Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Dunia kwa kutujaalia uhai na leo hii tuko hapa Bungeni, tunachangia Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Angeline Mabula na Mheshimiwa Ridhiwan Kikwete, mwanangu kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pia nawapongeza watendaji wote wa Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri ambazo wanaendelea kufanya kuiweka Wizara hii vizuri na kufanya Watanzania waweze kufurahia ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu pamoja na hizo pongezi kuna mambo ambayo ningependa kuyazungumza kwenye Wizara hii. Kwanza kabisa napenda kuzungumza kuhusu Tume ya Taifa ya Mipango ya Ardhi kama walivyoweza kuzungumza watangulizi wengine. Kazi za Tume hii ni kuipima ardhi ya Tanzania, lakini Tume hii haina meno ya kupima ardhi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ardhi ya Tanzania ikipimwa itajulikana maeneo ya wafugaji yako wapi, maeneo ya wakulima yako wapi na itajulikana maeneo ya mambo ya jamii yako wapi; kama shule na Hospitali. Hii itapunguza sana mwingiliano na vurugu zilizopo kati ya wakulima na wafugaji. Kazi hii inashindwa kutekelezeka kwa sababu Tume ya Mpango wa Ardhi inapewa fedha ndogo. Haieleweki akilini, Tume ambayo inapima ardhi ya Tanzania inapewa Shilingi bilioni 1.4 na hata mwaka 2021 ilipewa Shilingi bilioni 1.9. Naiomba Serikali, kama kweli inataka kuondoa matatizo ya wafugaji na wakulima nchini Tanzania, iipe Tume hii fedha za kutosha. Migogoro mingi iliyopo ni kwa sababu ardhi ya Tanzania haioneshi mipaka ya mfugaji iko wapi, mipaka ya mkulima iko wapi; na mipaka ya mashamba ya mwananchi wa kawaida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Tume pia ina Bodi ambayo siyo ya Utendaji. Tume hii ina Bodi ya Ushauri. Ili Bodi hii iweze kufanya kazi, inatakiwa iwe Executive Board, lakini hii ni Advisory Board. Naomba Serikali ibadilishe sheria ili Tume hii iweze kuwa na Bodi ambayo itakuwa ni Bodi ya Wakurugenzi, ambayo itakuwa na meno na pia itaweza kutoa ushauri mzuri kwenye Tume na Tume iweze kufanya kazi zake vizuri. Pia Tume hii itakapokuwa imepata mambo hayo, itaweza kuwa na bajeti yake. Sasa hivi Tume hii haiwezi kupanga mambo yake ya Bajeti kwa sababu haina Bodi yenye meno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusisitiza, kama jinsi wachangiaji wengine walivyosema, Tanzania tuna Vijiji 12,319 lakini Tume hii tangu imeanzishwa imeweza kupima vijiji 2,565. Ukienda kwenye Ilani ya CCM kama wengine walivyosema, inasema mpaka kufikia 2025 angalau vijiji 80,000 nchini Tanzania viwe vimepimwa, lakini kwenye mpango wa matumizi wa 2020 mpaka 2025 wenyewe umesema angalau asilimia 50 ya vijiji viwe vimewekewa mpango wa matumizi. Kutokana na hilo, naiomba Serikali iangalie ni jinsi itaweza kuipa nguvu hii Tume ya Taifa ya Mpango wa Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa kuzungumzia hapo hapo kwenye Tume suala la uhaba wa wafanyakazi. Tume hii ina wafanyakazi 79 tu nchini Tanzania. Ina uhitaji wa wafanyakazi 179, kwa hiyo, kuna upungufu wa wafanyakazi 100 kwenye Tume hii. Ili Tume iweze kufanya kazi mikoani vizuri, inatakiwa iongezewe wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Rais; Kamati ya Mawaziri nane ambayo ilipita kuzungumzia migogoro ya ardhi. Kwanza kabisa, napenda kuishukuru Serikali pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kuunda hiyo Kamati ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini Tanzania. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini pamoja na hizo pongezi, nimpongeze tu kwa Tuzo aliyoipata ya kuwa Kiongozi bora duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Kamati ya Mawaziri nane kwa sababu Mawaziri walipita kukagua masuala ya ardhi na matokeo yake Serikali ilitoa vijiji 975. Katika vijiji 975, vijiji 925 Serikali iliwapa wananchi. Katika Mkoani kwangu Katavi vijiji 60 tulipewa. Sasa basi katika hivi vijiji 60 vya Mkoani kwangu Katavi, havijapewa GN namba. Pia kuna matatizo makubwa katika utekelezaji, kwamba kuna maeneo ambayo vile vijiji vimepewa lakini bado kuna mamlaka zinakwenda kuwafukuza wananchi na kuwachomea nyumba. Nitoe mfano Kijiji cha Kaseganyama Wilaya ya Tanganyika, eneo la visima viwili, wananchi wale wamechomewa nyumba, na mazao yao na kufukuzwa wakati walikuwa wameruhusiwa kukaa pale.

Mheshimiwa Spika, nimetoa mfano Kijiji cha Kaseganyama Wilaya ya Tanganyika, eneo la Visima Viwili, wananchi wale wamechomewa nyumba lakini pia wamechomewa mazao yao na kufukuzwa wakati walikuwa wameruhusiwa kukaa pale. Pia vipo Vijiji kwa mfano vya Kapalala, Sempanda, operation ya kuwafukuza inaendelea.

Mheshimiwa Spika, siyo Kapalala tu, zipo Kata za Ilunde na kule Inyonga bado kuna operation kama hizo za kuwafukuza zinaendelea. Vile vile Kata ya Kamsisi kule Inyonga nako pia wananchi wamechomewa nyumba pa wamefukuzwa kwenye maeneo ambayo tena kuweka hali kuwa mbaya, Serikali ya Kijiji cha Kamsisi iliwauzia wananchi yale maeneo na ikapata fedha ambazo iliweza kujenga zahanati, lakini leo hii watu wa TAWA wameingia pale wanawafukuza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe mamlaka hizi zisiwe zinaingiliana, kama Serikali iliweza kutoa vile vijiji 920 ili wananchi wavitumie, tunashukuru sana na Mkoa wangu wa Katavi ukapata vijiji 60. Sasa kwa nini kunakuwa na mwingiliano wa mamlaka, kwa nini mamlaka nyingine ije kuwafukuza wananchi wakati walikuwa wameruhusiwa; na Kamati ya Mawaziri Nane ilipita na kuwakagua na kupewa ile ardhi. Sasa naona kuna mwingiliano wa mamlaka katika utendaji, haiwezekani, Serikali hiyo iwape wananchi vile vijiji kwamba wakae halafu Serikali hiyohiyo irudi kesho yake mamlaka nyingine iwaondoe na kuwachomea nyumba. Ningeomba sana Serikali ilirekebishe hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo ningependa kulizungumzia ni maeneo ya malipo kwa wananchi ambao Serikali inachukua ardhi yao. Kule Mpanda Mkoani Katavi kuna maeneo ambayo yana mgogoro mkubwa wa ardhi, maeneo ya Kampuni, Ilembo, Misukumilo, Mpanda Hotel, wananchi wametoka katika ile ardhi lakini wengine hawajalipwa malipo yao mpaka leo. Ningeomba Serikali inapowahamisha wananchi kwa ajili ya kujenga mambo ya maendeleo ya nchi yetu kama shule au zahanati, basi iwe inaandaa malipo kwa wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu kumekuwa na mgogoro mkubwa katika maeneo hayo niliyoyataja ambayo yapo pale Mpanda Mjini. Wananchi waliachia ile ardhi na Serikali imeanza kujenga taasisi zake nyingi, imejenga kama Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ipo kwenye maeneo ambayo wananchi bado wanadai ile ardhi; lakini mahakama imejengwa kule, vituo vya polisi na ofisi za Walimu, lakini unashangaa ni kwa nini maeneo hayo bado yana mgogoro wananchi hawajalipwa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda w Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ilikuwa imelia dakika moja nyuma.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. (Makofi)