Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara ya Ardhi, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa tuzo alizozipata, lakini pia kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM anayoendelea nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimpongeze Waziri wetu kwa kazi kubwa anayofanya kwenye wizara hii lakini nimpongeze Naibu Waziri shemeji yangu kwa namna ambavyo wanasaidiana na qaziri kusogeza gurudumu hili kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitazungumza polepole sana kwa sababu nina jambo kubwa ambalo ningetamani Mheshimiwa Waziri lifikie mwisho sasa, jambo hili ni mgogoro wa KIA. Mgogoro huu upo kati ya uwanja wa KIA na wananchi waliopo kwenye eneo lile na kihistoria sote tunafahamu uwanja ule ni miongoni mwa uwanja mkubwa wenye eneo kubwa kuliko viwanja vingine Tanzania. Uwanja wa kwanza ni KIA ambao una hekta 11,085 ukifuatiwa na Dodoma, Songwe halafu wa Dar es Salaam ni wanne lakini uwanja huu ulipatiwa hati yake tarehe 20 Aprili, 2006.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati uwanja huu unapata hati hizo kijiji cha Sanya Station ambacho kina hekta 221.3 kilikuwa kimeshasajiliwa tarehe 18 Agosti, 1976 kwa barua yenye Kumb. Na. KM/VC.295 wakati huo huo kijiji cha Tindigani kilikuwa kimesajiliwa tarehe 1 Februari, 1999 kwa barua yenye Kumb. Na. KM/KGI/477 na eneo lake lilikuwa ni hekta 12,000.37.8. Kijiji cha Mtakuja kilikuwa kimesajiliwa tarehe 18 Agosti, 1976 kwa barua ya Kumb. Na. KM/KG/285 na ukubwa wake ulikuwa ni hekta 3,859.8. Kijiji cha mwisho ni Chemka kijiji hiki kilisajiliwa tarehe 1 Februari, 1999 kwa barua Kumb. Na. KM/KG/504 ukubwa wa eneo hili ni hekta 778.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kilichotokea ukitazama ni kweli kabisa sisi wananchi wa Jimbo la Hai tunapenda sana uwanja wa ndege wa KIA na tunauhitaji sana hatuna shida kwenye hilo, lakini tunafahamu kwamba vijiji hivi vilikuwepo mgogoro huu umetengenezwa na Serikali yenyewe ndiyo waliotoa hati kwenye vijiji na ndiyo waliotoa hati kwenye uwanja wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe sana kwa dhati wananchi wale waliopo pale KIA wanapata taabu, wanaishi kwa mashaka mashaka juzi hapa mliona walienda kuwekewa alama ya “X” bila kushirikisha hata viongozi, nikauliza swali humu nikapewa majibu kwanini wamefanya hivi, tukasema jambo hili lisijirudie tena, lakini nimeambiwa hapa Mawaziri nane walitembelea Mkoa wa Kilimanjaro bahati nzuri baad ya kuzua taharuki kubwa wananchi wananipigia simu Mbunge tunakuja kuondolewa vijiji vyetu vinafutwa, nikakuona Mheshimiwa Waziri ukanisaidia kutoa ufafanuzi kwamba hapana, hatujafikia hapo jambo hili lipo chini ya Mkuu wa Mkoa.

Sasa mimi niwaombe kwa namna ambavyo nimefanya vikao na uongozi wetu wa Mkoa, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa anayodhamira ya dhati ya kumaliza tatizo hili, tafadhalini sana sisi tunaenda kurudi chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kukaa na wananchi kwa kushirikisha viongozi waliopo kule niwepo mimi Mbunge, Diwani, Wenyeviti wetu wa Vijiji na Vitongoji lakini Malaigonan wenzangu (viongozi wa kimila wa Kimasai) ambao ndiyo wengi kwenye eneo lile tushirikiane tuweze kumaliza jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe utakapohitimisha hoja yako uje na kauli thabiti kwenye jambo hili kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, mshauriane ili utoe sentensi wananchi wale wapumue. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri jambo hili linanitesa kwelikweli nanila muda mrefu. Wananchi wa Hai narudia tena wanajua umuhimu wa uwanja wa ndege hilo halina shida wapo tayari kukaa mezani tuzungumze tukubaliane hii ya leo tunaahirisha kila siku mgogoro unazidi kukua na watu wanazidi kuongezeka kwenye eneo lile. Mimi niombe ifike mwisho utakapokuja kuhitimisha hapa njoo na majibu jambo hili tunalihitimishaje ndani ya mwaka wa fedha unaokuja tumalize jambo hili na mama yangu kama unanipenda hili jambo ndiyo litakalonisaidia tuendelee kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa kazi kubwa waliyoifanya watu wa Hai miaka 15 wakaachana na yale mambo, wakakubali Serikali ya Chama cha Mapinduzi ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura moja ya jambo kubwa alilosema ni mgogoro huu, mgogoro huu usipokamilika pale mnatuingiza kwenye matatizo Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mgogoro huo mkubwa kuna migogoro mingine midogo midogo ambayo mimi naamini Mheshimiwa Waziri hii unaimudu; kuna mgogoro wa shamba namba 240 na 242 Lafofo pale, hili unaliweza ukitenga siku mbili au tatu ukaja ndani ya Jimbo la Hai hii migogoro yote unayoitaja hapo utaimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mgogoro mwingine wa wananchi ambao walitoa eneo lao kwa ajili ya kuruhusu Halmashauri ya Wilaya Hai ijengwe pale, bado wanadai eneo lao, wamezungushwa muda mrefu, wameandika barua muda mrefu, mwisho wa siku ikakubalika kwamba wizara ndiyo isaidie kulipa kwasababu Halmashauri ya Hai haiwezi kulipa fidia ile.

Mimi niombe na hili Mheshimiwa Waziri ulibebe wapo wananchi 19 wakiongozwa na Mzee Philemon Mushi wanahangaika kutwa na matatizo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mgogoro mwingine pia mdogo malalamiko ya wananchi ambao walikuwa wanafanya kazi pale Lambo Estate, wengine walipewa maeneo wengine hawakupewa, Mheshimiwa Lukuvi mzee wangu na mentor wangu alianza vizuri sana kazi hii niombe ukamilizie mgogoro huu uishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mgogoro mwingine huu mgogoro ni kati ya Kijiji cha Uduru na Kijiji cha Mshara na hili tunashindwa kulifanya kule kwetu, ni bahati mbaya sana mwenzangu aliyenitangulia alitoka Kijiji cha Mshara mimi natoka Kijiji cha Uduru, nikienda kuzungumza kuhusu mgogoro huu kunaonekana kuna mgongano wa maslahi. Mimi naomba nikubalie level ya wizara ishuke itusaidie kumaliza hapa, kuna wananchi wengi wameweka majumba yao wamekeza miradi yao hawapati hati kwa sababu ya mgogoro huu na ni mgogoro mimi naamini ukishuka wewe mwenyewe pale unahitaji masaa mawili kumaliza huu mgogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme la mwisho katika kuhitimisha tuna mashamba 17 ya ushirika; tumeshazungumza na Waziri wa Kilimo vizuri, niombe atakapokuja mezani kwako tutakapoanza ku-review upya mikataba ile na wewe utoe baraka zako na mwisho maombi ya Chemka…

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)