Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Freeman Aikaeli Mbowe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nchangie hoja ya wizara hii. Nitachangia masuala machache sana, na suala la kwanza ambalo ningependa nimuombe kabisa Mheshimiwa Waziri aelewe, nitazuia mshahara wake; ni suala linalohusu uwanja wa ndege wa KIA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala limezungumzwa Bunge la Nane, Bunge la Tisa, Bunge la Kumi, leo tuko Bunge la 11. Nimeshasimama katika Bunge hili zaidi ya mara kumi nazungumza suala la KIA, lakini mimi sielewi Serikali yetu inafikiri nini na inataka nini, na sijajua ni nani hasa beneficiary wa ule uwanja wa ndege wa KIA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida ya wale wapya nitatoa historia kidogo tu kwa muda mfupi sana. Uwanja huu mliubinafsisha mwaka 1997 kwa kipindi cha miaka 25 kwa gharama ya dola 1,000 kwa mwaka. Mkamkabidhi mwekezaji eneo la kilometa za mraba 110, mkamkabidhi na uwanja mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika kuhusu ule mkataba wa KIA kwamba ardhi mliyoikabidhi kwa huyo mwekezaji ilikuwa ni ardhi iliyogusa Wilaya mbili; Wilaya ya Hai na Wilaya ya Arumeru katika Mkoa wa Arusha. Ni ardhi ambayo imegusa kata sita na vijiji 12. Sasa uwanja wa ndege ule umetumika kama vile hauna mwenyewe. Tumelalamika, tumeunda tume tumekwenda na Mawaziri KIA, lakini bado kuna sintofahamu haieleweki kuhusiana na uwanja ule; hatimaye Serikali ikakiri kwamba uwanja ule una matatizo, mkataba una matatizo; mwaka 2009 Serikali ikavunja ule mkataba.
Baada ya Serikali kuvunja mkataba wakadai kwamba wamerejesha uwanja wa Kimataifa wa KIA katika miliki ya Serikali. Lakini Serikali ikatoa kauli kwamba asilimia 90 ya masharti ya mkataba hayakutekelezwa, lakini kitu cha ajabu mkataba ulipovunjwa Serikali ikailipa fidia kampuni ambayo ilitakiwa kuwekeza pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yakalipwa mamilioni ya dola; na wakati wamiliki hao wanaendesha ule uwanja Serikali ilikopa kutoka kwenye European Development Bank zaidi ya dola milioni nne ambazo tunalipa Watanzania wote. Mimi najiuliza viongozi wetu wako wapi, yaani wanafikiri nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kichekezo kikubwa kuliko vyote ni hiki; baada ya ule uwanja kuwa umerejeshwa Serikalini, Serikali ikamuachia yule yule aliyekuwa anauendesha ule uwanja kazi ya kuuendesha ule uwanja. Ukiiuliza Serikali leo au hata Waziri, uwanja wa Kimataifa wa KIA unaingizia Serikali hii shilingi ngapi hawezi kukuambia jibu ambalo linaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na uwanja huu ambao mwekezaji yule yule wa KADCO ameachiwa, tunaambiwa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, viwanja vyote vya ndege nchi hii vinaongozwa na Taasisi inayoitwa Tanzania Airport Authority. Kama uwanja ni asilimia 100 mali ya Serikali ni kwa nini mnawaachia watu binafsi wanauendesha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na watu hao hao ndio wale ambao walishindwa kutekeleza asilimia 90 ya masharti ya mkataba. Sasa leo uwanja wa ndege wa KIA unatumia eneo la kilometa za mraba, nimesema umetengewa eneo la kilometa za mraba 110. Umegusa watu, makabila mbalimbali na eneo lile waliishi Wamasai kabla hata ya Uhuru wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika pale sio uendelezaji wa uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro, ni watu ndani ya Serikali wanaweka mikakati ya ku-grab ile land inayozunguka uwanja wa KIA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawapa takwimu ambazo mtaona miujiza ya Tanzania. Mojawapo ya viwanja ambavyo viko bize sana duniani ni uwanja Heathrow nchini Uingereza, (London Heathrow) ambao una terminal one, terminal two, terminal three, terminal four na wanakwenda terminal five and six.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa Heathrow London umejengwa katika eneo la hekta 1,227. Lakini uwanja wa KIA uki-compare na Heathrow, London eti Serikali inasema uwanja ule unahitaji hekta 11,085. Uwanja wa Heathrow kwa mwaka mmoja una handle flight na hizi ni data za mwaka 2014, 500,000. Uwanja wa KIA kwa mwaka mzima una handle flight 7,800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja Heathrow kwa mwaka mzima unapitisha passengers milioni 75, uwanja wa KIA comparatively unapitisha abiria 820,000. Uwanja huo wa Heathrow unaotumia hekta 1,200 unapitisha tani 1,420,000 za cargo lakini uwanja wa KIA unapitisha tani 3,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema vijiji vinavyozunguka uwanja ule, vijiji vya Mtakuja, Tindigani, Sanya Station, Rundugai, Chemka, Majengo katika Jimbo la Arumeru, Samaria, Malulu na Maroroni upande Arumeru, haya maeneo yanatakiwa Serikali iweke mpango chini yarejeshwe kwa wananchi, wananchi waishi kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja wa KIA hauhitaji kilometa za mraba 110 kwa ajili ya kujenga uwanja haiwezekani, ni matumizi mabaya ya ardhi na wizi wa ardhi ya wananchi na mnajua kabisa mikoa ya Kaskazini ardhi ni tatizo kubwa kweli kweli. Hilo ni jambo la kwanza ambalo ningependa sana kulizungumza kuhusiana na mpango wa KADCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, barabara. Kuna barabara moja inajengwa, kwanza Waheshimiwa Wabunge nieleze jambo moja hapa. Kuna dhana ambayo inajengeka kwamba kuna barabara zinajengwa sana Kilimanjaro au pengine Kaskazini, ni kweli na napenda nikiri kuna mikoa yenye uhaba mkubwa wa barabara na ni lazima tupige sana kelele ili tupate barabara za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata huku Kilimanjaro hali sio shwari mnavyofikiria na naomba nitoe takwimu kwa Jimbo langu kwa mfano; barabara ya kwanza ya lami ilijengwa mwaka 1966, barabara ya kilometa 12, kwa miaka 40 haikujengwa barabara nyingine. Barabara iliyofuata kujengwa ilijengwa wakati ya awamu ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alitoa ahadi ya kujenga barabara inayoitwa Kwa Sadala - Masama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo imejengwa tangu mwaka 2010, kilometa hizo 12.5 hazijakamilika mpaka leo. Sasa kama tunaweza kujenga kilometa 12.5 kwa miaka sita ni dhahiri kwamba wajenzi (contractors) wanalipwa fidia kubwa kwa ajili ya interest kwa sababu ya kukaa site kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niiombe Serikali kwamba wamechukulia suala la ujenzi infrastructure kama priority ni jambo jema kwenye uchumi, lakini absorption capacity inanitia wasiwasi kidogo. Kwa idadi ya fedha iliyopelekwa katika Wizara hii, kwa idadi ya miradi ambayo itatakiwa kutekelezwa katika Wizara hii, ni lazima Serikali na Wizara hii iangalie uwezo wake wa kuweza ku-absorb kiwango hiki cha fedha otherwise mnaweza mkatoa room kubwa sana ya ubadhilifu na wizi wa fedha kupitia miradi mbalimbali ambayo inategemewa kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza kwa haraka sana ni reli ya kaskazini. Ni kweli reli ni kitu muhimu kwa nchi nzima kila mahali, nina-understand, lakini hii reli ya northern line tusiipuuze kwa muda mrefu kwa sababu hata kidogo kilichobakia pale kitapotea. Kwa hiyo, naungana Waheshimiwa Wabunge wa Tanga katika kilio chao, kwamba tunapofikira reli tusifikirie tu central line, tuiimarishe central line, tuimarishe TAZARA, tujenge reli ya kusini na vilevile northern line ambayo tayari ilikuwepo tusiipoteze ile reli kwa sababu itakuja kutugharimu fedha nyingi sana kuijenga wa mara nyingine.