Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Shabani Omari Shekilindi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja ambayo ipo mezani kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nilitaka kusimama na kutoa mwongozo kwa jambo linaloendelea kutokea kule jimboni kwangu, panya road wameingia kule na taarifa nilizozipata juzi na jana naambiwa wameshaua watu watano. Kwa hiyo, naomba Serikali itoe maelekezo juu ya suala hili ili liweze kukomeshwa mara moja, wananchi wangu waendelee kuishi kwa amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwanza kabisa nimpongeze Rais wetu Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hizi tuzo alizopata. (Makofi)

Ndugu zangu nataka niwaambie mtu mmoja alienda kwa Mtume akamwambia Mtume hivi ninani wa kufanyia hisani au wakumtanguliza kumfanyia hisani basi Mtume akamwambia mama; kisha baada ya mama Mtume akarudia tena akasema mama, ehee baada ya mama akarudia tena Mtume akasema mama. Kwa hiyo, mama ametajwa mara tatu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Baba?

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, baba ametajwa mara moja. Kwa hiyo, ona ukubwa wa Mungu ona akina mama walivyopewa uwezo mkubwa mpaka Mwenyezi Mungu anajua mpaka Mitume inajua kwamba mama ndiyo kila kitu kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini soma hata Surat Mariam utakuta mama bora ametajwa kwamba ni Mama Mariam ndiyo mama bora na mwanamke bora. Kwa hiyo, ndugu zangu hii tuzo aliyopata mama usije ukasema ni ya kwanza hii ndiyo imeanza zitakuja nyingi na nyingi zaidi kwasababu hii ipo kwenye mikono ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nimpongeze mama yangu Waziri wa Ardhi, Mama yangu Mabula kwa kazi kubwa anayoifanya, nimpongeze Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na watalaamu wote, kwa kweli wanafanyakazi kubwa, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Mama mimi sina mashaka nae kwa sababu ninyi wenyewe mmeyaona kwamba wakati wa Mheshimiwa Lukuvi ulikuwa unafanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lukuvi amemrithisha mama na tunamuona mama anaenda site.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye mchango wangu sasa. Kwanza nianze kuishukuru Serikali imetupa shilingi milioni 208 Halmashauri ya Lushoto kwa ajili ya kupima viwanja na kazi ile inaendelea vizuri, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, lakini pia fedha hizi ninazoomba naomba mtoe maelekezo kwa sababu yanayofanyika kule ni tofauti, kule wale wanaoenda kupimiwa hawana elimu yoyote, sasa unakuta wale ambao wanapima wanapita juu juu tu, mara siku moja, siku mbili tayari ina maana lile lengo halitimii. Kwa hiyo, niombe maelekezo yatoke kwa ajili ya watu wale wapewe elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapo hapo nichangie mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, tumezunguka karibia nchi nzima hii tumeona changamoto, changamoto kubwa iliyokuwepo ni kwamba sheria hizi zinakinzana na nimeona kwenye taarifa ya Waziri kwamba Sera ya Ardhi inakuja. Sasa niombe sheria hii iharakishwe haraka sana ili kuweza kunusuru kwa sababu sasa hivi tukisema kwamba tunamlaumu maana kila lawama inakwenda kwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, TAMISEMI inasheria zake, Madini inasheria zake, Kilimo inasheria zake, Mifugo inasheria zake, Maji inasheria zake, na Maliasili inasheria zake, lakini lawama ikitokea inatupiwa kwenye Wizara ya Ardhi. Mimi niombe sera hii ije haraka sana Sera ya Ardhi sheria hii ije haraka sana iletwe Bungeni ili tuweze kuipitisha ili tumpunguzie uzito, mzigo mama yetu Mama Angelina Mabula, Waziri wetu wa Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili kuna hizi Halmashauri kukopeshwa fedha, zinakopeshwa fedha mwisho wa siku hazirejeshi zile fedha kwa wakati, baada ya kupima viwanja na kuuza viwanja Halmashauri badala ya kurejesha fedha Wizarani basi wanabaki nazo na wanatumia kwa matumizi mengine, hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali sasa kwamba ikiwezekana kuwe na mkakati maalumu wa kurejesha fedha hizi kwa wakati ili fedha hizi zikirejeshwa na wengine waweze kupata na hii itakuwa salama sasa kwa kuharakisha kupima vijiji vyetu kwa uharaka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hii asilimia 30 ambayo ipo kisheria kwamba mtu anapopewa mradi Halmashauri husika basi asilimia 30 iende Serikali kuu mimi niishauri Serikali kwamba asilimia 30 hizi zirudi kule kule pamoja kwamba zipo kisheria lakini sheria ile iletwe tui-review, tuifanyie amendment ili fedha hizi ziweze kurudi kule kule Halmashauri. Sasa hivi tunalalamika kwamba vijiji vyetu havipimwi, tunalalamika kwamba ina maana upimaji umekuwa ni mdogo sana, lakini fedha hizi zikirudi tayari zitaenda kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Shekilindi mtaalamu wa dawa za Covid.

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)