impact yake isionekane kwa haraka kwa sababu ya maeneo mengi bado hayajafanyiwa kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi leo nitajikita sana kwenye kutoa ushauri. Ninajua mchango mkubwa na kazi kubwa wanayoifanya Mawaziri hawa. Kwa sababu kama wenzangu walivyochangia, migogoro ya ardhi ni mtambuka. Hapa leo tukipanga na kupima maeneo yote nchi hii bado tukubaliane kwamba kuna baadhi ya maeneo kutakuwa na migogoro ya ardhi, haiwezi kwisha yote kwa pamoja. Tunachojitahidi sisi ni kuhakikisha ile migogoro ambayo tunaishauri Serikali, ni kuhakikisha angalau inapungua kwa kadiri inavyowezekana ili angalau kutoa haya ambayo yangekuwa yakichangiwa humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitajikita kwenye sera katika ushauri wangu. La kwanza ninaloliona hapa ambalo linaleta shida kubwa humu ni Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995. Mimi nichukue nafasi hii kumuomba sana Mheshimiwa Waziri, haya yanayozungumzwa, kitu pekee ambacho kinaweza kikamuokoa ni kuharakisha ile Sera ya Taifa ya Ardhi ambayo imeshapitwa na wakati. Sera ya Taifa ya Ardhi ndiyo ilizaa mabaraza ya ardhi. Mabaraza ya ardhi ngazi za vijiji, kata na wilaya yote haya kuna confusion ya sheria namna ya uratibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukiwa kuna mgogoro kwenye kijiji umetatuliwa na baraza la ardhi la kijiji na haujakwenda sawa sawa atalaumiwa Waziri husika; pamoja na kwamba na yale mabaraza hayawajibiki kwa Mheshimiwa Waziri moja kwa moja ilhali yametajwa kwenye sheria kwamba yanawajibika chini ya mkurugenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niombe, sera ambayo itatupelekea mabadiliko ya sheria itaondoa hii changamoto iliyopo. Mimi niombe sana kwenye hili, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI mkimbizane na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ili tuone namna tunavyoweza kufanya review kwenye sera ili hatimaye tupate sheria nzuri. Haya mabaraza ya ardhi yote yasiwe na confusion. Baraza la ardhi la wilaya wanawajibika kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji yanawajibika kwa Waziri wa TAMISEMI. Hii confusion haiwezi kuwa sawa sawa. Kwa hiyo unakuta tayari huku wameharibu, ikija kufika kwenye baraza la ardhi ngazi ya wilaya, hata kama Waziri ataonekana ametatua bado inarudi kwenye Wizara ile ile ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe, ili kuondoa hii confusion, kwa sababu imetajwa kwenye sheria, ni lazima tukimbizane kutengeneza sera uya ardhi na kupata sheria ambayo ita-regulate na itasimamiwa kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tukubaliane; sehemu mbili ambazo zinaweza zikashughulika na changamoto ya migogoro ya ardhi ni mabaraza ya ardhi pamoja na Tume ya Taifa ya Mipango. Tume ya Taifa ya Mipango, tutakubaliana hapa; kwa mwaka wa jana na mwaka huu peke yake imetengewa bilioni 1.5. kuandaa mpango wa matumizi bora ya kijiji kimoja yanagharimu zaidi ya milioni 11 mpaka milioni 15, kijiji kimoja. Leo mnawapa 1.5, maana yake nini; atakwenda kuandaa mpango wa matumizi bora ukigawanya pale ni vijiji 100 tu peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo hautakidhi na mpango huu ambao tunazungumza hapa, ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha umeuwasilisha. Wakati huo huo unakuwa kinyume na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi hapa inasema, angalau kwa mwaka vijiji vinavyotakiwa kupangiwa matumizi yake visipungue 750. Maana yake ni kwamba, kwa miaka mitano, wame-project mpaka mwaka 2025 tuwe tuna vijiji elfu tatu, mia sab ana kidogo. Lakini sasa hawa watu mnawapa bilioni 1.5, kwa mwaka anapanga vijiji 100 peke yake. Maana yake ni kwamba anakwenda kinyume na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Mpango wa Tatu wa Mandeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tutafute namna ya kuinusuru hii Wizara. Ile Tume ya Taifa ya Mpango haya yote yanayozungumzwa inatakiwa iende site, ishughulike na kutatua migogoro iliyopo kati ya wafugaji na wakulima na migogoro ya mipaka iliyopo. Sasa haiwezi ikatatua kama haina fedha ya kufika kwenye maeneo husika. Hii ndiyo instrument ambayo inatakiwa iende ikashughulike na migogoro hiyo, haina fedha, wanakwendaje? Wanatatuaje migogoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe, solution ya kwanza kabisa ni kuongezewa fedha. Tuwape fedha angalau waendane na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inavyosema pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa. Vinginevyo tutafanya 25 hawatakuwa na fedha ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, fedha ipo. Mheshimiwa Mdee alizungumza asubuhi hapa vizuri sana, fedha ipo na sehemu ambayo ipo, ukisikiliza Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa nane, anasema, hakufikia malengo ya makusanyo ya kodi ya ardhi kwa sababu kuna Mashirika ya Umma hayalipi kodi. Wanadaiwa zaidi ya asilimia 70; na wanazalisha zaidi ya Shilingi bilioni 78 Mashirika ya Umma zaidi ya 114. Maana yake ni nini? Yale Mashirikia yakibanwa yakalipa ile Shilingi bilioni 78, tutapata Shilingi bilioni 10 iliyokuwa inaombwa na Tume ya Taifa ya Mipango kwenda kutekeleza jukumu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu haya ni Mashirika ya Umma, ni Mashirika ya Serikali, yanaingia kwenye Bajeti kila mwaka, yatenga fedha kwa ajili ya kulipa kodi ya ardhi na hayalipi, leo hii jioni naomba, kesho tutakapokuwa tunahitimisha, Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri Mkuu angekuwepo tungemwomba, watoe maelekezo na matamko ya haya Mashiriki ili yaweze kubanwa kulipa hii fedha. Kwa sababu vingenevyo, Wizara ya Ardhi kila mwaka inapanga bajeti na ikipanga bajeti inaonesha kwamba Mashirika yaliyopo yanatakiwa kulipa kiasi gani cha kodi ya ardhi, halafu unafika mwishoni, hayalipi ile fedha, unakwenda mwaka mwingine. Hawa watu mtawakamua kadri mnavyoweza lakini hawatafika lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni Mashirika ya Umma, kwa nini mwananchi mnyonge tunamwambia lipa kodi ya ardhi? Shirika la Umma ambalo linatengwa kwenye bajeti, linapewa fedha ya Serikali, hawalipi. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kigezo kimojawapo cha Mkurugenzi yeyote wa Shirika la Umma ambaye halipi kodi ya ardhi ili angalau ile fedha iende kushughulikia kutatua migogoro ya wananchi, iende ikatumike kwa shughuli nyingine; na iwe ni kipimo kimojawapo cha kumtathmini kama kweli anaweza kufanya kazi ile. Kwa sababu haina maana kama mashirika mengine yanalipa fedha, halafu wengine hawalipi. Mashirika 114 nchi hii hawalipi, na tunakwenda kumaliza mwezi wa Sita hawatalipa. Wanabeba madeni, yanakwenda mwaka ujao, hawatalipa. Lini Wizara hii itafikia lengo? Lini itapata fedha ili iende kuweza kupanga na kupima maeneo ambayo hayajapimwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba ili tuweze kumnusuru Mheshimiwa Waziri na hii Wizara ya Ardhi, tuhakikishe angalau wale ambao wanatakiwa kulipa kodi kwa wakati, walipe kwa wakati na kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, sambamba na hili kwa Mheshimiwa Waziri, nilisema leo sitakuwa na la kulalamikia, nilitaka tu nishauri kwa namna ambavyo imekaa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, tuliwahi kuzungumza toka mwaka 2021 kuhusiana na Housing Policy, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Mchechu kurudi kwenye Shirika la Nyumba la Taifa. Najua kwa namna anavyofanya kazi vizuri, ataanza kazi muda wowote wa ujenzi wa hizi nyumba. Shida yangu ni kwamba, anapooanza shughuli zile za ujenzi, kelele huwa zinakuwa nyingi kwamba bei za nyumba zinakuwa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema sana, bei ya nyumba inaweza kuwa regulated na Housing Policy, lakini inaweza kuwa regulated kama tutaipitia tukaainisha maeneo yote namna ya ku-regulate. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watu wake wote ndani ya Wizara; Mheshimiwa Naibu mimi naamini kwamba wewe ni kijana umeingia na unafanya kazi vizuri, tuchangamkie hii ili yule atakapoanza Shirika la Nyumba kukimbizana na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, mwananchi aweze kupata nyumba kwa gharama nafuu kadri inavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba maeneo ya mpakani, ya maziwani na baharini tuone namna ya kuweka maboya, tuone namna ku-identify, kutenganisha mipaka kati ya Tanzania na zile nchi mbili ili angalau tuondokane na yale ambayo yanayotokea kule. Wananchi kule wanavamiwa, wanapigwa na maeneo mengine wanaumizwa. Naomba sana, mipaka ile, yale maboya yakiwekwa yatasaidia sana maeneo ya maziwa na baharini ili angalau mvuvi wa Uganda anapokuja akiona yale, ajue nikienda naenda Tanzania, huku ninapokwenda naenda kuchukua cha watu. Watanzania nao vivyo hivyo. Naomba sana, pamoja na maeneo mengine, mwone namna ya kulifanya hili kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)