Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niwe mmoja wa kuchangia katika Wizara hii. Niungane na Wabunge wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaletea Watanzania maendeleo; na hata Tuzo aliyoipata hii ni heshima kwetu kubwa sana Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimpongeze sana Dokta, Waziri wa Ardhi kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na msaidizi wake Ridhiwani Kikwete, mchapakazi, songambele kazi ni nzuri, tunategemea atamsaidia Waziri kufanya kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo Watanzania. Vile vile Katibu Mkuu Kijazi na wasaidizi wake, wanafanya kazi nzuri katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee tu machache. Naishukuru Wizara ya Ardhi kwa kutupatia fedha za kupima ardhi, Halmashauri ya Mji wa Makambako, tunawashukuru sana mmefanya kazi nzuri na ndiyo sasa tunaendelea, lakini ombi langu kubwa Mheshimiwa Waziri, wako watu wanaokaimu katika nafasi mbalimbali sasa utendaji kazi unakuwa ni mgumu sana katika Halmashauri nyingi ikiwepo Halmashauri ya Makambako. Afisa Ardhi anakaimu zaidi ya miaka minne, tunaomba sasa athibitishwe ili kusudi afanye kazi yake kwa uhakika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wako watendaji ambao siyo waaminifu. Kwa mfano, kwa maksudi kabisa wako watu ambao wanatoa kiwanja kimoja zaidi ya watu wawili, hii ni hatari sana. Wanagonganisha jamii ya Watanzania watu waanze kuichukia Serikali bila sababu. Tunaomba watu hawa wanaotoa kiwanja kimoja zaidi ya watu wawili wachukuliwe hatua za kinidhamu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo tuna matatizo ya fidia, hasa nizungumzie Jimbo la Makambako, baadhi ya wananchi imefika mahali aidha warudishiwe maeneo yao. Kwa mfano, eneo la kwanza ambalo lina tatizo ni eneo la Polisi kwa hiyo, tunakuomba Waziri ukae pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani muone namna ya kuwapa fidia hawa wananchi, maana eneo hili limetwaliwa kwa muda mrefu hawajalipwa fedha zao na sasa hawawezi kuendeleza kufanya kitu chochote. Ninaomba sana kwamba, jambo hili liweze kutatuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya pili ni eneo ambalo lilikuwa lijengwe soko la Kimataifa pale kwetu Makambako. Fidia baadhi ya watu walilipwa, baadhi ya watu 18 hawajalipwa, Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo ilikuwa inashughulikia kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri mkae pamoja ili muweze kutatua tatizo hili la wananchi wa soko la Kimataifa pale Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni eneo la Idofi ambalo Serikali ilikuwa inajenga One Stop Center imeshalipa fidia zaidi ya Milioni Mia Nane na kitu, bado hela nyingine wananchi kwa muda mrefu hawajalipwa. Ninaomba ukae na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Mbarawa ili muweze kutatua tatizo hili wananchi waweze kufaidika na fidia yao ambayo wanaisubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho katika fidia ni suala la umeme wa upepo, wananchi wa Makambako wanapata shida sana maeneo yale tangu yametwaliwa. Nilikaa na Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Januari Makamba, alisema atalishughulikia. Sasa niombe mshirikiane ili wananchi hawa waweze, kama imeshindikana waweze kurudishiwa eneo lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri napenda niliseme, tunataka Wizara ya Ardhi isimamie mpango bora wa matumizi ya ardhi ili mara nyingine Rais wetu aweze kupewa tuzo ya Kimataifa kutokana na matumizi bora ya ardhi. Tuzo hii atakayoipata itategemea na uchapaji kazi wenu, tuzo hii itakuwa ni faida kwetu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja, Rais huyu wa Awamu ya Sita ni mteule na Mungu, huo ndiyo ukweli. Sasa siku nyingine nitawaambia kwa kirefu zaidi ili mujue huyu ni mteule na Mungu, leo naomba niishie hapa. Mheshimiwa Waziri chapa kazi, songa mbele, tuna imani kubwa na wewe na timu yako, pamoja na Naibu Waziri wako Mheshimiwa Ridhiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja ya ardhi. (Makofi)