Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge nianze kwa kumshukuru Mungu kwa fursa ambayo ametupa hadi tunafikia hatua hii tunapokwenda kuhitimisha hoja yetu. (Makofi)

Aidha, niungane pia na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa tuzo aliyoipata. Naomba niishie hapo kwa sababu pongezi nyingi zimetolewa lakini nia na dhamira ya dhati sana ni kwamba kuhakikisha watanzania kwamba tunaye Rais ambaye anafanya kazi na kazi hiyo inatambulika katika ulimwengu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge 27 waliochangia kwa kuzungumza na Wabunge wawili wamechangia kwa maandishi, kwa sababu hoja ni nyingi na nyingi zinahitaji maelezo ya msingi ili muweze kuzielewa vizuri tutaleta pia kitabu ambacho kitakuwa kinaelezea hoja moja baada ya nyingine. (Makofi)

Kwa hiyo kwa nafasi hii niliyopewa ya dakika 20 nitakwenda kujibu hoja chache ambazo zinahitaji maelezo ili tuweze kuona jinsi gani tunafahamisha kikao chako hiki cha Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyopigiwa kelele sana na Waheshimiwa Wabunge hasa ile pia ya Mawaziri Wanane katika vile vijiji 975. Kama nilivyosema kwenye hotuba yangu tunastahili sana kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu vijiji vile 975 angekuwa ni Rais ambaye si msikivu asingeridhia vijiji 920 kuweza kuridhiwa na kurasimishwa na kupewa watu na tukumbuke katika changamoto hiyo ambayo ipo maeneo mengi ambayo yana migogoro kuna muingiliano wa matumizi ya ardhi unakuta kuna maeneo ambayo yalitengwa kwa ajili ya hifadhi lakini kutokana na sababu pengine ziwezi kusema zilisababishwa na nini tukajikuta tena tumeingia katika mgogoro mwingine wakuhalalisha vijiji ndani ya maeneo ambayo tayari yanahifadhi. Kwa hiyo, hapo ndipo mgogoro ulipoanzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika utatuzi maelekezo ndani ya Serikali ni kwamba lazima tuangalie vijiji ambavyo havina athari viweze kurasimishwa lakini tukumbe katika vijiji hivi 920 vinarasimishwa, vinavyobaki 55 shughuli inaendelea ya kufanyia tathimini. Tukumbuke katika hivi vijiji 55 tunayo miradi mikubwa ya kimkakati ambayo iko kwenye maeneo hayo, nikichukulia mfano wa Bwawa la Mwalimu Nyerere wote lazima tujiulize hivi lile bwawa kama halitaweza kupata maji ya kutosha na pesa yote iliyowekezwa pale maana yake Serikali itakuwa imepoteza fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza lile bwawa ambalo mwisho wa siku litakuwa halifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maeneo yale yamezungukwa na watu ambao wanafanya kazi katika vyanzo vya maji ambavyo vinazuia maji kwenda katika ule mkondo ambao unapelekwa kwenye bwawa. Kwa hiyo, Serikali imejikita katika kufanya tathimini ya kina athari ambazo zinaweza kusababishwa na watu kuwepo na shughuli za kibinadamu na wakati huo huo bwawa linategemea maji yale. Kwa hiyo, kinachofanyika pamoja na Mawaziri Wanane kwenda kazi ya mikoa, lakini tukumbuke ile mikao saba au nane ya mwanzo Kamati ile inakwenda kwenye vijiji inaongea na wananchi na baadaye inakuja inawaachia mkoa kwendelea na hile shughuli na timu ya wataalamu inabaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukihesabu vijiji hivyo kama ngazi ya Taifa peke yake ndiyo itakuwa inakwenda kwenye maeneo, hiki tunachokipigia kelele cha migogoro itachelewa kutatuliwa kwa sababu siyo rahisi ngazi ya Taifa kwenda vijiji vyote na ukamaliza, tunaachia mamlaka ya mkoa, wanaofahamu maeneo yao, wanaoweza kuzungumza na watu pale na ambapo hata sisi tumeshatoa maelekezo.

Kwa hiyo tunachofanya kama Serikali ni kuwataka mamlaka zilizoko kwenye maeneo ambayo bado yanafanyiwa tathimini kuweza kuangalia uhalisia wakisaidiwa na wataalamu wetu, uhalisia wa maeneo yale yaachwe kama yalivyo, wananchi waendelee kufanya shughuli zao au kuna haja ya kuwaondoa wananchi maeneo yale ili miradi ile iwe salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hiyo tathimini yake bado inaendelea, kwa hiyo, mpaka sasa hapa ninapozungumza siwezi kukwambia nani na nani ataondoka pale ni mpaka ile tathimini ikamilike na wataalamu wapo. Na mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, pesa nyingi mnahidhinisha kwa ajili ya miradi ya kitaifa, sasa tukiidhinisha pesa halafu sisi wenyewe tukataka kukwamisha mwisho wa siku tutakuwa tunapoteza nguvu ya umma lakini tutakuwa tunapoteza pesa ya Serikali kwa kukwamisha miradi ambayo tunajua kabisa ni vielelezo kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niwaombe katika hivyo vijiji ambavyo tathimini inaendelea muwaamini viongozi wenu ndani ya mkoa, muwaamini viongozi wenu ndani ya Serikali hakuna utatuzi utakaokwenda kufanyika bila kushirikisha wananchi, wananchi watashirikishwa sehemu zote na maelekezo ya Serikali ndivyo yalivyo.

Kwa hiyo, tulikuwa tunakwenda kwa ajili ya kutoa maelekezo naomba sana hili lieleweke kwa sababu limechukua kidogo wazungumzaji wanaotoka katika maeneo hayo wamezungumza sana. Ikiwemo na GN 28 ambayo ni kati ya yale ambayo yanakwenda kufanyiwa kazi ukanda huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa suala la fidia, suala la fidia limekuwa ni changamoto na kizungumkuti katika maeneo mengi. Tunazo taasisi nyingi zinazodaiwa, Waheshimiwa Wabunge hapa wametaja baadhi, wametaja maeneo ambayo yamechukuliwa kwa muda mrefu na wengine wanasema karibu miaka 20, 25 lakini fidia hailipwi na tayari watu pale wanaathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke mwaka 2017 tulipitisha sheria hapa tukaipitia ile Sheria ya Fidia ambayo ilikuwa haina muda maalumu ambayo ilikuwa inaonesha kwamba watu wakitaka kutwaa eneo kama hajalipa fidia ndani ya muda kadhaa aweze kuendelea mwananchi na shughuli yake. Tulipitisha hapa kwamba ni ndani ya miaka miwili kama mlipa fidia hajalipa mwananchi anaendelea na shughuli yake, lakini hiyo ilikuwa yale maeneo ambayo yametwaliwa kwa sasa na kila baada ya miezi sita anakuwa charged na interest kama hatalipa.

Kwa hiyo, mimi niwatake mashirika yote na taasisi zote pamoja na wawekezaji ambao wanachukua maeneo ya wananchi kulipa fidia kwa wakati, vinginevyo Serikali haitakubali na hata kwenye hotuba yangu nimesema kama taasisi ya ushirika haijajiandaa katika kulipa fidia wasichukue maeneo ya watu, hilo ndiyo tunalolizungumza kwa sababu tunaleta kero ndani ya Serikali lakini unapotaka kufanya mradi lazima uwe umejiandaa kuhakikisha kwamba utalipa fidia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo yaliyotajwa ya EPZA tayari Serikali imeshaanza kuyachukua baadhi ya maeneo ili mengine yanagaiwa wananchi, lakini pia nitoe tahadhari kule ambako maeneo yanarejeshwa tuweze kuweka mpango mzuri wa matumizi ili basi ardhi ili itufae katika matumizi. Kwa mfano maeneo ambayo yanakuwa yana mashamba, Wabunge wengi mmeomba mashamba wametaja Mbunge wa Mkinga kule ametaja na wengine wametaja kwamba kuna maeneo ambayo yapo tu yamekaa likiwepo shamba la Efatha limetajwa kwamba halijaendelezwa.

Naomba niseme ya kwamba maeneo ambayo yanaumiliki sahihi wa kisheria, taratibu zile za kuyatwaa lazima zizingatiwe. Kwa hiyo, inapofikia mwisho anayekwenda kubatilisha umiliki huo ni Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, ikienda kwa Mheshimiwa Rais na Waziri akimshauri Mheshimiwa Rais kubatilisha kama Mheshimiwa Rais akiona hii inafaa atafanya na kama alivyofanya na mpaka na kufuta yale mapori 12 ambayo wananchi wamepangiwa.

Kwa hiyo katika ufutaji au katika utwaaji lazima sheria zinafatwa. Kuna maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wanalalamikia kwamba yamekaa idle na watu hawaendelezi lakini ukiangalia taratibu za kuanza kufuta ukienda kwenye Sheria Na. 4 ukianzia kile kifungu cha 45 unakwenda mpaka kifungu cha 48 kuna taratibu zote zimewekwa. Kuna kumpa onyo akajibu, kuna kumwambia ajirekebishe, kuna kumpa notice yakumnyang’anya. Sasa usipofuata taratibu zile huku Wizarani hatuwezi kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais kufuta, lazima taratibu zifatwe na wengine wanatoa Ilani halafu wanatulia, sasa sisi huku Wizarani au Serikalini hatuwezi kuja kukupangia wewe nani anyang’anywe wewe uliyekaa kule ndiyo Mamlaka za Upangaji wa Miji, angalia taratibu zako zote kisheria zimezingatiwa, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kuna mengine yanakuwa yana migogoro kwenye Mahakama mfano mzuri shamba la Efatha linalozungumziwa, Serikali na Mheshimiwa Naibu Waziri amelijibu pale. Lakini Serikali ilishafanya kazi yake vizuri na Mahakama ikatimizwa wajibu wake na hii ni Mihimili mitatu iliyo tofuati. Kama kuna agizo la Mahamaka sisi hatuwezi kuliingilia kwa sababu tunaheshimu ule Muhimili. Lakini bado tulifanya mazungumzo na wenzetu wa Efatha na wakaridhia ekari 3,000 kutoka kwa ajili ya kugawia vile vijiji vitatu vinavyozunguka pale.

Kwa hiyo kazi inayotakiwa kufanyika pale ni zile ekari 1,000 waweze kuonyeshwa. Lakini utaratibu wa kusema unamnyang’anya kwa sababu tayari shamba lile lilipata nadhani hati yake kwenye mwaka 1997, kijiji au vijiji vimekuja kuandikishwa mwaka 2007 vimeandikishwa ndani ya umiliki wa muhusika. Sasa pale inakuwa ni vigumu vinakinzana katika namna vyote vimetoka Serikalini halafu wananchi wanabaki wanaangalia. Lakini kwa kuona tatizo hilo ambalo tayari lilionekana ndiyo maana Serikali ilichukua uamuzi wa kuzungumza naye ili aweze kuridhia ekari 3,000 zitolewe wananchi wapewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii inakuwepo kwa sababu tu namna ambavyo tunaishi kule katika maeneo na wawekezaji na namna ambavyo wawekezaji wasivyokuwa waaminifu katika kutimiza masharti ya hati wanazozimiliki. Kwa hiyo, ndiyo changamoto kubwa ambayo sasa Wizara yangu itaendelea kuangalia kwa kina na naagiza katika kikao hiki Halmashauri ambazo ni Mamlaka za Upangaji fanyeni ukaguzi wa maeneo yote ambayo wawekezaji wamepewa na muangalia masharti yake kama yametimizwa kama hayajatimizwa taratibu za kuwanyang’anya zianze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tutakapokuwa tumewanyang’anya kwa mfano kwenye mashamba tusikimbilie kupanga viwanja, kuna maeneo wanataka kwa ajili ya kupanga tukipanga viwanja maana yake tutajikuta tunakosa hata maeneo ya kilimo. Kilimo cha mjini kinakubalika, kwa hiyo chukua eneo, panga maeneo yako kama yameshavamiwa na watu tutapanga makazi ambayo hayajavamiwa basi wekeni kile kilimo cha mjini ili walau wananchi waweze kupata maeneo ya kuendelea kuwa na kilimo. Sasa leo ukimnyang’anya mmiliki aliyekuwa analima, halafu wewe ukaweka majengo tu maana yake utakuwa hujaisaidia Serikali. Kwa hiyo, naomba kusema kwamba taratibu zizingatiwe na tuone jinsi ambavyo tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mheshimiwa Mwita Waitara ambalo amelizungumzia eneo lake ambalo amelisema la Kijiji cha Komarero ambalo lina jumla ya ekari 652 tayari katika eneo lile lina wananchi 6,847 tathmini ilishafanyika na fidia imeshalipwa kwa watu 1,515 kati ya hao 6,847. Na katika kijiji kingine ambacho amekitaja cha Kewanja tayari kazi ya tathmini inaendelea kule, tatizo linalokuja ni katika lile eneo ambalo mwekezaji alitaka kulichukua akiwa na mawazo ya kuwa na ile open pitch process za kuchimba, baadae akabadilisha mawazo akasema anakwenda kwenye underground, akaamua kuacha. Serikali hatujakaa kimya tumefanya mazungumzo naye ili aone namna gani, kwa sababu wananchi wale walisimama kwa muda mrefu kuweza kuendeleza maeneo yao kwa sababu alionesha nia ya kulichukua. Lakini kashindwa kulichukua pengine kwa sababu amebadilisha, badala ya kuwa na open pitch sasa anakwenda na underground kwenye uchimbaji wa madini.

Kwa hiyo, tumemtaka pengine aweze kuona namna ya kulipa walau fidia kidogo kwa wale aliowachelewesha, lile amelichukua na amepeleka kwa mshauri wake anasubiri kushauriwa namna ya ambavyo ataweza kuwalipa kwa sababu kosa ni la kwake na siyo la wananchi amewachelewesha katika maendeleo yao. Kwa hiyo, hayo yote yanafanyika kwa kuangalia ni namna gani tunaweza kusuluhisha haya mambo yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumzia suala la kupanga, kupima na kumilikisha na hiyo ndiyo hoja ya msingi zaidi pengine ningetaka Waheshimiwa Wabunge tuichukue vizuri na tuone namna gani tunafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu ni Wizara ambayo inasimamia, inatunga sera, Miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia katika taaluma yake au sekta ambayo inaiongoza. Mamlaka za Upangaji zote ni Halmashauri kwa mujibu wa Sheria Namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007. Takwa hili la kisheria si mamlaka zote za Halmashauri zinalitekeleza Serikali imeingilia kati kutaka kuongeza ile kasi pengine ya upimaji ili kupunguza malalamiko ya wananchi na ndiyo maana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan tunamshukuru sana kwa kutoa ile shilingi bilioni 50 ambayo tumekwenda kuikopesha katika Halmashauri 55 lakini kuna pesa nyingine ambayo imetoka bilioni tano ambayo imekwenda kufanya kazi ile ile. Lengo letu ni kutaka kusaidia kusukuma kwenye mamlaka husika ambayo ndiyo hasa inayotakiwa kufanya kazi ya upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya Wizara kusaidia mamlaka zote zimetulia kama vile ile ni kazi ya Wizara. Mkitulia na kuachia Wizara maana yake ni kwamba tutachelewesha wananchi kuweza kupata umiliki ya maeneo yao na kuwajengea uwezo kiuchumi. Ninyi wenyewe hapa mmesema sekta ya ardhi ni sekta ambayo tukiweza kuisimamia vizuri itakwenda kunyanyua uchumi wa kila Mtanzania. Lakini tunaisimamiaje kama hatuwezi kuwamilikisha wananchi na kuwapa uwezo wa kutumia miliki zao kwenda kukopa benki.

Kwa hiyo niwatake sana Mamlaka za Upangaji watimize takwa lao la Kisheria sisi kama Wizara tutaendelea na ule mfuko ambao tulikuwa tukiutumia katika kukopesha bado tumeendelea kumuomba Mheshimiwa Rais kwamba tuweze kurejeshwa ili tuongeze ile nguvu ambayo tunaweza kusaidia. Rai yangu kwa Halmashauri zinapewa pesa Wakurugenzi wanatumia tofauti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ni sehemu ya Baraza la Madiwani mnapokuwa kwenye vikao watakeni Halmashauri zenu wawaoneshe matumizi ya pesa waliyopewa kwa ajili kupanga, kupima na kumilikisha ili tuweze kuona ile kasi tunaenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo tunawataka pia kumekuwa na changamoto pengine ya pesa tunasema wanapouza wanakuwa na pesa nyingi za kutosha, basi katika zile pesa wanazozipata waweze kugawa kulingana na madaraja ya Halmashauri zetu. Watenge kati ya asilimia 40 mpaka 60 ya pesa zile wanazozipata faida kwenye mauzo zikaendeleze sekta ya ardhi badala ya kuzitumia kwenye matumizi mengine. Tukifanya hivyo tutajikuta kasi imeongezeka na tunatambua sana katika suala hili kama Halmashauri zingeweza kutenga walau vijiji au hasa vijiji vitano, 10 kila mwaka tungeweza kusogea mbele. Lakini hawafanyi kazi hiyo wanaangalia Tume, Tume iko kwa ajili ya kuwezesha katika kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo Tume inaingia pia katika suala zima la kupanga mpango mzima wa matumizi ya ardhi ikiwa pia ni kuhakikisha Halmashauri zinajengewa uwezo kupitia zile Kamati zake waweze kuendelea na hili zoezi.

Kwa hiyo, mimi niwaombe Halmashauri waone kwamba hili pia ni jambo la msingi kama Serikali tunatakiwa kulifanya kwa pamoja ili tuweze kuona tunakwenda namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika masuala mengi ambayo yamezungumzwa limezungumzwa suala la hatimiliki za kimila kuweza kukopa benki. Naomba niseme tu kwamba tunao mfano mzuri Halmashauri ya Mbinga, Bariadi, Babati na nyinginezo ambazo zimetumia hatimiliki za kimila kuweza kukopa benki, tatizo lililopo tu hapa ni la kisheria ambalo kama Mheshimiwa Kakunda alivyosema tutakwenda kuiangalia sheria. Kwa sababu hairuhusu mtu mmoja anapojisikia kwenda kupima aende apime, lazima mamlaka zinazohusika ziweze kufanya kazi hiyo.

Kwa hiyo tutaiangalia ile sheria tuweze kuona ni jinsi gani tunaweza tukaweka utaratibu ambao utaongeza kasi ya kumiliki, kwa sababu sasa hivi mtu akitaka kupima anaambiwa pengine apime na wanakijiji wenziwe wote kitu ambacho kinakuwa ni gharama ambacho pengine yeye hawezi. Lakini kama Halmashauri zetu zingefanya kazi hiyo zingeweza kutusaidia sana. Kwa hiyo mimi niombe tu hayo yaweze kufanyika ili tuweze kuona ni jinsi gani tunakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uwekezaji limezungumzwa hapa Mheshimiwa Chumi amezungumza na nimpongeze kwa kutenga eneo la industrial park sisi kama Wizara tayari tumeshatenga hekta 224,000 tukiwa tumejiweka tayari kwa sababu tunafahamu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ameshatuelekeza, Wizara iwe tayari wawekezaji wanapoingia maeneo yawepo. Niwaombe tena Mamlaka za Upangaji, Mamlaka ambazo zimeshaandaa mipango kabambe kwa ajili kutenga maeneo kwa matumizi hakikisheni maeneo yale yanakuwa na umiliki either imilikiwe na Halmashauri au imilikiwe na Halmashauri ya Kijiji au Halmashauri yenyewe kwa maana ya kwamba mwekezaji anapopatikana asianze tena kusubiri mchakato wa uhaulishaji kama ni eneo la kijijini, lakini kama ni la mjini basi tujue umiliki uko kwa nani ili mwekezaji anapokuja anakwenda moja kwa moja tayari kwa mmiliki na wanakubaliana namna ya kulitoa lile eneo. Mwekezaji akija mpaka twende kijijini tuweke vikao tunachelewesha kitu ambacho Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan hataki kusia hayo. (Makofi)

Kwa hiyo mimi niwaombe sana katika hili Mamlaka za Upangaji zione haja ya kuona ni jinsi gani tatakwenda kutatua tatizo hili kwa sababu tunajua ni hitaji nchi imefunguka na wanahitaji kuwa na wawekezaji wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mengine nitayaruka lakini nizungumzie suala la National Housing; limezungumzwa suala la nyumba zimechoka ni kweli nyumba nyingi, lakini tukumbuke mwaka jana tuliripoti hapa walikuwa wameshaweka mpango kwa ajili ya kufanya ukarabati na walitenga shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuendelea kufanya ukarabati katika majengo yao 300 ambayo hasa yapo katika Mkoa ya Kilimanjaro, Mtwara, Katavi na Tabora itaingia katika mwaka huu wa fedha. Ni kweli yako yamechoka, lakini tunaamini, mmempongeza pia na Mkurugenzi Mkuu ninaimani kwa usimamizi wake atakwenda kufanya kazi yake vizuri. Na majengo yale ya uwekezaji ambayo yamezungumzwa yalikuwa yamesimama kwa muda mrefu tayari Serikali ilisharidhia ili waweze kuendelea kuyakwamua na kuendelea kuweza kuendelea nayo kama kitega uchumi. (Makofi)

Kwa hiyo, tusema haya yote tunayachukua tukitambua ya kwamba tupo pamoja katika kuhakikisha kwamba kila ambalo mnaelekeza, kila ambalo mnashauri tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii wameelekeza mambo mengi ushauri wao wameutoa tumeupokea kwa jinsi walivyoutoa, lakini niwahakikishie tu siku zote tumekuwa tuko pamoja katika hili. Tuzungumzie suala la kutofikia malengo katika ukusanyaji, kama ambavyo property tax iliingia kwa watoaji huduma sisi Wizara tunataka pia kuzungumza na watoa huduma kama wa maji ama TANESCO. Mtu ambaye anayetakiwa kulipa kodi pengine ya 300,000 kwa mwaka ukiagawa kwa miezi 12 utasikia ni kidogo sana. Kwa hiyo, tunajaribu kuangalia namna itakavyokuwa mbali na hiki ambacho amekizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ile mifumo yetu pia itakwenda kuongeza kasi ya makusanyo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunawezesha mfuko mkuu wa Serikali kupata kile ambacho Mheshimiwa anakihitaji. Tusipo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa toa hoja.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU SPIKA: Umejibu vizuri sana, toa hoja. (Makofi/Kicheko)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba tumeyachukua, tutayafanyia kazi, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.