Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi na nitakuwa na mambo makubwa mawili. Niwapongeze kwanza kwa kazi nzuri pia ambayo wanafanya kwa sababu yapo mazuri mengi pia ambayo wanayafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kuchangia kuhusiana na mpango wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa makazi. Kama Mbunge mmoja alivyokwishasema hapa; ardhi ni nguzo moja wapo katika nguzo nne ambazo Mwalimu Nyerere alisema, tunahitaji ili tuendelee, kwa sababu kila kitu kinafanyika kwenye ardhi. Sasa basi, kwenye upande wa makazi na matumizi bora nimeona kwamba wanasema mpaka 2025 inatakiwa vijiji vyote viwe vimepima na wamejiwekea namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miji tunayotoka pia kuna maeneo ambayo ni peri urban, haya sijaona mpango wake wamewekaje, yaani kwenye miji hakuna vijiji lakini tuna mitaa, lakini ile mitaa inaitwa mitaa kwa sababu tu ipo kwenye municipals au kwenye majiji; lakini ukiangalia hali halisi ni kama vijiji. Sasa sijui hii inaingizwa kwenye mpango gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni cha muhimu sana kukizingatia kwa sababu inatuletea shida hata kupeleka huduma kama hatuweki huu mpango wa matumizi bora ya ardhi mapema; hata kupeleka huduma kwa wananchi inakuwa ni kazi. Wakati ule Mwalimu Nyerere alianzisha zile program za vijiji vya ujamaa, of course yeye alianzisha kwa sababu ya mambo yake ya ujamaa na siasa za ujamaa na kujitegemea, lakini zilikuwa zina msaada kwa sababu hata wanapopeleka huduma wanawakuta wananchi wapo sehemu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunataka kujenga barabara, unamkuta mtu alikuwa ni mwindaji, akaenda kuwinda mbali na wenzie, baadaye akajenga nyumba, akaanzisha familia iko mbali sana, sasa kule wanaendelea wanatengeneza familia wapo watu 200, wapo watu 150 kutoka kwa wenzao walipo ni kilometa zaidi ya 70 au 60; Serikali inalazimika kupeleka barabara mpaka kule, kuwapelekea shule lakini hawa watu wangekuwa sehemu moja kwenye kijiji ingelikuwa ni rahisi au kwenye mtaa, ingekuwa ni rahisi ku-concetrate kwamba tunawapelekea mahitaji ya muhimu pale ya huduma; lakini yale maeneo mengine wakatumia kwa ajili ya uwindaji au kwa ajili ya kilimo kama ambavyo wametumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wanaimarisha TEHAMA, naomba katika zoezi la kuimarisha TEHAMA waangalie pia kuwapa mafunzo watu wao wa chini hasa kwenye kada hizi za chini kwenye halmashauri. Nasema hivi kwa sababu wengi, leo ukienda kwenye halmashauri wanatoa risiti za kuwadai kodi za ardhi wananchi ambazo siyo halisi. Ukiwauliza wanasingizia mfumo, wakati mfumo ule anau-feed mtu, hakuna mfumo ambao unajiweka peke yake halafu una generate data peke yake, ni watu ndiyo wana feed zile information kwenye mfumo. Sasa inaonekana watu wanakuwa hawapewi mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine tunaomba kwenye mambo ya MKURABITA, sasa hivi kwenye miji yetu MIKURABITA haipo tena, zile program za MKURABITA za kupima yale makazi ambayo hayakuwa rasmi haziendelei, sasa ujenzi holela unaendelea. Hata hivyo, kipo kipengele waliotoa kwenye Kamati zetu za Mipangomiji, cha kupitisha vibali vya ujenzi, wakaacha inawezekana walikuwa na nia njema kwamba vitolewe kwa wakati, viende na kasi na wananchi kwa sababu zile Kamati zina muda maalum. Hapa nafikiri wanatakiwa warudie waangalie ili kwamba Kamati zile zipewe mandate tena ya kuwa zinatoa vile vibali; kwa sababu tayari katika miji yetu ujenzi holela unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ninalotaka kuongea linahusiana na kodi ya ardhi (land rent) hasa kwenye taasisi; Taasisi za Dini, Taasisi za Shule na Taasisi za Vyuo. Ukiangalia hasa kwenye shule binafsi na kwenye vyuo binafsi. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa lakini katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, alikuja hapa tarehe 22 Aprili, 2021, akatuambia kasome ile hotuba yake kitabu chake ukurasa wa 10, paragraph ya kwanza, ya pili mpaka ya tatu; alielezea ni namna gani ambavyo mazingira yetu ya uwekezaji wa biashara hayajaboreshwa; hasa kwenye Sera, Sheria na Kanuni zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, akaahidi katika paragraph ya kwanza kuonesha anaboresha sera, sheria na kanuni. Paragraph ya pili na kuelezea hatua zinatakiwa kuchukuliwa ili kuvutia uwekezaji na sekta binafsi kuwekeza; lakini paragraph ya tatu akasema, nchi yetu imekuwa ikilalamikiwa kwa kutokuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji. Kwanza kutokuwa na kodi zisizokuwa na utulivu, lakini pia kuwa na sera ambazo zinabadilika badilika, hiki ni kitu ambacho hakivutii wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna watu wamewekeza kwenye elimu, uwekezaji kwenye elimu ni investment ya muda mrefu, return yake on investment ni zaidi ya miaka 10. Leo land rent unapokwenda kumchaji mtu mwenye shule binafsi, kwenye eneo la eka tatu katikati ya mji kwa mwaka anatakiwa kulipa milioni tisa, milioni sita inatoka wapi? Sasa uwekezaji umeanza kuwa kwa sababu hizi shule binafsi ndani ya manispaa lazima awe na eka tatu ndani yake kuna choo, viwanja vya michezo, madarasa, maabara, library vyote hadi choo kinachajiwa land rent, leo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje wakati hawa watu binafsi ni wawekezaji, wametupunguzia msongamano kwenye shule zetu za public; lakini hawa watoto ni watoto wa Watanzania, Watanzania hawa wanaosomesha kwenye shule binafsi wana haki kabisa ya kuhudumiwa kielimu na Serikali hii, lakini wameamua kulipa kodi, wameendelea kusomesha watoto wao kwa gharama zingine, kwa nini tuwaongezee mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie katika hizi shule binafsi, Serikali inatumia zaidi ya gharama za asilimia 97 kumsomesha mtoto kwenye shule ya public, lakini haichangii chochote kwenye shule ya private. Leo hii shule ya private inalipia fire, yaani shule ikitaka kuungua lazima ilipe ili ije izimiwe moto. Leo hatuna hata grant ya temptation tunayopata, unalipa land rent wakati fulani Katibu wa Wizara ya Fedha aliona kwamba suala la kuchaji kodi kwenye shule wakati ni taasisi zinazotoa huduma akazuia tukatolewa kodi ya SDL; lakini kodi hii imerudishwa kwa mtindo wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, vile vitu alivyoongea mama Samia kuangalia sera na kanuni zetu; kanuni mojawapo inayowatesa wananchi wa Tanzania ni ile kumpa commissioner room na kumpa power zaidi ya Bunge, nasema zaidi ya Bunge kwa sababu gani haiwezekani kwenye hati mtu aandikiwe hati hii utalipa kwa mwaka Sh.1,000,000 labda ndiyo itakuwa land rent yako; Kamishna anakaa anabadilisha mtu alipe milioni sita au milioni tisa nani hapo mwenye mamlaka kuu? Hivi ndivyo vipengele ambavyo Rais alisema viondolewe kwenye kanuni, sera zetu na sheria kama zinawakandamiza Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo tukafikiri viwanja vya michezo navyo vilipiwe kwa utaratibu upi? Tuwaangalie hawa watu kwa sababu ni wawekezaji wa ndani na tuwasaidie; na kwenye maeneo ya Makanisa, maeneo ya Vyuo, hawa wamechukua jukumu la Serikali la kuelimisha Watanzania, kwa nini tusiwasaidie kama hatusaidii hata kulipa mishahara, watu hawa hata fedha ya kukaguliwa, kuletewa mitihani, wanalipa mitihani, kukaguliwa lakini hawajalalamika. Unaposema watu hawa wanachaji fedha, basi umchaji kodi, ujue ile kodi inapelekwa moja moja kwa Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba ndugu zetu wa ardhi, kwa sababu wao ni msingi mmojawapo wa maendeleo kwa hiyo wasiposimamia vizuri sera hii na wakaweka kodi za aina hii maana yake ni kwamba huo mhimili hautasimama vizuri na hatutaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Ameshamaliza muda wake; ahsante sana Mheshimiwa Jesca.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nakushukuru sana. Naomba hilo lishughulikiwe.