Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, jana sikupata nafasi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa tuzo aliyopata kama mwanamke wa kwanza na ambayo imetuheshimisha sana sisi Watanzania, lakini pia imeendelea kuifanya Tanzania kuonekana kwamba kidiplomasia tunaendelea kunawiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais alisema yeye hastahili tuzo ile, mimi naomba kusema kwamba kama tungepata Rais asikubali kuendeleza yale ambayo alikuwa anaendeleza Rais mtangulizi, maana yake angeanzisha ya kwa kwake mengine leo tungekuwa na migogoro kwenye miradi mingine iliyokuwa inaendelea. Kwa hiyo, mimi nampongeza sana kwa kuyaendeleza yote na kwa juhudi kubwa na kwamba tuzo hiyo inamstahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku mbili zilizopita nilisema kwamba Geita Mjini tulikamilisha uandaaji wa master plan na master plan ya Geita Mjini tuliikamilisha mwaka 2020 na ilitugharimu zaidi ya shilingi milioni 400. Sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri kuwa na master plan ni jambo linguine, ninaona bado maoteo ya makazi yaholela yanaendelea kuwepo katika maeneo ya mengi ya mji pamoja na uwepo wa master plan kwa sababu maeneo mengi ya miji pamoja na kuwa na master plan yanachelewa sana kupimwa na matokeo yake yasipopimwa watu wanajijengea vyovyote vile na baadaye tunashindwa kupitisha miundombinu.

Kwa hiyo, juhudi zilizoanza za kutoa fedha katika baadhi ya Halmashauri na tunaipongeza Serikali kwa juhudi hizo tunaomba atukumbuke na atupatie pia Geita Mjini tuweze kupima maeneo yote ili kuweza kuepuka mji ule kuja kujengwa holela. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeomba kuchangia kwa jambo moja mahsusi tunazo sheria mbili, Sheria ya Madini inatoa surface right kwa mtu mwenye leseni ya kuchimba na anapopewa surface right anatakiwa kwa mujibu wa Sheria za Ardhi aidha, awafidie wananchi walioko pale au amalizane nao ili kuweza kumiliki eneo lile.

Sasa tumekuwa na mgongano wa Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi kwenye Mji wa Geita, tunayo mitaa saba; Mtaa wa Katoma, Mtaa wa Compound, Mtaa wa Nyamalembo, Mtaa wa Samina, Mtaa wa Nyakabale na Mitaa ya Katumaini ambayo kwa miaka 23 imeshindikana kuwapimia wale wananchi waweze kupata hati, tuweze kupitisha miundombinu kwa sababu wanapokwenda kuangalia kwenye kumbukumbu wanakuta kwamba eneo lile linamilikiwa na mgodi, lakini kimsingi mgodi unamiliki surface right. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alikuja Mheshimiwa Waziri akiwa na Kamati ya Mawaziri wa Nane, Mheshimiwa Lukuvi, akatoa agizo kwa Kamishna wa Ardhi wa Mkoa ambaye anafanya kazi yake vizuri sana, Mheshimiwa Waziri naomba nikuhakikishie Kamishna anatoa ushirikiano mzuri sana, anafanya kazi yake vizuri sana na ametusaidia sana kumaliza migogoro kwenye eneo letu lile pale. Lakini tumeshindwa kuendelea mbele kwa sababu inaonekana kisheria eneo lile ambalo tayari lilikwishatolewa haki ya kumilikiwa na watu wa mgodi haliwezi kumilikishwa tena kwenye mamlaka zingine kwa watu wengine kwa wamiliki wengine wananchi wa Jimbo la Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokumilikishwa kwa wananchi kwa eneo hili kunasababisha adha nyingi chache zifuatazo; tunazungumzia maeneo ambayo yako kwenye kata tatu ambayo yanahitaji shule, lakini huwezi kwenda kujenga shule kwenye eneo ambalo huwezi kulipima, tunazungumzia maeneo ambayo wananchi wapo wamekutwa na mgodi, lakini ni katikati ya mji hatuwezi kupima kuwapa hati waweze kutumia hati kujiendeleza na kupata mikopo kwa sababu kila unapotaka kwenda kupima watu wa ardhi wanasema mchoro unagongana na mchoro mwingine kwa hiyo, haiwezekani kupima. Lakini siyo hivyo tu maisha ya wananchi katika mitaa hiyo kila siku polisi wanapita, kila siku mgambo wanapita, kwa hiyo, ukichimba choo unaonekana unachimba madini, ukiwa na mifugo umeingia kwenye eneo la mgodi, ukilima unaonekana umeingia kwenye eneo la mgodi. Wananchi wameishi kwa mateso makubwa kwa takribani tangu mwaka 1999. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kwamba sheria zetu zinauwezo wa kulimaliza jambo hili haiwezekani jambo moja Rais wa sasa akiwa Makamu wa Rais alikuja akalitolea maagizo, akaja Hayati Rais Magufuli akalitolea maagizo, Mawaziri wote waliopita kwenye Wizara hii wanakuja kutoa maagizo lakini jambo haliishi. Nafahamu juhudi za Mkuu wa Mkoa ameitisha kamati mbalimbali, amekutanisha watu wa TAMISEMI, wamekuja watu wa madini, wamekuja watu wa Wizara yako lakini bado hatufiki mwisho. Ni jambo gani hili halifiki mwisho!

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu mimi haki ya wananchi wale kumiliki ardhi ni haki yao ya kiasili, walikutwa pale na mgodi, mgodi ukapewa leseni, hatuna tatizo na mgodi tunaupenda, kama wanapenda kumiliki lile eneo basi tuko tayari lile eneo wawalipe fidia wananchi waweze kulichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama lile eneo bado hawajafikiria kuliendeleza watuache tulitumie tunavyotaka mwisho wa siku wakilihitaji waje watulipe. Haiwezekani kwa miaka 20 umeweka matangazo hamruhusiwi kujenga eti leo katika nchi yangu ardhi, ya kwangu nikitaka kujenga lazima nikaombe kibali mgodini ndiyo sheria inavyosema.

Mheshimiwa Waziri nimesimama kuchangia jambo hili, ninaamini ofisi yako ina uwezo wa kulimaliza kisheria, kwa kutumia sheria zilizopo na kama hazipo tuangalie upya sheria zetu ili tuweze kumaliza jambo hili, ni kikwazo kikubwa sana kwa maendeleo ya wananchi wa mitaa saba ya Mji wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Serikali imeridhia kuwaachia zaidi ya vijiji na vitongoji 900. Sasa kinachonisikitisha kidogo, Kata yangu ya Mgusu, Mitaa ya Nyakabale pamoja na Manga…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu ahsante kwa mchango mzuri sana, kengele ya pili.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)