Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie kwenye hoja iliyopo mezani. Namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye anaendelea kutupa baraka zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayofanya, tulizoea huko nyuma, Wizara hii ilikuwa ni Wizara ya migogoro sana, lakini kadri siku zinavyokwenda tunaona mabadiliko makubwa sana, hongereni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri haya nitakayoyasema sio mageni kwa Wizara, ni mambo wanayoyafahamu naomba wayashughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni tatizo la mpaka kwenye ukanda wa bahari, Mheshimiwa Waziri ulifika Mkinga tukaenda Jasini unajua kilichotokea, tuliingia kwenye nyumba pale, upande mmoja ni Mkinga upande mmoja ni Kenya. Kwa hiyo, changamoto ile unaifahamu. Katika eneo lile hasa kwenye ukanda wa bahari wavuvi wetu wanapata shida kubwa, kila unapoenda kuvua wanaambiwa wameingia kwenye eneo la Kenya, mali zao zinachukuliwa, boti zao zinachukuliwa, wanapelekwa Kenya wanafunguliwa kesi kule. Hiki kimekuwa ni kilio cha muda mrefu cha watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali twendeni tukaweke mipaka twendeni tukaweke maboya yale yaliharibika ili mpaka ule ujulikane kinagaubaga tuondoe tatizo la watu wetu. Pale Jasini askari wa Kenya wanaingia mpaka Tanzania wakikamata watu, hebu tulishughulikie tatizo hili kwa haraka kabla halijaleta madhara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni tatizo la migogoro ya vijiji na vijiji katika Wilaya ya Mkinga, hili nimelileta kwa maandishi muda mrefu na chanzo cha migogoro ile ya vijiji na vijiji, ni ramani iliyotolewa mwaka 2007 wakati Mkinga inamegwa kutoka Wilaya ya Muheza. Zoezi lile halikuwa shirikishi, wanakutwa kijiji kimoja kijiji cha upande wa pili uongozi haupo, wananchi hawakushirikishwa, kwa hiyo tumezalisha migogoro karibu kila kata, kata na kata kijiji na Kijiji. Naomba hili lichukulieni kwa umuhimu mkubwa twende tukaondoe tatizo lile, kama ni kutafsiri ramani ile twendeni tukatafsiri kwa wananchi wale tuondokane na migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamefikia sasa wanashikiana mapanga huko, tusisubiri watoane uhai twendeni tukashughulikie tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo ambao tuliomba shamba la Kwantili ambao limetelekezwa kwa zaidi ya miaka 20, shamba ambalo hata ulipaji wa ada ya kodi pale anayemiliki halipi sawasawa, tumeomba shamba hili lifutiwe hati. Shamba lenye Hati Na. 47 22 lenye ekari 58 na shamba lenye Hati namba 14501 lenye ekari 2,841 tulitoa ilani mwaka jana baada ya kugundua kwamba mwenye shamba huyu alienda kukopa nje ya nchi na hati zile alizigeuza kuweka dhamana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilani ile imetolewa tangu mwaka jana, imeiva mwaka jana mwezi wa tisa mpaka leo hatujui nini kinaendelea! Mheshimiwa Waziri hili unalifahamu tuliteta kule Tanga Kamishna wa Ardhi alisema anakwenda kuliangalia, hatujapata majibu, tunaomba mtusaidie tufute shamba hili ili ardhi ilejeshwe kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni lile linaloshughulikiwa na timu ya Mawaziri mlipokuja kule Tanga tulieleza, eneo la Kimuni mgogoro ule tulikwisha ushughulikia kwa kina mwaka 2016; Wizara ilituma timu kikosi kazi kikafanya kazi ile tukafanya kazi nzuri ya kushiriki, mikutano ya hadhara na wanavijiji tukafika makubaliano, timu ya uongozi wa mkoa iliyohusisha Mkuu wa Mkoa, Wabunge wa Wilaya zinagusa maeneo haya tulikuja Wizara ya Maliasili tukakubaliana. Tunaomba mnapoenda kufanya maamuzi mapendekezo yale yazingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa upande wa kule Maramba kuna ahadi ya Waziri Mkuu kwenye shamba la Mwele, Waziri Mkuu alishaahidi wananchi wale watapatiwa ardhi kutokana na changamoto kubwa ya ardhi, tunaomba ahadi ile ya Waziri Mkuu ipewe umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)