Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. OLIVER D. SUMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza kwa kukushukuru kwa namna ambavyo umekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha Bunge letu tukufu linatimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali ili iweze kutimiza wajibu wake kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda ninaomba nianze moja kwa moja kutoa mchango wangu kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mchango wangu unaanza kwa kuishauri Serikali kuwekeza nguvu kubwa katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Maafisa Ardhi katika Wilaya zote na mikoa yote nchini ili waweze kupata ari na ubunifu wa kuweza kutimiza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi kirefu tumekuwa tukishuhudia migogoro mingi ya ardhi ambayo mara nyingi imetokana na Idara ya Ardhi na Mipango Miji katika maeneo mengi ya nchi hii kushindwa kutimiza majukumu yao kwa ufanisi kutokana na ufinyu wa bajeti na vitendea kazi katika Idara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengi ningependa kuiomba Wizara ya Ardhi kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yote yanayozunguka Hifadhi za Taifa nchini pamoja na maeneo yenye miradi ya kimkakati. Kwa kufanya hivyo itapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi ambayo tumekuwa tukiishuhudia mara kwa mara pale wananchi wanapoamua kuvamia maeneo ya mapori ama Hifadhi za Taifa kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Wilaya ya Ngara ambayo imepakana na Mapori ya Akiba ya Kimisi na Burigi kunahitajika kuwekwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuweza kuwanufaisha moja kwa moja wananchi wa Wilaya ya Ngara hususani wakazi wa vijiji vya Rusumo, Mshikamano, Kasulo, Rwakalebela, Keza na Kazingati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naiomba Wizara ya Ardhi kukaa pamoja na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kuandaa mpango huo wa matumizi bora ya ardhi ambao utahusisha kutenga baadhi ya maeneo kwa matumizi ya kilimo, ufugaji, uwekezaji viwanda pamoja na utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ningependa kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi kuandaa mpango bora wa matumizi ya ardhi hususani kwa Wilaya ya Ngara eneo la Mgodi wa Tembo Nickel. Kutenga maeneo matatu maalum kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kama kilimo, ufagaji pamoja kuanzisha mpango wa kuinua hadhi ya Kijiji cha Bugarama kilicho eneo jirani ya mgodi huu ili kiweze kuwa na hadhi ya kibiashara.