Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata fursa ya kuweza kuchangia katika hoja ya Wizara hii, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu.

Naomba niungane na Wabunge wenzangu ambao wamepongeza hotuba nzuri, ninampongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa ujumla kwa kazi kubwa, nzuri, ambayo wanaifanya katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri akiwa Naibu Waziri, katika maeneo ambayo alipongeza kwamba, yamepimwa na kupangika vizuri ni pamoja na Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo, kwa maana ya Mji Mdogo wa Matai. Jitihada zile ambazo zilikuwa zimeonekena mpaka akasifia hapa katikati fedha hazijapatikana kwa hiyo, ule utaratibu uliokuwa ukitumika wa kuwezesha Halmashauri kupima maeneo yao vizuri naomba ile sifa ambayo alikuwa ametoa katika Wilaya yetu ya Kalambo kwa maana ya Mji Mdogo wa Matai isije ikaishia. Zile jitihada fedha ipatikane, tukipewa tunapima viwanja tunauza kwa wananchi na sisi tumekuwa waaminifu katika kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo napenda nimuombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Mifugo, washirikiane pamoja katika kutatua mgogoro wa Ranch ya Kalambo, hasa katika vijiji vya wananchi wa Katapulo, Kijiji cha Mimba, vijiji vingine vyote ambavyo vinazunguka ranch ya Kalambo ambavyo walitoa ardhi ile wakiamini kwamba, watakuwa wanaweza na wao kushiriki katika kufuga, kulima na kujifunza, lakini kwa bahati mbaya wamekuja wawekezaji ambao hakuna ambacho wananchi wa Mao, Mbuluma, wanaweza kujifunza. Kijiji cha Mbuluma na Mao wanakosa mpaka maeneo ya kuweza kuzika watu wao, ni wakati muafaka kwa Serikali kutizama namna gani itakavyowawezesha wananchi hawa kupata ardhi kwa ajili ya kilimo na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee eneo lingine ambalo linahusu Muhimili wetu, kwa maana ya Bunge. Katika Kamati yetu ya Bajeti tulitoa mapendekezo tukiwa tunaona upo umuhimu kwa sasa, eneo la Bunge kuongezwa kwa maana ya kutwaa maeneo jirani. Katika hotuba ile ambayo tulikuwa tunawasilisha kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwamba, Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Wizara husika waone utaratibu gani ambao utafaa, ili tuweze kutwaa maeneo yaliyo jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini upo umuhimu wa kufanya mambo haya? Kwanza ni suala zima la usalama. Bunge, kama Muhimili, ndiyo kama mti mkubwa ambao wananchi wote wa Tanzania wanatakiwa wakusanyike, lakini wametutuma sisi tukusanyike kwa niaba yao, kwa hiyo, eneo hili linahitajika kuwa na usalama. Maana sisi sote tunakubaliana kwamba, Mheshimiwa Rais ni sehemu ya Bunge na wakati mwingine anawaalika Marais wengine kuja kuhutubia Bunge hili, usalama ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haipendezi hata kidogo eneo muhimu kama hili likawa limezungukwa na maeneo mengine kama ambavyo ukienda upande huu unaambiwa kuna eneo la Soko la Mama Nchimbi, ukienda huku kuna Bohari, lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba, eneo lenyewe unapoliongelea ni square meter 41,678 ni sawasawa na hekta 4.2 ambazo tunazidiwa hata miongozo ambayo inatolewa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wanapotaka kujenga sekondari wanataka at least iwe eka 15. Sasa tunazidiwa hata na sekondari. Ni wakati muafaka kwa sababu, Bunge ndiyo tulitangulia Serikali ikafuata na sisi ni mashuhuda kwamba, ukienda kwenye Mji wa Serikali namna ambavyo maeneo yapo yakutosha na taasisi za Serikali zinaweza zikapewa huko ili mwananchi wa Tanzania akija kutafuta huduma aende kupata huko ambako uko Mji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipendeze kama ikikupendeza kwa wakati mwingine tena utoe maelekezo hoja hii irejee Kamati ya Bajeti, tuwe na wakati muafaka wa kujadiliana namna gani ya kuweza kutwaa maeneo haya na Bunge liwe na eneo lake kubwa la kutosha. Nimepata fursa ya kutembelea Mabunge mengine, nitolee mfano wa Bunge la kama Zambia, ukienda wana zoo ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wewe umekuwa ni shuhuda unahitaji wakati mwingine uende kushiriki shughuli za michezo, ukienda Jamhuri unaambiwa leo kuna tukio ambalo hutaruhusiwa Mbunge, unarudi kiunyonge, wakati katika hali ya kawaida sisi Wabunge tunatakiwa ofisi zote na huduma zote tupate tukiwa katika ukumbi huu na maeneo ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja pia ya kuwepo na hospitali yetu ya Bunge, tuna zahanati kwa Muhimili kama huu hailingani na hadhi yetu. Ifike wakati tuwe na eneo la kutosha, tuwe na hospitali yetu kubwa, nzuri, ili pale ambapo Mbunge anapokosekana kutibiwa hapa iwe ni ugonjwa ambao inabidi awe refereed kwa uhalisia, lakini kwa hali ilivyo tuna zahanati, imefika wakati tuwe na eneo la kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo taasisi za Serikali ambazo sidhani kwamba ipo haja hata ya kutoa fidia. Yapo maeneo makubwa huko nje ambako ndiyo wanatakiwa wakajenge ili kuboresha Mji, lakini ili kupisha Bunge, Bunge liwe na hadhi yake, juzi tulipata nafasi ya kutembelea Mahakama. Napongeza sana Mahakama wanajua kujinafasi, wamekuwa na eneo kubwa sana, tumeoneshwa mpaka sehemu ambayo kutakuwa na swimming pool, jambo ambalo kwetu sisi kila ukigeuka, ukienda nje huko ndiyo Wabunge wanalazimika ku-park magari yao, na siku za nyuma ilishawahi kutokea mpaka malalamiko Mbunge ame-park mara anakuta kuna kifaa kwenye gari lake kimeibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatakiwa kuwa na ofisi za Makamishna, Wenyeviti wa Kamati na huko mbele ya safari hata Kamati hizi zinatakiwa ziwe na kumbi zake za mikutano. Sisi sote ni mashuhuda hata canteen yetu tuliyonayo wakija wageni ukichelewa kidogo unakuta chakula hakuna, ifike wakati ikupendeze na nafasi uliyokalia utoe maelekezo ili tukutane na Wizara ya Fedha Kamati ya Bajeti, Wizara ya Ardhi na Wizara zote ambazo taasisi zake ziko hapa Jirani, tuweze kukaa tukiwa tumetulia tuone namna iliyo bora ya kutwaa maeneo haya ili Bunge liweze kujinafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipita huko nje msimu wa mazao unakuta kwamba, kuna Bodi ya Mazao Mchanganyiko, malori yanakuja kwa ajili ya kufanya shughuli ambayo katika hali ya kawaida shughuli hizo zilitakiwa zifanyike nje siyo karibu na Bunge. Usalama siyo mzuri kwa jinsi ambavyo tumezingirwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa sauti hii na jinsi ambavyo nimeona unatikisa kichwa utatoa maelekezo ili Bunge tukutane na Serikali kwa maana ya Kamati ya Bajeti tujadiliane namna bora, ili kama kuna maeneo ya kutoa fidia itolewe fidia stahiki, lakini Bunge kama Muhimili ambao unajitegemea ambao ndiyo muwakilishi wa wananchi Tanzania lipate hadhi yake na eneo ambalo linalingana na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)