Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naitwa Hawa Mwaifunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na nimeweza kusimama tena katika Bunge hili na mimi niweze kuchangia hoja ya Wizara hii ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Wabunge wenzangu wametangulia kuzungumza nami naomba niseme mambo yafuatavyo; naomba na mimi nijielekeza kwanza kwenye hii Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume hii kwangu mimi ndiyo niliona muarubaini wa kupunguza migogoro ya ardhi katika nchi hii. Lakini tume hii ina sheria nzuri, tume hii imejiandaa vizuri katika kutekeleza majukumu yake, tume hii ina kiongozi mzuri ambaye ni Profesa na maandiko yao ni mazuri kabisa ukiyaona kwenye makaratasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini changamoto kubwa iliyopo ni ukosefu wa fedha. Haiwezekani nchi hii ikatulia, nchi hii ikapata amani ya migogoro kama tume hii haijaingia kazini kwenda kupanga matumizi ya ardhi kwenye vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwenye Ilani yenu ya Chama cha Mapinduzi mmesema angalau kila mwaka vijiji 750 viende vikapimwe. Leo mnatoa fedha ya vijiji 100 vikapimwe, hivi vijiji 3,000 ambavyo mnasema ndani ya miaka mitano viwe vimeshapimwa vitafika lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu mnapotoa fedha huwa mnaangalia kwanza Ilani halafu ndiyo mnakwenda kutoa fedha. Sasa kwa nini hii tume imewekwa nyuma wakati imo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi? (Makofi)

Kwa hiyo, niombe sana kama ambavyo wenzangu wamesisitiza, tunaomba sana Kamati ya Bajeti, Serikali, Waziri wa Fedha wakae, waangalie namna bora ya kuweza kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mama Mabula aweze kufanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu inafika mahali Wabunge tunashindwa kuzungumza vizuri kwa sababu tutasema nini wakati huyu mama bado hajapewa fedha? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Ndiyo.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hebu mpeni fedha, halafu ashindwe kufanya kazi ili tusimame hapa tuseme. Kwa sababu sasa hivi hata tukisema tutakuwa tunamuonea na huku ndiyo kwenye eneo mahususi ambalo anaweza kufanya kazi vizuri na kwenda kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwepo. Wanapambana sana kupunguza hii migogoro. Leo kuna Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya, kuna Mabaraza ya Ardhi ya Kata, kama hii tume ikiwezeshwa hata haya mabaraza yatakuwa hayana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na huku kwenye mabaraza kesi nyingi sana unazokutana nazo za migogoro ya ardhi wengi wanaoteseka ni wakinamama tena wajane. Ifike mahali tuwaonee huruma hawa wanawake, kwanza wamefiwa na wanaume zao, lakini pili bado wanapambana na migogoro hii ya ardhi. Kila siku kwenda na kurudi kwenye haya Mabaraza ya Ardhi kwa kweli ni mtihani mkubwa. (Makofi)
Kwa hiyo, niombe sana na mimi kama Mjumbe wa Kamati hii na tulishaomba na ninarudia tena, bila fedha hizi kuwapa hawa tume, hakuna kitu kitakachoweza kufanyika kupunguza migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe shilingi bilioni 10 walizoomba siyo nyingi, ni hela kidogo sana kama alivyozungumza ndugu yangu jana hapa, ni hela kidogo sana ambayo Serikali haishindwi kutoa hii fedha ili hawa Mawaziri na watendaji wao waende wakafanye kazi. Tunahitaji angalau vijiji 750 angalau viweze kupimwa jamani tupunguze hii migogoro kupangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumekwenda Singida Vijijini, Kijiji cha Ntondo na Kijiji cha Nkwae tumejionea wananchi wale wakiwa na furaha baada ya kupangiwa maeneo yao. Kwa hiyo, sasa hivi hakuna mtu anayeweza kwenda kuvamia pale Nkwae na Ntondo. Kwa sababu wale wananchi wameshatengenezewa mazingira mazuri na kila unayemuuliza anakwambia hapa ni hiki, hapa ni hiki, hapa ni hiki, hapa ni hiki. Nani atakuja kuvamia? Ili tupunguze hata mauaji ya wakulima na wafugaji? Tupange matumizi bora ya ardhi, hakuna mtu atakayeweza kuja kuvamia kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Mawaziri Nane; mimi nipo kwenye Kamati ya Ardhi na tuliomba hapa na kuna mwenzetu mmoja aliomba mwongozo. Kamati hii ilikuwa haijawahi kutoa taarifa, tulivyoomba walikuja wakatupa taarifa kidogo. Kwa taarifa ile ambayo wametupa, ninachokiona badala ya kwenda kutatua changamoto za migogoro ya ardhi tumekwenda kufukua moto ambao sijui huko mbele hali itakwenda kuwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri nane wanapokwenda kwenye Majimbo ya watu na kwenye Mikoa ya watu waonane na wananchi na siyo kuishia kwenye Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, waende kwa wananchi. Wanakwenda kwa wananchi wakikuta sehemu imetulia, lakini wakikuta sehemu moto unafuka, hawaendi wanaishia kwenye Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Inawezekana kabisa hii Kamati ya Mawaziri Nane ikawa ni mwiba mchungu kwa wananchi kuliko ilivyo kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa dada yangu Angeline Mabula mkienda kule, nendeni mkawaone wananchi waambieni ambacho mnakwenda kukifanya. Zile kamati zetu ndogo mnazoziacha kule chini ndiyo mwiba mchungu kwa wananchi na kila siku nawaambia mtakuja kukuta mambo ambayo hamkuyategemea huko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la kurasimisha. Hili jambo sisi labla pengine kama Wajumbe wa Kamati tunaweza tukawa tumelielewa na baadhi ya Wabunge. Lakini wananchi huko hawalielewi hasa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam. Naomba sana watakapokuja ku-windup hapa waeleze hili zoezi la kurasimisha lina maana gani na nini kifanyike ili wananchi wale waweze kulielewa, vingingeno mtakuwa mnatangwa maji kwenye kinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba. Wizara hii inahitaji wafanyakazi. Waongezewe wafanyakazi ili kazi ziweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa kuliko ilivyo hivi sasa, wafanyakazi ni wachache, kazi ni nyingi, wanahitaji kufanya mbambo mengi kuliko uwezo walionao wa wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la mwisho naomba nijikite kwenye Mkoa wangu wa Tabora, hususan kwenye Manispaa ya Tabora Mjini ambako mimi ni Diwani kwenye Manispaa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Tabora Mjini waliamua kutoka mjini na wakaenda kwenye eneo la nje ya mji ambalo linaitwa Ndevelwa. Eneo lile limepimwa viwanja na wananchi wamepewa hati. Lakini watu wa TARURA mpaka sasa bado hawajapeleka miundombinu ya barabara ili wananchi wale waweze kuonyeshwa maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Ardhi mshirikiane na Wizara ya TAMISEMI, watu wa TARURA wapeleke barabara ili wananchi waweze kuoneshwa maeneo yao. Haiwezekani mtu ana hati mkononi halafu eneo lake halijui, eneo langu ni lipi. Kwa hiyo, naomba sana watu wa Wizara hakikisheni wananchi hawa wanajua ili watu waweze kulipia zile hati, tuweze kupata fedha kwa ajili ya kutatua migogoro iliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naliomba, naomba sana na naomba nisisitize sana kwa Wizara, fanyeni ukarabati kwenye nyumba za National Housing, yamekuwa kama magofu, tumechoka kuona hali hizi ikiwemo kwenye Manispaa yangu ya Tabora, yaani zile nyumba zimezeeka pamoja na kwamba Tabora ni mji mkongwe lakini tunaomba mtusaidie zile nyumba zenu pale ziko nyingi lakini zote hazifai zimechakaa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Ahsante kwa mchango. Ahsante, unga mkono hoja.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Unga mkono hoja.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi/Kicheko)